MAAGIZO MATANO YA DKT. BITEKO NANENANE MBEYA

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa maagizo matano kwa Wizara ya Kilimo, Taasisi na Mikoa yanayolenga kukuza na kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.

Dkt. Biteko ametoa maagizo hayo leo Agosti 2, 2024 jijini Mbeya wakati akifungua Sherehe za Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ya Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale.

“ Wekeni mipango ya matumizi bora ya ardhi na izingatiwe kuwa makundi makubwa ya mifugo yameingizwa katika mikoa ya nyanda za juu kusini. Madhara yake ni makubwa ikiwemo kuharibiwa sana kwa mazingira. Hivyo, Wizara zote husika na Wakuu wa Mikoa chukueni hatua thabiti,” amesema na kuongeza “Kumekuwepo na matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu na kemikali nyingine. Jambo hili lina athari kubwa kwa afya ya binadamu na viumbe hai vingine. Nawasihi wakulima, wafugaji na wavuvi kuzingatia maelekezo ya wataalam ili tuweze kuzalisha pasipo kuathiri afya ya binadamu na mazingira yetu.”

Pia ameagiza kupimwa kwa maeneo ya taasisi za utafiti wa kilimo kupewa hati na kulindwa yapewe hati miliki na yalindwe pamoja na utaratibu mzuri wa kutenga maeneo kwa madhumuni ya uzalishaji wa mbegu na pia utunzaji wa yale yaliyopo. “Naelekeza Mamlaka zinazohusika pia kutenga na kupima ardhi kwa ajili ya madhumuni hayo ya kuzalisha mbegu na kuyalinda dhidi ya uvamizi,” amesema Dkt. Biteko.

Kuhusu usalama wa chakula katika ngazi ya kaya amesisitiza wananchi kuhifadhi chakula kwa ajili ya matumizi ya kaya. Aidha, kwa mazao ya biashara amewasihi wakulima kutoyauza kabla ya kukomaa na kufikia ubora unaokubalika ili kulinda soko la mazao ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia uhaba wa mbegu za malisho na mbegu bora za mifugo vikiwemo vifaranga vya Samaki. Dkt. Biteko ameielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi na taasisi za utafiti wa mifugo na viumbe maji kuhakikisha mbegu za malisho na mifugo zinapatikana kwa wananchi na kwa gharama nafuu.

Pia, Dkt. Biteko amesema uzalishaji wa mazao ya chakula kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini umeendelea kuongezeka ambapo kwa msimu wa mwaka 2022/2023 Kanda hiyo ilizalisha tani 11,814,480.63 za mazao ya chakula huku mwaka 2023/2024 ikizalisha tani 13,559,101.43 sawa na ongezeko la asilimia 15.

“ Mahitaji ya chakula katika Kanda hii inakadiriwa kuwa tani 3,044,561.8 hivyo Kanda itakuwa na ziada ya tani 10,514,539.63. Hii inafanya mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini kuchangia hali ya usalama wa chakula katika nchi yetu. Aidha, ongezeko hilo la uzalishaji limetokana na juhudi na jitihada za Serikali za kuhakikisha kuwa tija inaongezeka katika sekta ya kilimo kwa kuandaa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea na kuutekeleza kwa kutoa ruzuku ya mbolea kwa Wakulima wote.” Amebainisha Dkt. Biteko.

“ Serikali imedhamiria kuendeleza Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuongeza uzalishaji, tija na thamani ya mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na kukuza kipato na kutoa ajira kwa wananchi hasa ikizingatiwa kuwa kilimo ndiyo kimeajiri wananchi zaidi ya asilimia 85 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na makazi ya 2022. Kwa sababu hiyo, Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Shilingi 275 bilioni mwaka 2021/2022 hadi Shilingi 295 bilioni mwaka 2023/24 na ile ya Wizara ya Kilimo kutoka Shilingi 294,162,071,000 kwa mwaka 2021/2022 hadi Shilingi 1.3 trilioni mwaka 2024/2025.” Amesisitiza Dkt. Biteko.

Vilevile Dkt. Biteko ameitaka Wizara ya Kilimo na Mamlaka ya Hifadhi ya Chakula (NFRA) kusimamia utekelezaji wa agizo la Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha bei ya mahindi kwa kilo moja inauzwa shilingi 700 kama ambavyo wananchi waliomba.

Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji na kuhimiza matumizi ya mbolea kupitia Mpango wa ruzuku ili kuendelea kuongeza tija na uzalishaji. Ambapo kupitia Mpango huo matumizi ya mbolea kwa mwaka 2023/2024 yamefikia tani 412,859.76 ikilinganishwa na tani 313,593 kwa mwaka 2022/2023. Aidha, katika mwaka 2024/2025 Serikali itaendelea kuwezesha upatikanaji wa mbolea nchini kupitia Mpango wake wa ruzuku.

Sambamba na hayo Dkt. Biteko ameishukuru Benki ya Azania na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kutoa mikopo kwa wakulima na kuwaomba waongeze kasi ya kutoa mikopo nafuu kwa wakulima nchini.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa kaulimbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka 2024 inasema “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya killimo, Mifugo na Uvuvi”. inalenga kuwakumbusha wananchi katika uchaguzi wa mwaka 2024 kuchagua viongozi bora wa Serikali za Mitaa, hasa kwa kuzingatia kuwa shughuli za uzalishaji katika sekta za kilimo zinafanyika katika ngazi ya Serikali za Mitaa.

Naye, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Akson amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali mkoni humo ikiwemo ujenzi wa shule, vituo vya afya na barabara.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde amesema kuwa Wizara ya Kilimo imeanza utekelezaji wa agizo la Rais Mhe. Dkt. Samia la kutaka Uwanja wa Nzuguni ulipo Dodoma na Uwanja wa John Mwakangale vinajengwa ili kuwa na hadhi ya viwanja vya kimataifa vya maonesho ya Nanenane.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo amesema kuwa mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini imeendelea kuzalisha chakula cha kutosha na kuwa wameendelea kuhimiza wananchi kujitahidi kuzalisha chakula kwa wingi zaidi.

Related Posts