Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob Mkunda leo Ijumaa Agosti 2, 2024 ameongoza hafla ya kuwaaga majenerali sita wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliostaafu kulitumikia jeshi hilo.
Hafla hiyo imefanyika Kambi ya Jeshi ya Twalipo iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam.
Walioagwa ni pamoja na Meja Jenerali Gabriel Mhidze, Meja Jenerali Ally Katimbe, Meja Jenerali Chelestino Msolla na Meja Jenerali Charles Mbuge, aliyewahi kuwa mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (Taifa)
Pia wamo Brigedia Jenerali William Likangaga na Brigedia Jenerali Andrew Mughamba.
Jenerali Mkunda amesema tukio hilo ni utaratibu na utamaduni wa jeshi kuwaaga maofisa waliofikia ngazi ya jenerali kwa staili hiyo, ikiwa ni kutambua mchango wao mkubwa katika kulitumikia jeshi.
“Tumewakabidhi vitambulisho vyao vya kustaafu lakini watakuwa ni sehemu ya jeshi letu kwa miaka mitatu na ni kwa mujibu wa sheria.
“Tukiwahitaji tuna uwezo wa kuwatumia tena kwa miaka hiyo, kisha itakuwa ni hiari yao kulitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania,” amebainisha.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Meja Jenerali Gabriel Mhidze amewataka wanajeshi waliobakia wafanye kazi kwa welevu na ushupavu wa hali ya juu kwa maendeleo ya jeshi na Taifa kwa ujumla.
Majenerali hao ambao wengi wamelitumikia jeshi kwa zaidi ya miaka 30, wamesindikizwa kwa kusukumwa wakiwa kwenye magari ya kijeshi, kama ishara ya kuwaenzi kwa utumishi wao uliotukuka.
Kwenye hafla hiyo lilipigwa gwaride rasmi la heshima mbele yao.
Mbali na Jenerali Mkunda, wengine waliohudhuria ni wakuu wa kamandi, shule, makamanda wa vikosi, matawi na maofisa wengine wa jeshi hilo, waliopo na wastaafu.
Baada ya gwaride kumalizika kwa kuunda umbo la omega kuashiria mwisho wa utumishi wa maofisa hao ndipo walisukumwa wakiwa kwenye magari hadi lango kuu, kisha kuondoka.