Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amewataka mawakala wa forodha nchini kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa huku akiwaahidi mazingira bora ya kazi.
Ameyasema hayo jana Agosti 1, 2024, alipokutana na wanachama wa Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFFA) kwa lengo la kusikiliza changamoto zao, kujadiliana namna ya kuzitatua na kuboresha huduma za forodha ili kuhakikisha wanalipa kodi stahiki.
Mwenda amesema wapo kwenye mchakato wa kuboresha mifumo yao ili kutimiza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan ili kuweza kuingiza mapato mengi na kuondoa changamoto ya rushwa.
“Pale changamoto zitakapojitokeza naomba ushirikiano ili tufanye kazi pamoja kuepusha ucheleweshaji wa mizigo ya watu kukaa muda mrefu. Pia Serikali haitaki udanganyifu,” amesema.
“Neno rushwa linazungumzwa sana inaonekana rushwa zinatolewa sana. Nashauri hilo suala lisifanyike, ni kosa zaidi, tutaboresha ili huduma zitolewe haraka hasa kwenye maeneo ambayo kuna shida hiyo.”
Mwenda amewataka TAFFA wafanye kazi kwa kushirikiana na TRA ili kupunguza changamoto ya ucheleweshwaji wa mizigo huku akiwasisitiza kutopokea rushwa kutoka kwa wateja ili kuwahisha bidhaa zao.
Aidha, Mwenda amewahakikishia wanachama hao kuwa ameyachukua maoni yao na changamoto kwa yale yaliyokuwemo ndani ya uwezo wao watakwenda kuyafanyia kazi na yale ya kisera watayapeleka sehemu husika.
Kwa upande wake, Rais wa TAFFA, Edward Urio, amesema ushirikiano wao na maofisa wa idara ya forodha umewasaidia kuvuka malengo waliowekewa katika ukusanyaji kodi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
“Tumevuka malengo ya ukusanyaji wa kodi kutokana na ushirikiano mzuri kati ya maofisa wa TRA na sisi mawakala wa forodha na kufanikiwa kukusanya kodi kwa niaba ya Serikali,” amesema Urio.
Amesema kwao ni faraja kubwa baada ya Mwenda kukubali kukutana nao na kujadiliana namna ya kuongeza ufanisi wa ukusanyaji kodi na kuboresha ushirikiano.
“Tunamuhakikishia kuwa malengo aliyopewa si yako pekee yake tutashirikiana naye kuhakikisha yanatimia,” amesema.