Timu ya Soka ya Diamond Trust Bank (DTB) imetawazwa kuwa bingwa mpya wa mashindano ya mabenki msimu huu yaliyofikia tamati usiku wa jana Agosti Mosi kwenye viwanja vya klabu ya Gymkhana, Dar es Salaam.
DTB imeifunga timu ya CRDB benki bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliokuwa na upinzani mkali kwa pande zote.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu hizo zilitoshana nguvu kwa suluhu, kabla ya Jumaa Ramadhan kuiandika bao la kuongoza DTB dakika ya kwanza ya kipindi cha pili baada ya kupigwa kaunta na kuwashinda ujanja mabeki wa CRDB kisha kuachia shuti lililojaa wavuni, bao lililodumu hadi mwisho wa mchezo.
Bao hilo liliongeza hamasa ya mashabiki wa DTB walioongozwa na ofisa mtendaji mkuu, Ravneet Chowdhury ambao walitawala uwanja kwa kuishangilia kwa nguvu timu yao ambayo ilicheza kwa kushambulia na kujilinda kwa pamoja vipindi vyote viwili.
Akizungumzia mashindano hayo, Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi amesema hamasa ilikuwa kubwa msimu huu.
“Yamefanyika kwa mwezi mmoja kuanzia hatua ya awali hadi leo (jana) inafanyika fainali, mechi ya fainali ilikuwa na upinzani mkali mno na tumepata bingwa mpya,” amesema Sabi
ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa CRDB.
Amesema lengo la mashindano hayo ilikuwa ni kuwaunganisha pamoja, kufahamiana kupitia michezo na kujenga afya kwa wafanyakazi wa benki nchini.
“Kama nilivyosema awali, huu ni msimu wa pili, tulipoanza yalishirikisha ‘bankers’ wenye umri wa miaka 35 na zaidi , msimu huu yameshirikisha wote bila kigezo cha umri na hamasa imekuwa kubwa,” amesema.
Kwa mujibu wa Sabi, mashindano hayo yatakuwa endelevu na wataendelea kuyaboresha kila mwaka ili yawe makubwa zaidi.
Akizungumzia mchakato wa mashindano hayo,
Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Tuse Joune amesema msimu huu timu 26 zimeshiriki.
“Lengo limetimia, msimu huu ni wa pili hamasa imeongezeka na tunategemea iwe kubwa zaidi,” amesema.
Joune amesema mashindano hayo sasa yatakuwa yakianza Julai Mosi ya kila mwaka kuanzia msimu ujao.
Msimu huu timu ya benki ya Absa ilikamata nafasi ya tatu huku timu ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ikicheza na wenyeji Gymkhana katika kunogesha fainali iliyozikutanisha DTB na CRDB.
Michezo mingine iliyofanyika msimu huu ni rede na kuingiza mpira kwenye pipa sanjari na mechi ya mabenkers senior wapenzi wa Simba na Yanga, na timu zilizofanya vizuri zilikabidhiwa medali na vikombe pamoja na timu yenye nidhamu na mfungaji bora wa mashindano hayo.