Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinawapanga vema watumishi walioajiriwa hivi karibuni ili wasaidie kutoa huduma katika maeneo yote, zikiwemo hospitali.
Amesema Serikali kwa sasa haina uwezo wa kufikia asilimia 100 ya mahitaji ya watumishi, lakini angalau wachache waliopo wagawanywe ili wawanufaishe wananchi wote.
Rais Samia ameyasema hayo leo Ijumaa, Agosti 2, 2024 alipozungumza na wananchi wa Kilosa, wakati wa uzinduzi wa Daraja la Berege, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
Mkuu huyo wa nchi ametoa maelekezo hayo wakati akijibu ombi ya Mbunge wa Kilosa (CCM), Profesa Palamagamba Kabudi aliyeomba wapatikane watumishi wa afya katika zahanati na vituo vya afya wilayani humo.
Akimjibu amesema “hivi karibuni Serikali iliajiri watumishi wengi, mgao utakapokuja hapa, halmashauri ifanye mgao mzuri ndani ya halmashauri hii ili vituo vya afya vyote na hospitali zilizoko ndani ya wilaya hii zipate madaktari na wauguzi,” amesema.
Sambamba na hilo, amesema daraja alilolifungua litasaidia kuwaunganisha wananchi na kuvusha mazao kwa magari makubwa badala ya pikipiki walizokuwa wanatumia awali.
“Kujengewa daraja ni jambo moja, kulitunza ni jambo lingine. Kama mlivyosikia daraja hili limetumia fedha nyingi, niwaombe sana tunzeni daraja hili litumike miaka mingi vizazi na vizazi,” amesema.
Vilevile, ameridhia ombi la Profesa Kabudi la kubadili majengo yaliyokuwa ya World Vision kuwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameeleza sababu za kufanya ziara ya siku sita mkoani Morogoro ikiwa ni pamoja na kutatua kero zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.
Sababu nyingine amesema ni kusalimiana na wananchi wa Morogoro akisema tangu ashike uongozi Machi 19, 2021 kutoka kwa mtangulizi wake Dk John Magufuli hakuwahi kufanya ziara ya kikazi mkoani humo.
“Nimekuja kuwaona ndugu zangu toka mwaka 2021, nilipokabidhiwa dhamana sikuja kuonana nanyi, nimeamua kuja tuonane, wengi mnahamu ya kuniona. Nimekuja kusikiliza shida zenu tuzichukue na kuzifanyia kazi,” amesema Rais Samia.
Mbali na hilo, mkuu huyo wa nchi amesema ziara hiyo ina lengo la kuona matokeo ya fedha zinazotolewa kwa lengo la kuondoa changamoto za wananchi kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ya afya inayotekelezwa.
“Bahati nzuri asubuhi nimeanza na kutembelea Hospitali ya Gairo, nimeridhika na matumizi ya fedha pamoja kazi iliyofanyika pale. Ni hospitali nzuri yenye vifaa vya kisasa, naomba tuitunze ili iendelee kutupa huduma bora,” amesema Rais Samia.
Pia, Rais Samia amesema kupitia ziara hiyo, ataweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ambayo Serikali imeshusha fedha kwa ajili ya utekelezaji.
“Jingine nimekuja kujionea maendeleo ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na mvua kubwa za El-Nino,”amesema Rais Samia.
Mvua kubwa zilizonyesha mapema mwaka huu zilisababisha uharibifu wa miundombinu hasa ya barabara za kilomita 3,115 kati ya kilomita 6256.9 zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura).
Pia, makalavati 211 kati ya 3,500 yanayohudumiwa na Tarura yalisombwa na maji, changao hiyo ilisababisha baadhi ya watumiaji wa barabara kusitisha kutoa huduma zao kwa wiki kadhaa.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amewataka wananchi wa Morogoro kutunza amani iliyopo ili viongozi watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.
Sambamba na hayo,, amewataka wananchi wa Morogoro kujitokeza kwa wingi katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongaji utakaofanyika mwisho mwa mwaka huu.