DC LULANDALA AKAGUA MABANDA MAONYESHO NANE NANE ARUSHA

Na Mwandishi wetu, Arusha

MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Fakii Raphael Lulandala amekagua mabanda ya maonyesho ya 30 ya kilimo ya nane nane kanda ya Kaskazini yanayofanyika viwanja vya Themi Njiro jijini Arusha na kuridhika na maandalizi yaliyofanyika.

Kauli mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu wa 2024 ni chagua viongozi wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Lulandala ambaye amemwakilisha mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Cuthbert Sendiga kwenye maonyesho amekagua mabanda mbalimbali na kujionea namna taasisi, halmashauri, mashirika ya serikali na binafsi na wadau mbalimbali walivyojipanga kushiriki maonyesho hayo.

Akiwa kwenye maonyesho hayo ametembelea maeneo mbalimbali ikiwemo mabanda ya halmashauri za wilaya mbalimbali, vipando vya miche ya mazao mbalimbali, zana za kilimo na mabanda ya mifugo.

Akiwa kwenye banda la kampuni ya Agrimaco amejionea zana za kilimo ikiwemo matrekta yakiuzwa na kuelezewa namna ya mbolea bora zinavyostawisha mazao.

Bwana shamba wa kampuni hiyo Mohamed Hussein amemuelezea mkuu huyo wa wilaya namna wanavyotoa ushauri kwa wakulima kwenye matumizi ya mbolea.

Pia, mkuu huyo wa wilaya ametembelea banda la halmashauri ya mji wa Babati na kupatiwa elimu ya upimaji udongo kwenye maabara ili kubaini ubora wake.

Bwana shamba wa halmashauri ya mji huo Sebastian Joseph akielezea zao la muhogo uliokuwepo kwenye maonyesho hayo amesema wakulima watapata tija endapo watafuata maelekezo ya wataalamu.

“Zao la muhogo aina ya kiroba kutoka kata ya Mutuka kwenye shamba la ekari moja ukipanda miche 4,000 utazalisha Tani 40,” amesema Joseph.

Mkulima wa kijiji cha Naberera, Wilayani Simanjiro, Namnyaki Mollel amemweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa amefika na mazao yake ya mifugo kwa ajili ya kupata elimu zaidi.

DC Lulandala akizungumza baada ya kutembelea mabanda hayo amewapongeza washiriki wote kwa namna walivyojipanga katika kuonyesha bidhaa zao kwa walaji.

“Japokuwa leo Agosti mosi ndiyo mwanzo wa maonyesha inaonyesha kuwa ufunguzi rasmi utakapofanyika Agosti 3 mambo yatakuwa mazuri zaidi ila nawapongeza washiriki wote kwa namna walivyojipanga na bidhaa zao,” amesema DC Lulandala.

 

Related Posts