Mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis ameungana na nyota wa kikiosi cha Simba SC tayari kwa maandalizi ya msimu mpya huku uongozi wa timu hiyo ukiweka wazi kuwa adhabu yake ipo pale pale kwa sababu alikiuka utaratibu.
Staa huyo hakuwa pamoja na timu Misri ilipoweka kambi ya kujiandaa na msimu wa 2024/25 alitimka nchini kwenda Norway kwaajili ya kujiunga na Kristiansund BK.
Kutokana na Kibu kuwa na mkataba mpya na Simba haikuwa rahisi kukamilisha dili hilo kwani inaelezwa Simba walihitaji Dola 1 milion (Sh 2.7 bilion) ili kumuuza moja kwa moja na timu hiyo imeshindwa kufanya hivyo na ndio sababu ya mshambuliaji huyo kurejea nchini.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kililiambia Mwanaspoti kuwa Kibu alijiunga kambini na wenzake ambao walipewa mapumziko ya siku moja baada ya kuwasili kutoka Misri.
“Kibu yupo kambini na ataungana na wachezaji kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuvaana na APR kwenye mchezo wa Simba Day tamasha maalum la kutambulisha kikosi cha msimu mpya.”
Mwanaspoti lilimtafuta Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amesema ni kweli mchezaji huyo ameungana na timu na leo ‘ atakuwa sehemu ya kikosi kitakachofanya mazoezi.
“Ndio ni kweli yupo kambini bado ni mchezaji wa Simba na ndio maana amejiunga na kikosi mambo mengine uongozi ndio unafahamu nini cha kufanya.” Alisema.
Taarifa ya awali iliyotolewa na Simba ilieleza kuwa uongozi wa timu hiyo utamchukulia hatua mchezaji huyo kutokana na utovu wa nidhamu na umma utapewa taarifa.