Afya ya akili inavyostawisha, kudhoofisha unyonyeshaji

Dar es Salaam. Afya ya akili kwa mjamzito na mama anayenyonyesha inaelezwa na wataalamu wa afya kuwa ni muhimu kuzingatiwa, kwa sababu katika kipindi hicho, mama hupitia mabadiliko mbalimbali ya kimwili, kiakili na kihisia.

Katika kuthibitisha hilo, Mwananchi imezungumza na baadhi ya wanawake wanaopitia hali hiyo, akiwamo Salma Suleiman, mkazi wa Kigogo jijini Dar es Salaam, ambaye anasema alipitia changamoto ya kukosa maziwa kutokana na kupata msongo wa mawazo baada ya kuachana na mumewe.

“Miezi michache baada ya kujifungua, mume wangu aliniacha, nikaachishwa kazi siku chache baadaye.

“Nilianza kuona utokaji wa maziwa unapungua na nilipozungumza na mtaalamu wa afya, alinishauri kupunguza msongo wa mawazo.”

“Haikuwa rahisi, lakini kupitia ushauri wake nilifanikiwa na baadaye maziwa yaliendelea kutoka vizuri, hadi leo mwanangu ana mwaka mmoja na ninaendelea kumnyonyesha,” anasema Salma.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwanamke mmoja kati ya watano hupata tatizo la afya ya akili wakati wa ujauzito au ndani ya mwaka mmoja baada ya kujifungua.

Kwa mujibu wa tovuti ya The Breastfeeding Network, inaonyesha kuwa asilimia 20 ya wanawake wanaopata ujauzito hupatwa na changamoto mbalimbali za afya ya akili, ikiwemo msongo wa mawazo ambao baadaye husababisha sonona katika kipindi cha uzazi ambayo kitaalamu hujulikana kama ‘Postpartum Depression’.

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa katika tovuti hiyo mwaka 2014, wanawake watatu kati ya watano waliacha kunyonyesha watoto kabla ya wakati kutokana na changamoto mbalimbali za afya ya akili pamoja na msongo wa mawazo.

Daktari wa Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Kanda Mbeya, Dk Raymond Mgeni anataja mambo yanayoweza kusababisha mama kupata changamoto ya msongo wa mawazo pamoja na sonona katika kipindi cha uzazi ni pamoja na migogoro katika familia pamoja na mahusiano, kufiwa na mwenza, kukataliwa kwa mtoto na mwenza au familia yake.

Pia anataja sababu nyingine zinazochangia mhusika kupitia katika matukio ya ukatili, ugumu wa maisha na matatizo mengine ambayo huweza kusababisha mama kupata msongo wa mawazo.

“Changamoto hizo huweza humfanya mwanamke kupata msongo wa mawazo katika kipindi cha ujauzito au mara baada ya kujifungua na asipopata msaada huweza kusababisha sonona,” anasema.

Tovuti ya jjbreastfeeding inataja mambo mengine yanayoweza kumweka mama katika msongo wa mawazo ni pamoja na wasiwasi kama ataweza kuwa mama bora na kumlea mtoto vizuri.

Pia namna gani anaweza kumudu malezi na shughuli nyingine kama vile biashara, kazi, majukumu ya kifamilia, pia mabadiliko ya maumbile kama vile matiti, mwili mara baada ya kujifungua, hasa kwa wanawake ambao wamejifungua kwa mara ya kwanza.

Kufuatia hilo, Dk Mgeni anasema mwanamke aliyekumbwa na changamoto hiyo huweza kuonyesha dalili mbalimbali, ikiwemo mfadhaiko, vipindi virefu vya huzuni, kupoteza hamasa ya kumhudumia mtoto, kuwa na uchovu.

Pia anaweza kuonyesha kutawaliwa na mawazo ya kujidhuru au kufanya majaribio ya kujiua, kujitenga, kupoteza hamu ya kula au kula kupita kiasi, kupunguza umakini pamoja na changamoto katika kupata usingizi.

Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu wa masuala ya chakula na lishe na Meneja mradi wa afya ya mama na mtoto kutoka Shirika la World Vision, Dk Daud Gambo anasema kuwa mama anayenyonyesha anapopitia changamoto zinazoweza kusababisha kupata msongo wa mawazo, huleta athari katika mchakato wa unyonyeshaji.

Dk Gambo anasema msongo wa mawazo huathiri uzalishaji wa vichocheo vinavyosababisha maziwa kuzalishwa na kutoka, ikiwemo homoni iitwayo ‘Ploractin’.

Anasema homoni hiyo inapotoka kwa kiwango kidogo, hufanya pia uzalishaji wa maziwa ya mama kuwa katika kiwango kidogo.

Pia anasema mama anapopata changamoto ya sonona au msongo wa mawazo huweza kukosa utulivu wa kumuweka kwa usahihi mtoto katika titi, kama inavyoshauriwa na wataalamu.

“Baadhi ya wanawake wanaonyonyesha wanapokosa utulivu wa afya ya akili, huweza kufikia hatua ya kuacha kunyonyesha watoto mapema, uzingativu hafifu wa mtoto na wengine hufikia hatua hata ya kudhuru watoto,” anasema.

Pamoja na msongo wa mawazo, mambo mengine yanayotajwa kuathiri unyonyeshaji ni pamoja na kutozingatiwa kwa mlo kamili na kutopata muda wa kutosha wa kupumzika.

Dk Gambo anasema ni muhimu mama anayenyonyesha kuonyeshwa upendo, kutiwa moyo na mwenza wake, marafiki pamoja na jamii kwa ujumla ili kumsaidia kupata utulivu wa akili, pia asaidiwe kazi ili aweze kupata muda wa kutosha kupumzika.

“Wenza kwa kipindi hicho wajitahidi kutenga muda kuzungumza na wake zao waliotoka kujifungua, kuwaonyesha upendo, kuwajali na kuonyesha shukrani kwa kuwaletea mtoto. Hii itasaidia kuleta amani ya moyo,” anaongeza.

Naye Daktari wa masuala ya uzazi, Cyril Masawe anaeleza kuwa ni muhimu saa kadhaa baada ya mama kujifungua mtoto aweze kunyonya ziwa la mama, kwani kadiri mama anapomuweka mtoto kunyonya ndivyo anavyozalisha maziwa mengi.

Anasema pia ni muhimu kwa mama kula mlo kamili, maji ya kutosha pamoja na vyakula vyenye majimaji ili kumrejeshea maji yanayopungua wakati wa kunyonyesha.

Mtaalamu wa lishe, Dk Elizabeth Proscovia, anasema katika kipindi cha unyonyeshaji mama hahitaji kula chakula kingi, bali huhitaji mlo kamili wenye virutubisho sahihi ili kurudishia virutubisho vilivyopotea wakati wa kujifungua.

“Ili kuondoa hali hii, ni muhimu mama kupata elimu ya kutosha kuhusu unyonyeshaji, namna bora ya kumuweka mtoto katika titi ili aweze kunyonya vizuri, kupangilia mlo wake, kujiepusha na mawazo, pia kusaidiwa kazi zake ili apate muda wa kutosha wa kupumzika,” anasema.

Related Posts