Yanga hii… Tabu iko pale pale

YANGA imesharejea nchini kutoka Afrika Kusini ilipoenda kuweka kambi ya siku 10, ikicheza mechi  tatu za kimataifa za kurafiki, ikuiwamo kubeba ubingwa wa Kombe la Toyota, huku mastaa wapya wakimpa kiburi kocha Miguel Gamondi.

Katika mechi hizo tatu dhidi ya FC Augsburg ya Ujerumani, TS Galaxy na Kazier Chiefs za Afrika Kusini, kocha Gamondi alionyesha kiburi kwa kutumia vikosi tofauti, akithibitisha hata msimu ujao mambo yanaweza kuwa balaa zaidi ya msimu uliopita kwa mziki alionao.

Katika mechi ya Augsburg alianza na mseto wa wachezaji wa kigeni na wazawa, lakini katika mechi ya Galaxy alianza na wazawa watu kabla ya kuwaingia wageni baadaye na mwishowe akamalizia na mseto na kubeba ubingwa kwa kishindo ikiifumua Kaizer kwa mabao 4-0.

Clatous Chama, Prince Dube, Jean Baleke, Duke Abuya, Chadrack Boka, Abubakar Khomeiny, Aziz Andambwile ndio waliongizwa kikosi na wote wameonyesha moto wakishirikiana na waliosalia katika msimu uliopita walipotetea ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kwa msimu wa tatu mfululizo.

Katika mechi hizo zote ikianza ile dhidi ya timu ya Ujerumani na kulala 2-1, kisha kushinda 1-0 kwa Galaxy na ile ya 4-0, Yanga ilionekana kuwa moto zaidi, kwani kila mchezaji alionyesha uwezo na kumfanya Gamondi kuonekana kusuuzika roho na kuwasifia mastaa wa timu hiyo.

Hata chini ni dondoo ya kambi hiyo ya Sauzi na kilichoonekana kabla ya timu kurejea nchini kujiandaa na Kilele cha Wiki ya Mwananchi kinachofanyika keshokutwa Jumapili ikivaana na Red Arrows ya Zambia.

Katika siku 10 za kambi ya muda mfupi huko Afrika Kusini ilipoweka kambi maalumu ya kujiandaa na maandalizi ya msimu mpya (pre season), huku ikitwaa ubingwa michuano ya Kombe la Toyota Cup 2024, baada ya kuifunga, Kaizer Chiefs mabao 4-0.

Yanga imepata taji la kwanza baada ya ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Kaizer Chiefs katika michuano ya kombe la Toyota Cup 2024, ikiwa ni sehemu ya kudumisha uhusiano mkubwa wa kibiashara baina ya timu hizo ulioanza tangu mwaka jana. 

Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Prince Dube dakika ya 24, Clement Mzize dakika ya 62 huku Stephane Aziz Ki akipachika mawili dakika ya 45 na 62, yaliyotosha kuipa ubingwa wa kwanza kikosi hicho kinachojiandaa na msimu ujao.

Uhusiano huo ulianzia tangu mwaka jana ambapo Kaizer ilipata mualiko wa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Yanga katika kilele cha ‘Wiki ya Wananchi’ ambapo wenyeji walipata ushindi wa 1-0, lililofungwa na nyota Mzambia, Kennedy Musonda.

Kabla ya mchezo huo, ikiwa Afrika Kusini Yanga ilianza kushiriki michuano ya Mpumalanga Premier international Cup 2024 ambapo ilianza kwa kichapo cha mabao 2-1, dhidi ya Augsburg inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani maarufu ‘Bundesliga’.

Baada ya kichapo hicho, Yanga ikasawazisha makosa hayo kwani mchezo uliofuatia dhidi ya wenyeji, TS Galaxy ya Afrika Kusini ilishinda bao 1-0, lililofungwa na nyota mpya wa timu hiyo, Prince Dube aliyejiunga nayo msimu huu akitokea Azam FC.

Bao alilolifunga mshambuliaji, Prince Dube katika mchezo dhidi ya Kaizer Chiefs, limemfanya nyota huyo kuendeleza ubabe kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi aliyeteuliwa hivi karibuni baada ya kuachana na FAR Rabat ya Morocco.

Kichapo cha Kaizer ni cha kwanza kwa Nabi tangu ateuliwe huku Dube akiendeleza rekodi mbaya kwa kocha huyo kwani kabla hapo alianza kumfunga mechi yake ya kwanza tu wakati anajiunga na Yanga, kipindi hicho akikichezea kikosi cha Azam FC.

