AKILI ZA KIJIWENI: Aussems awe makini na Singida BS

KOCHA wa mpira Patrick Aussems anapaswa kujipanga vilivyo Singida Black Stars anakoendelea na kibarua cha kuifundisha.

Najua ukweli unauma, lakini hakuna namna inabidi tumwambie ukweli maana tunapenda kuona akiendelea kufundisha soka hapa nchini.

Kwa namna alivyoanza, haonyeshi matumaini kama anaweza kuifanya Singida Black Stars kuwa na makali ambayo wengi wanategemea kuyaona yatakayoifanya iwe tishio kwa vigogo vya soka nchini.

Matokeo ya uwanjani bado hayaridhishi maana ilipoteza mechi mbili kati ya tatu za Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) na ikashinda moja hivyo kutolewa mashindanoni.

Kijumla haikuonyesha kiwango bora kwenye yale mashindano lakini tukamwelewa Aussems kwa vile timu ilikuwa na wachezaji wengi wapya.

Baada ya Kombe la Kagame ikarudi katika uwanja wa mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya msimu na mechi yake ya kwanza ya kirafiki dhidi ya Dodoma Jiji ikapoteza.

Ukiondoa matokeo, bado Singida Black Stars haionekani kuwa na utawala ndani ya uwanja licha ya kuwa na kundi kubwa la wachezaji wazuri ambao wamesajiliwa wakati wa dirisha la usajili linaloendelea.

Aussems akumbuke uwekezaji mkubwa wa fedha ambao Singida Black Stars imeufanya kwa kusajili wachezaji wenye wasifu mkubwa barani Afrika unahitaji matokeo mazuri na soka safi  na sio vinginevyo.

Asitegemee kama kutakuwa na msamaha kwake ikiwa ushindi utakuwa mgumu kupatikana na huku timu haionyeshi kabumbu la kuvutia.

Related Posts