Kaliua. Wananchi wamepatwa na taharuki baada ya uwepo wa makaburi mawili kubwa na dogo ambayo hayakuwa na watu bali yakiwa yamezikwa vitambaa vyeupe.
Tukio hilo limetokea Julai 27, 2024 katika Kitongoji cha Usinga, Kata ya Ukumbisiganha, Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora ambapo wananchi walishangazwa uwepo wa makaburi hayo bila uwepo wa matangazo ya msiba.
Kutokana na tamaduni zilizozoeleka za wananchi kupewa taarifa za uwepo wa msiba imekuwa tofauti kwa makaburi hayo ambayo wenyeji wa eneo hilo hawakushirikishwa kwenye msiba na kutahamaki kuyaona.
Leo Ijumaa, Agosti 2, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema bada ya kupata taarifa walifanyia kazi kwa haraka na kugundua vilivyozikwa ni vitambaa bila uwepo wa miili ya watu ya makaburi hayo.
“Kweli Julai 27 tulipata taarifa za uwepo wa makaburi mawili Kitongoji cha Usinga kata ya Ukumbisiganga huko Kaliua kwamba kuna makaburi mapya yameonekana na kuleta taharuki kwa wananchi wetu kwakua hakukua na taarifa za msiba katika maeneo hayo,” amesema Abwao.
Amesema walifungua jalada la uchunguzi na kuomba kibali cha mahakama ili kuyafukua makaburi hayo kwa kushirikiana na viongozi pamoja na wananchi, walifukua makaburi na kukuta kila kaburi likiwa na kitambaa cheupe chenye urefu wa mita moja na nusu.
Hata hivyo, amesema baada ya kufukuliwa kwa makaburi hayo na kukutwa vitambaa wananchi waliondokana na taharuki na kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Amesema upelelezi wa kuwatafuta wahusika waliofanya jambo hilo unaendelea ili kueleza sababu ya kuvizika vitambaa hivyo katika eneo hilo.
Naye Mkazi wa Usinga, Ndulla Mihayo amesema wakiwa kwenye shughuli zao walishangaa kuona makaburi mawili kubwa na dogo yakiwa katika eneo moja ndani ya kitongoji chao na hakukuwa na tangazo la uwepo wa msiba.
“Tulishangaa uwepo wa makaburi mawili mapya kubwa na dogo yakiwa kwenye kitongoji chetu na ni mapya kabisa, maana hatukuwa na taarifa ya uwepo wa msiba kwenye eneo hili kwahivyo ikaleta taharuki kwa kiasi kikubwa,” amesema Mihayo.
Amesema kutokana na taharuki hiyo walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuchunguza kilichopo katika makaburi hayo kwani walikosa amani kwa saa kadhaa kwa kutofahamu waliozikwa kwenye makaburi hayo ni kina nani.