DRC yawakumbuka mamilioni ya watu waliokufa kwa vita – DW – 02.08.2024

Mjini Goma, sherehe zilianza kwanza katika makaburi ya Genocost, yaliyotengwa kwa ajili ya waathiriwa wa vita, kisha ikafuatiwa na hafla kwenye uwanja wa Benki ya Maendeleo ya Nchi za Maziwa Makuu. Zaidi ya Goma, nchi nzima ilishiriki kwa dhati katika kumbukumbu hii ya Genocost.

Siku ilianza mjini Goma kwa mazishi ya watu saba, waliokuwa waathiriwa wa shambulio la mabomu la waasi wa M23 takriban wiki tatu zilizopita katika mji mdogo wa Bweremana. Mazishi haya yalifanyika katika makaburi yaliyotengwa kwa ajili ya waathiriwa wa vita, makaburi ya Genocost.

Serikali ya DRC inasema vita vinavyoendelea nchini humu ni vya unyakuzi wa mali

Mjumbe wa serikali kuu mjini Goma kwa tukio hili, Waziri wa Madini, Kizito Pakabomba, alikumbusha kwamba vita vinavyoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni vita vya kiuchumi, vinavyolenga kunyakua utajiri wa asili uliopo katika sehemu hii ya nchi. Zaidi alisema “Damu ya Wakongo imemwagika vya kutosha. Damu ya Wakongo inaendelea kumwagika. Tumekusanyika leo katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini kuadhimisha mauaji ya kimbari ya Kongo kwa ajili ya faida za kiuchumi. Ni wakati wa haki kurejeshwa. Waathiriwa wetu hawapaswi kusahaulika.”

Jeshi la Kongo katika doria huko Goma
Picha iliyopigwa Aprili 11, 2024 inaonyesha wanajeshi wa Jeshi la Kongo wakiwa doria huko Goma, jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Wang Guansen/Xinhua/picture alliance

Kwa miongo kadhaa, nchi jirani zinatuhumiwa kuwa chanzo cha migogoro mikubwa kwenye ardhi ya Kongo, ambapo raia, hususani wanawake na watoto, wamekuwa wahanga wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na haki za kimataifa za kibinadamu, kupitia mauaji ya halaiki, ubakaji, mauaji ya kikatili na ya kulenga.

Tafakari ya ukimya wa kimataifa kuhusu hali ya mzozo wa Kongo

Yote haya yanafanyika kukiwa na ukimya mkubwa wa jumuiya ya kimataifa, kama ilivyokuwa ikilalamikiwa na mamlaka zaKongo.

Gavana wa kijeshi wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini, Peter Chirimwami, katika siku hii, alikemea ukimya huo wa jumuiya ya kimataifa dhidi ya kile alichodai ni “vitendo vya kikatili vya Rwanda,” aliongeza kusema “Mahali pengine kama kuna shida, wanalaumu haraka, lakini maafa ya Wakongo, wanaiona kama sio kitu, ijapokuwa nasi ni binadamu kama wengine, na tuna sheria kama wengine.” Alisema kiongozi huyo.

Soma zaidi: Takriban nyumba 2,750 zimechomwa moto DRC

Bendera ya taifa la Kongo ilikuwa nusu mlingoti siku nzima ya leo. Katika kila mkoa na katika diaspora, Wakongo waliwakumbuka mamilioni ya Wakongo waliouawa kikatili. Mwisho wa kumbukumbu ya leo ilikuwa ni kwa maputo meupe kurushwa angani kama kumbukumbu kwa waathiriwa na kutaka amani.

DW Goma

Related Posts