MIAMBA ya soka nchini, Yanga na Simba zina historia ndefu kwenye mchezo huu na zaidi ya yote ni tambo zao uwanjani. Hata hivyo, mbali na uwanjani, hata nje ya uwanja zimekuwa zikitambiana kwa mambo mengi na zinashindana hadi kwenye maendeleo yao ya kisoka.
Dunia inazidi kubadilika. Maendeleo yanazidi kukua na timu hzi haziko nyuma kwenye maendeleo hayo. Zipo sambamba na utandawazi na matumizi ya inteneti kwenye maendeleo yao.
Hata hivyo, pamoja na ushindani mbalimbali, ila huu wa miaka ya karibuni kwa upande wa mavazi, nao unazidi kushika kasi na zimekuwa zikiangaliana kila msimu mwenzake ametoa uzi gani (jezi gani) toifauti na miongo kadhaa nyuma hazikuwa zikifanya hivyo.
Takribani misimu mitano sasa, klabu hizi pamoja na nyingine zimeanza kulichukulia suala hili kwa umakini mkubwa na zinazidi kushindana kwenye mavazi (jezi).
Kuishi kwingi, kuona mengi. Ndiyo. Wahenga hawakukosea. Nakumbuka enzi nikicheza soka shule ya msingi, timu zilitofautishwa kwa upande mmoja kucheza vifua wazi na mwingine ukivaa sare za shule au fulana.
Hali ilikuwa nafuu kidogo tulipocheza ligi daraja la pili na jezi tulipewa na wafadhili. Nakumbuka jezi zisizozidi aina tatu kwa timu mbili za Scud na Afya SC nilizochezea kwenye Ligi ya Mkoa.
Tulikuwa na jezi ya manjano yenye nembo ya kampuni ya mafuta ya BP, jezi ya bluu mawingu na jezi ya damu ya
mzee. Jezi hizi tulipewa na wafadhili wa ndani; nadhani ile ya damu ya mzee tulipewa na ndugu zetu ambao walihamia Arabuni, hivyo wakawa wakizikumbuka timu za nyumbani.
Uwepo wa jamii ya waswahili wenye asili ya arabuni ilikuwa ni faida kwetu kwani tulionekana tuna nafuu kwenye kupata jezi. Yote kwa yote, bado timu zangu mbili ziliazimana jezi (na pia wachezaji) pale mmoja alipopata nafasi ya kuwakilisha wilaya kwenye ligi ya mkoa.
Hadithi ya timu zangu za Karagwe pia ni hadithi ya maeneo yote ya nchi hata kwa klabu kubwa kama Yanga na Simba ambazo zipo kwa takribani miaka 90 na hata timu ya Taifa ilishawahi kukumbwa na kadhia hii ya kutokuwa na uhakika wa kupata jezi.
Kuna picha maarufu ya wachezaji wa timu ya Taifa Stars wakikaguliwa na Rais Jafary Nimeiry wa Sudan na mwenyeji wake Rais Julius Nyerere huku wakiwa vidari wazi.
Kuna maelezo mengi tofauti ya kwa nini timu yetu haikuvaa jezi, lakini itoshe kusema jezi zilikuwa ni kauka nikuvae au ikitokea jezi kuchelewa kufika kwenye vyumba vya kuvalia au jezi kugongana (kufanana) ilibidi timu moja icheze vifua wazi.
Wanasema ombaomba hapaswi kuwa mchaguzi. Nina picha ya wachezaji wa Simba wakiwa wamevaa jezi ya timu ya taifa ya Ujerumani (Magharibi?) iliyotwaa ubingwa wa dunia wa mwaka 1990.
Pia nina picha ya Yanga ikiwa imevalia jezi ya Taifa stars. Ilikuwa kawaida na hakuna aliyejali. Wafadhili kama Highway Carriers ya Azim Dewji na Bobby Soap ya Mohamed Viran walinunua jezi na kuzipiga chapa na kuwapa Simba na Yanga ambao kwao hicho kilikuwa ni kivuno.
Ni hadi miaka ya 2000 ndipo timu zilipoanza kuingia mikataba ya kuvalishwa jezi na wadhamini. Hata hivyo, starehe hiyo walikuwa nayo Yanga na simba na baadae Azam ambao walipanda daraja wakiwa na uhakika wa fedha za kuwavalisha.
