Marekani yatoa onyo vitisho kuishambulia Israel

Dar es Salaam. Baada ya Iran na washirika wake kutangaza kuishambulia Israel, hatimaye Marekani imeibuka na kuikingia kifua Israel.

Rais wa Marekani, Joe Biden akizungumza kutoka Ikulu ya White House, amethibitisha kujitolea kwa usalama wa Israeli dhidi ya vitisho vyote kutoka kwa Iran, ikiwa ni pamoja na makundi ya Hamas, Hezbollah, na Huthis.

Rais Biden jana alikuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wakijadili juhudi za kuunga mkono ulinzi wa Israeli dhidi ya vitisho, ikiwa ni pamoja na dhidi ya makombora ya balestiki na drones.

Pamoja na ahadi hiyo ya ulinzi wa Israel, Rais Biden alisisitiza umuhimu wa juhudi zinazoendelea za kupunguza mvutano mkubwa katika eneo hilo. Makamu wa Rais Kamala Harris pia alijiunga na wito huo.

Awali, Iran ilitangaza kuishambulia Israel moja kwa moja ikiwa ni kulipiza kisasi baada ya mauaji ya kiongozi mkuu wa kisiasa wa Kundi la Hamas la Palestina, Ismail Haniyeh, mjini Tehran.

Haniyeh na mmoja wa walinzi wake waliuawa alfajiri ya juzi, Jumatano, Julai 31, 2024, baada ya jengo walilokuwa wakiishi kuvamiwa na kushambuliwa. Kutokana na mauaji hayo, Israel inanyooshewa kidole kuhusika ingawa haijatoa taarifa kuhusu tukio hilo.

Tovuti ya Times of Israel ilisema Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, aliamuru shambulio dhidi ya Israel. Khamenei na maofisa wengine wa Iran waliapa kujibu mapigo licha ya kwamba haijaelezwa ni lini watatekeleza mashambulizi hayo.

Hata hivyo, ikiwa Iran itatekeleza shambulio hilo, itakuwa si mara ya kwanza, kwani Aprili 14, 2024, Iran iliishambulia Israel kwa makombora takribani 300 baada ya Israel kudaiwa kushambulia ubalozi wake uliopo Damascus na kuua makamanda wa Iran.

Taarifa zaidi zilisema, maofisa hao wamesema Khamenei amewaambia makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Jeshi la Iran kuandaa mipango ya mashambulizi.

Vilevile, kutokana na tuhuma hizo, Israel haijazungumzia tukio hilo, huku kwa upande mwingine vita vyake na kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza vilivyoanza Oktoba 7, 2023, vinaendelea.

Israel imekuwa ikipambana na Hamas katika Ukanda wa Gaza tangu shambulio la kundi hilo lililosababisha vifo vya watu 1,197, wengi wao wakiwa raia, kulingana na hesabu ya AFP na takwimu rasmi za Israeli.

Imeandaliwa naVictoria Michael

Related Posts