Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imesema kanuni ya mwaka 2023 ya ulinzi wa mizigo na usalama wa utendaji kazi katika bandari zimekuwa msaada mkubwa katika kuboresha utendaji na kukuza pato la taifa.
Kwa mujibu wa kamati hiyo, kanuni hizo zilitungwa kulinda usalama wa watu na mizigo, kulinda mali, kuzuia uharibifu wa mazingira na kuimarisha bandari kuwa shindani.
Tayari kanuni hizo zimekwishatangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na 381 la Julai 2,203 na marekebisho yake ya Mei 24, 2024 la tangazo la Serikali Na 406 ikiwalenga waendeshaji wa bandari ya kwenye bahari, maziwa na bandari kavu.
Hayo yameelezwa leo Agosti 2, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Jason Rweikiza ambaye aliambatana na wajumbe wa kamati hiyo kutembelea shughuli zote zinazodhibitiwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) katika Bandari ya Dar es Salaam na bandari kavu.
“Tumekuja kuangalia utendaji wa Sheria ndogo na kipekee niseme baada ya kufika gati sufuri katika bandari ya Dar es Salaam tumeshuhudia mambo ya tofauti hasa ufanisi kuongezeka, uongozi wa DP World umetueleza kabla ya kuanza kazi meli hapa bandarini ilikuwa inasubiri siku 30 lakini baada ya kuanza kazi miezi minne sasa meli zinasubiri kwa siku saba na wanaendelea kuboresha zaidi meli isubiri kwa muda mfupi zaidi,” amesema.
Dk Rweikiza ambaye ni Mbunge wa Bukoba Vijijini amesema kwa sasa meli ya mizigo haikai foleni kwenye bandari hiyo badala yake inapofika huenda moja kwa moja kupakuliwa mizigo.
Amesema kwa sasa wanazipitia sheria ndogo vifungu kwa vifungu na watakapoona uhitaji wa maboresho watayafanya kwa lengo la kuinua ufanisi zaidi ya bandari.
Kuhusu matukio ya wizi amesema hakuna matukio ya wizi ambayo yamewahi kuripotiwa hivi karibuni kutokana na kuimarishwa kwa usalama uliochangiwa na uwepo wa kanuni.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema kanuni ambazo wabunge hao wamekuwa wakizipitisha zimekuwa msaada mkubwa katika kuinua ufanisi wa bandari.
“Kwa kipindi cha miezi minne yangu DP World waanze kufanya kazi ufanisi umeongezeka, ukiangalia utendaji wetu kwenye bandari miaka ya mitano iliyopita tulikuwa tunahudumia tani milioni 17 ya mizigo na sasa tumefikia tani milioni 37 kwa mwaka, hizi ni juhudi kubwa zinazotokana na uwekezaji unaofanyika kwenye bandari,” amesema.
Akizungumzia utekelezaji wa kanuni ya ulinzi na usalama wa utendaji kazi katika bandari ya mwaka 2023, Kaimu Mkurugenzi wa TASAC, Nelson Mlali shirika hilo linasimamia utekelezaji kwa kuandaa na kuhuisha ‘checklist inayobainisha maeneo ya ukaguzi kuhusu usalama:
“Pia tunaendesha kampeni za mara kwa mara kwa kuwapatia elimu watoa huduma zinazodhibitiwa, kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali kama vile Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha) kudumisha usalama wa mizigo na mazingira ya kazi zinazohusiana na shughuli za usafiri kwa njia ya maji,” amesema.
Mlali amesema pia wanakagua maeneo ya kazi za bandari na bandari kavu ili kujiridhisha na hali ya uzingatiaji wa usalama na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo mbalimbali yanayotolewa kwa nyakati mbalimbali ikiwemo wakati wa utoaji elimu.
Mkuu wa Idara ya Fedha Kampuni ya DP World, Mathew Clifft amesema wataendelea kuongeza ubunifu na kuimarisha utendaji kwenye bandari hiyo kuifanya kuwa na ushindani mkubwa.