Wakati Nabi anajiunga na Yanga Aprili 20, 2021, akitokea Al-Merrikh SC ya Sudan, mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Azam FC Aprili, 25, 2021, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo alipoteza bao 1-0, lililofungwa pia na Prince Dube.

Hata hivyo, licha ya kuanza kwa kichapo hicho ila Nabi alitengeneza ufalme ndani ya Yanga kwani kuanzia hapo, timu hiyo ilicheza jumla ya michezo 49 ya Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza yaani (‘Unbeaten), ikiwa ni rekodi katika kikosi hicho.

Nabi mwenye uraia wa Tunisia na Ubelgiji, aliachana na Yanga Juni 14, 2023, baada ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo kisha kuipeleka fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo.

Katika kipindi cha miaka miwili, Yanga imekuwa na rekodi nzuri na timu za Afrika Kusini kwenye michuano mbalimbali ya kiushindani na kirafiki, jambo linaloonyesha kikosi hicho kinazidi kuimarika chini ya Kocha Muargentina, Miguel Gamondi.

Mei 10, 2023, Yanga ilicheza na Marumo Gallants katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kushinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Stephane Aziz Ki na Bernard Morrison.

Katika mchezo wa pili uliopigwa Afrika Kusini Mei 17, 2023, Yanga ilishinda kwa mabao 2-1, yaliyofungwa na Fiston Mayele na Kennedy Musonda huku la Marumo likifungwa na Ranga Chivaviro, hivyo kuipeleka timu hiyo fainali kwa jumla ya mabao 4-1.

Msimu huo ndio ambao utakumbukwa zaidi kwa mashabiki wa Yanga kwa sababu timu hiyo ilipoteza fainali kwa faida ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger, baada ya kupoteza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa mabao 2-1 na kushinda Algeria kwa bao 1-0.

Mbali na mchezo huo, ila Yanga ilikutana na Kaizer Chiefs Julai 22, 2023 katika kilele cha ‘Wiki ya Mwananchi’ jijini Dar es Salaam ambapo ilishinda bao 1-0, lililofungwa na Mzambia, Kennedy Musonda akipokea pasi ya Maxi Mpia Nzengeli.

Pia msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali, ilikutana na Mamelodi Sundowns ambapo miamba hiyo ilishindwa kutambiana nyumbani na ugenini na ndipo mikwaju ya penalti ilipoamua na Yanga kutolewa kwa kuchapwa 3-2.

Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya TS Galaxy na 4-0, mbele ya Kaizer Chiefs iliyoupata Yanga, inaonyesha ni wazi timu hiyo kwa hivi karibuni imekuwa tishio ndani na nje ya nchi huku ikichagizwa na ubora wa wachezaji ambao imekuwa ikiwasajili.

Ukiachana na Dube ambaye tayari ameshafunga mabao mawili akiwa na kikosi hicho tangu asajiliwe, ila miongoni mwa nyota ambaye hakutarajiwa kufanya vizuri na ameshabadilisha upepo kwa mashabiki wa timu hiyo ni kiungo Mkenya, Duke Abuya.

Abuya aliyejiunga na kikosi hicho akitokea Singida Black Stars, ni miongoni mwa sajili ambazo hazikuzungumzwa sana ila tangu ametua Jangwani tayari Kocha Mkuu, Miguel Gamondi amemuamini huku akitishia nyota wengine akiwemo, Mudathir Yahya.

Moja ya usajili mkubwa ambao mashabiki wa Yanga wanautegemea ufanye makubwa ni wa kiungo mshambuliaji Mzambia, Clatous Chama aliyetoka Simba ingawa bado hajaonyesha kitu kikubwa kilichotarajiwa, japo ni mapema kwa sababu msimu haujaanza.

Wengine ni nyota wa zamani wa Simba, Jean Baleke aliyetokea Al-Ittihad SCS Tripoli ya Libya, beki wa kushoto, Chadrack Boka (FC Saint Eloi Lupopo), kipa, Khomeiny Abubakar (Singida BS) na kiungo, Aziz Andambwile kutokea Fountain Gate FC.

Rais wa Yanga Injinia Hersi Said anasema, kambi ya Afrika Kusini imekuwa na manufaa makubwa kwao, japo mwanzoni ilikuwa ngumu kwa kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi kukubali mualiko huo, kwani alitaka kikosi hicho kibaki Dar es Salaam.

“Kocha wetu Miguel Gamondi mwanzoni hakutaka kabisa timu itoke nje ya nchi kwa sababu alitaka ikae sehemu moja tulivu ya kujiandaa na michuano ijayo, ingawa tunashukuru alikubali na mwenyewe amekiri amefaidika na maandalizi tuliyoyafanya.”

Related Posts