Dar es Salaam. Kamati ya Rufaa ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), imetoa majibu ya rufaa iliyokatwa na aliyekuwa mgombea uenyekiti wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo, ambaye ameshindwa katika rufaa hiyo.
Rufaa hiyo yenye kurasa sita ambayo Mwananchi imeiona leo Ijumaa Agosti 2, 2024 Doyo amekiri kuipokea jana Agosti Mosi, 2024 saa saba usiku kutoka kwa kamati hiyo kwa njia ya mtandao wa WhatsApp ikiwa imesainiwa na wajumbe John Noco, Lydia Beshe na Said Miraji.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Katibu wa kamati hiyo, John Mboggo amethibitisha kuwa wamemtumia uamuzi wa rufaa Doyo, akisema kilichobaki ni wahusika kuendelea na mazungumzo ndani ya chama.
Hata hivyo, Doyo amesema hajaridhishwa na uamuzi wa rufaa akisisitiza msimamo wa kwenda kufungua kesi wiki ijayo upo palepale.
Wakati Doyo akisema hayo, Mwenyekiti wa ADC, Shabaan Itutu amesema wamepokea kwa furaha majibu ya rufaa hiyo, huku akimkaribisha Doyo ambaye ni katibu mstaafu wa chama hicho kurudi na kuendelea kukijenga kupitia nafasi yake ya mjumbe wa kudumu wa Taifa wa ADC.
Itutu pia ametaka wanachama kuweka tofauti zao pembeni kwa kuwa suala hilo limeshaisha hivyo wawe pamoja katika kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Doyo aliyegombea uenyekiti wa ADC Juni 29, 2024, alikata rufaa akipinga matokeo ya uchaguzi uliompa ushindi Itutu aliyepata kura 121 dhidi ya kura zake 70.
Katika rufaa hiyo, Doyo alikuwa akilalamikia ongezeko la wapigakura, mkutano kutofuata sheria ya vyama vya siasa, wajumbe wa bodi ya uongozi Taifa hawakuchaguliwa bali waliteuliwa.
Pia, analalamikia msimamizi wa uchaguzi kuwazuia kufanya kampeni wakati wa uchaguzi na mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Hamad Rashid kuendelea na uenyekiti wa kikao cha uchaguzi hadi mwisho ikiwa ni kinyume cha katiba na kanuni za ADC.
Katika rufaa hiyo iliyoanza kusikilizwa Julai Mosi, kamati imesema ilipitia vielelezo 109 vya ushahidi kutoka vyanzo tofauti ikiwemo picha jongefu na ushahidi kwa wanachama mmoja mmoja.
Kwa mapitio ya ushahidi wa zaidi ya siku 28 tangu kufanyika kwa uchaguzi, kamati hiyo imesema haikuona hata siku moja wala kupokea si kwa mlalamikaji wala mlalamikiwa, vielelezo vinavyoonyesha ongezeko la wapigakura.
Badala yake iligundua kuwa kamati ya uchaguzi ilizuiwa kupiga kura ili kutoleta mkanganyiko wa kimasilahi, hivyo wajumbe wake wanane kutopiga kura ili kuweka uwiano sawa na kura zilizopigwa kuwa 192 na si zaidi.
“Pamoja na hali hii bado kamati iliangalia iwapo kukosekana kwa kura nane kungeliweza kuathiri vipi matokeo ya kura 121 ambazo alipata mshindi na zile 70 alizopata mlalamikaji na kura moja kuharibika.
“Hii ni baada ya kujiridhisha kwamba tofauti ya kura kwa mshindi na mshindwa ni kubwa mno, kamati imeona dai hili nalo halina mashiko,” inasomeka sehemu ya uamuzi wa rufaa hiyo.
Kuhusu malalamiko ya uwepo wa mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Rashid Hamad, kamati iligundua kwamba uwepo wake ulikuwa na baraka za wajumbe wa mkutano mkuu akiwemo mgombea maana hakuna aliyehoji juu ya uwepo wake na kuwa kwa kuwa mkutano mkuu ndiyo chombo chenye mamlaka ya juu, hivyo haikuwa tatizo.