Pale timu zilipoanza kuwa na uhakika wa kuvaa jezi za kwao na wadhamini kifuani ndipo mashabiki walipoanza kuwa na uhakika na jezi inayovaliwa na timu zao kwani ule utamaduni wa kila siku kuja na jezi ambayo haikuzoeleka ukawa unakufa taratibu. Mashabiki nao wakaanza kuvaa jezi ili kujinasibisha na klabu zao pendwa.
Kufunguka kwa China kama taifa linaloongoza kwa utengenezaji wa jezi ambazo hata mtu wa kawaida anaweza kumudu, kukachochea wafanyabiashara (maarufu wakinga) kuleta jezi nyingi zilizofanana na jezi za Yanga na Simba na kujitengenezea faida kibao.
Kwa miaka mingi kulikuwa na mvutano kati ya klabu na wafanyabiashara ya jezi kiasi cha kuhusisha vyombo vya dola. Tatizo kubwa ni kuwa uhitaji (demand) ilikuwa ni kubwa lakini klabu hazikuwa na uwezo au maarifa ya kuhakikisha wanakata kiu ya wapenzi wao. Wakinga walitumia hiyo fursa kujipatia riziki na kukuza biashara zao.
Ni hadi hivi karibuni, klabu zilipoanza kuingia makubaliano na wawekezaji ambao kwa kiasi kikubwa wameleta mapinduzi katika biashara ya jezi za timu.
Hivi karibuni, nilikutana na picha mtandao ya mswahili mmoja akiwa kwenye mitaa ya jiji moja huko Marekani ambako alitembeza sare za Yanga na simba za msimu wa 2024/25 kwa staili ya wamachinga, huku akitangaza bei ya Dola 50 Sh135,000), kwa jezi ambayo hapa nchini haizidi Sh40,000.
Mapinduzi makubwa katika utengenezaji na uuzaji wa jezi kwa klabu na kukua kwa utamaduni wa kuvaa jezi za timu kwa mashabiki na wasio mashabiki wa klabu hizo, kumefungua fursa na mnyororo mkubwa wa thamani. Kuanzia msanifu, klabu, wasafirishaji, maduka na hata wamachinga kila mmoja anapata tonge kutoka biashara hiyo.
Mbali na faida za kifedha, biashara ya jezi imelitangaza sana soka la Tanzania na chapa za klabu kama Simba, Yanga na Azam.
Najaribu kudodosa kujua kama kuna nchi barani Afrika ambako katika kila kundi la watu unalokutana nalo hutakosa aliyevalia jezi ya moja ya klabu hizi.
Angalia jezi za Liverpool, Manchester United, Juventus, Real Madrid na nyinginezo za ughaibuni zinavyopungua kwa kasi hapa Tanzania.
Baba, mama na watoto wote wanataka kujinasibisha na klabu za hapa nchini. Uzalendo unajengeka kupitia jezi za timu hizi.
Hii ni fursa kubwa sana kwa klabu kujipatia mashabiki ndani na nje ya nchi na hata klabu nyingine zinatakiwa kuhamasihsa wanachama na mashabiki zao kupenda kuvaa jezi za timu zao.
Klabu inapokuwa na wafuasi wengi inakuwa ni soko kubwa litakalovutia uwekezaji mkubwa utakaochochea na kuiwezesha timu kufanya vizuri na kuleta furaha na kwa mashabiki na taifa kwa jumla.
Klabu za Ulaya kama Barcelona, Real Madrid, Bayern Munich, Liverpool, Arsenal, Manchester United, Juventus, Chelsea, Manchester City na nyingine nyingi zinatengeneza fedha nyingi kutokana na biashara ya jezi zao na huzitumia kwa ajili ya kugharimia usajili za wachezaji wakubwa na mahitaji mengine. Hili hata hapa linawezekana.
Uelekeo ni mzuri, kutoka kuvaa masurupweta hadi kuwa na jezi jozi tatu kwa timu na nyingine nyingi kwa ajili ya mashabiki, Kutoka kuwa ombaomba, kauka nikuvae hadiu kuwa wauzaji wakubwa wa jezi, ni hatua kubwa sana.
Sitashangaa siku moja kuona kazi nzuri za kina Sheria Ngowi, GSM, MO, Vunja Bei, Kassim Dewji, Sandaland na kufanya vizuri kwa timu nyumbani na kimataifa zikavutia chapa kubwa kama Nike na Adidas kuomba kandarasi.
Mwandishi wa makala haya ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kwenye simu yake hapo juu.