“Hakuna kanuni iliyokiukwa katika jambo hili maana ipo wazi kuhusu nani anayepaswa kujiuzulu na kuondoka katika madaraka yake kwenye mkutano mkuu zaidi na kwamba, kamati imejiridhisha hakukuwepo na athari ya moja kwa moja au kwa taathira yake kwa mwenyekiti aliyemaliza muda wake kuendelea na nafasi hiyo kwa ridhaa ya mkutano mkuu maana alikuwa ni mjumbe halali wa mkutano mkuu huo,” inaelezwa katika uamzi huo.
Kuhusu hoja ya utaratibu wa kuwapata wajumbe wa bodi, kamati imeeleza kwa kuzingatia kanuni, mgombea ndiye mwenye haki ya kukata rufaa na kwamba mlalamikaji hakugombea nafasi hiyo.
Pia hakuna mgombea yeyote wa ujumbe wa bodi aliyeonyesha kutokuridhishwa na uchaguzi wao au aliye kata rufaa mbele ya kamati au kuwasilisha malalamiko yoyote mbele ya kamati ya rufaa.
“Hii inaonyesha kwamba wameridhishwa na matokeo waliyopata sambamba na uchaguzi wa nafasi zote nyingine katika uchaguzi huo, hivyo hoja hiyo nayo haina mashiko,” imesema rufaa hiyo.
Katika hoja ya mlalamikaji kutaka kurudiwa kwa uchaguzi, kamati imetupilia mbali na kuyafuta kabisa madai hayo ikieleza uchaguzi huo ulikuwa huru na mdai alikubali matokeo kwa kupitia wakala wake, Ibrahimu Pogora kuweka saini ya kukubali idadi ya kura, hivyo kuonyesha kuwa zoezi lilikuwa sahihi na lisilo na dosari.
Kutokana na hilo, kamati imemshauri mleta rufaa kurudi katika uongozi anaoukubali kwa ajili ya mashauriano ya namna atakavyopata nafasi anazohitaji ndani ya chama hicho.
Kamati hiyo imesema inaheshimu nia za kutimiza haki za kikatiba ila inapenda kutoa angalizo kuwa haki yoyote isiyofuata taratibu sahihi ni sawa na kupinga uhalali wa uhusika wake tangu mwanzo.
“Kamati ina nia ya dhati ya kuona jambo hili likitatuliwa bila mvutano ndani ya chama, hivyo inajitoa na kurudisha mamlaka yake kwa uongozi wa chama uliochaguliwa kwa kikao halali na kupigiwa kura halali kisheria, ili uongozi ufanye hatua stahiki za kutimiza azma za wanachama.
Kwa apande wake, Doyo amesema hakubaliani na majibu ya rufaa hiyo na mpango wake wa kwenda mahakamani wiki ijayo upo palepale.
Amesema atapeleka barua kwa msajili wa vyama vya siasa kulalamikia rufaa kutotolewa majibu ndani ya saa 48 baada ya kumalizika uchaguzi kama sheria inavyotaka badala yake imechukua mwezi mzima.
Kwa mujibu wa Doyo, atafungua kesi mbili mahakamani, moja ikihusu haki ya kutosikilizwa katika rufaa hiyo ambayo amesema walisikilizwa upande mmoja.
Hata hivyo, katibu wa kamati ya rufaa anapinga akisema kilichokuwa kinafanyika ni maridhinao na iliamuliwa madai yake ya msingi katika hilo kuondolewa katika kikao walichokaa Julai 8 na Doyo aliridhia.
Amesema kesi nyingine ya msingi ni kutaka kutenguliwa uchaguzi huo kwa kuwa haukuendeshwa kwa kufuata katiba ya chama hicho.
Hata hivyo, amesema katika majibu ya rufaa hiyo, kamati imeweza kumuongezea vielelezo vya kuwasilisha mahakamani ikiwemo ya kubaini uwepo wa uvunjifu wa wapigakura.