Sababu mgonjwa kupata nafuu saa chache kabla ya kifo

Dar es Salaam. Kuna hadithi nyingi kuhusu uzoefu wa maisha ya mwisho ya binadamu. Wengine hubishana kwamba wanaofariki dunia huwa hawawezi kuhisi maumivu wala kusikia chochote kwa sababu wameshaingia katika ulimwengu mwingine.

Wengine husema wanaofariki hupata nguvu nyingi, huagiza chakula wapendacho, huongea kama walishafikia hatua ya koma au husimama na kutembea.

Hali hii huwafanya wanaomuuguza mgonjwa kupata faraja na matumaini, lakini wanapojiandaa kuondoka hospitali, hali hubadilika na mgonjwa kuaga dunia.

Hali hiyo kitaalamu hujulikana kama ‘surge phenomenon’, ikiwa na maana ya mwelekeo wa ghafla usioeleweka.

“Ni taswira isiyoeleweka kwa uhakika, maana hujui lini mgonjwa huyu atakufa au lini atapona, mtaalamu wa afya huwezi kumwambia mgonjwa atakufa kesho, maana unaweza kuona hivyo na kesho akapata nguvu zaidi akapona na ndiyo maana huitwa ‘surge phenomenon,” anasema Dk Ali Mzige, mtaalamu wa afya ya jamii na mkurugenzi mstaafu wa Huduma za Kinga katika Wizara ya Afya.

Ripoti ya mwaka 2023 ya Maktaba ya Kitaifa ya Tiba ya Marekani iliyofanya utafiti juu ya ishara na dalili za mwisho wa maisha kwa watu waliougua kwa muda mrefu au ugonjwa mkubwa, iligundua kuwa asilimia 84 ya watu wanaopatwa na hali hiyo, hufariki ndani ya wiki na asilimia 43 ndani ya saa 24.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, hali hii inapowapata wagonjwa wanaokaribia kufariki, huwafanya kuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali. Hii kwa kawaida hutokea siku, saa au hata dakika chache kabla ya mtu kupoteza uhai.

Kisayansi, hali hiyo hurejelea ufahamu wa mwisho katika kipindi kisichojulikana kabla ya kifo.

Ufanyaji kazi wa ubongo wa mgonjwa huongezeka, haswa huwa na utendaji wa hali ya juu wa utambuzi, kama vile kumbukumbu na fahamu kama zilikuwa zimepotea.

Wagonjwa waliolala kwa muda mrefu hutoka kitandani na kuanza kujihudumia, kutembea na wale walio nyumbani huuliza iwapo wanaweza kwenda matembezi au katika shughuli zao.

“Babu alipata hali hiyo kabla ya kifo chake,” anasimulia Anuwar Lyimo, aliyepoteza babu yake Februari 2023, baada ya kumuuguza kwa takribani miaka 12.

“Alikuwa akiugua kisukari kwa muda mrefu. Tulimuuguza nyumbani na ilipofika mwaka 2021 akawa mtu wa kulala tu, alipata vidonda mgongoni na baadaye alipona. Machi 2022 alipata tatizo la moyo na baadaye walisema figo pia zina shida kwa kuwa alitumia dawa za sukari zaidi ya miaka 25,” anasimulia Anuwar.

Anasema huo ulikuwa mwanzo wa kulazwa na kuruhusiwa na baadaye alifanyiwa upasuaji wa moyo.

“Alizidiwa Desemba mwaka 2022 akalazwa moja ya hospitali kubwa ya moyo hapa nchini. Alitibiwa hapo na alipozidiwa alipelekwa ICU, lakini wiki moja kabla ya kifo chake alianza kuongea na akaruhusiwa kutoka ICU. Alisimama kitandani na tulifurahi sana kama familia, lakini siku chache baadaye akazidiwa ghafla na kufariki.”

Uzoefu wa Anuwar unawapata ndugu wengi wa wagonjwa, lakini madaktari wanasema watu wanaokaribia kufariki, baadhi yao huonyesha dalili ambazo wataalamu wa afya huzibaini, mojawapo ikiwa ni hiyo.

Hata hivyo, Daktari bingwa wa upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mugisha Nkoronko anasema hali hiyo hutokea kwa wagonjwa wengi lakini hakuna sababu za kisayansi, ingawa wengi huhusianisha hali hiyo kati ya mgonjwa mmoja na mwingine.

Dk Mugisha anasema kimsingi mwili hushindwa kufanya kazi katika maeneo mengi ya mwili wakati huo.

“Kale kanafuu kidogo watu wanakaona, lakini kimsingi mpaka mauti yanamkuta mwili hushindwa kufanya kazi katika maeneo mengi, viungo vingi vya mgonjwa huwa vimeshapata hitilafu kubwa. Kuna chembechembe zinazokufa na kuzaliwa kila siku na unapozidi kuzeeka kasi ya chembechembe kufa na kuzeeka huongezeka.

“Baadhi ya viungo vina chembechembe chache na seli zake haziwezi kujitengeneza upya, zikiwemo za ubongo, sasa kama mtu atawekewa mpira wa kupumua, wengi wakirudi kawaida huchukua muda kupata nafuu. Lakini kale kanafuu kadogo kanakoonekana, ndugu mnaona yupo vizuri, tofauti na jana, lakini kimsingi ndani ya mwili kasi ya viungo kufa huwa ni kubwa kuliko kasi ya kupona,” anasema Dk Mugisha.

Anasema wako baadhi ya wagonjwa ambao hupata nafuu ndogo. “Pengine huwa ni ishara ya kwamba tunaweza kufanya kazi zaidi ya kumsaidia, lakini bahati mbaya hali huwa inabadilika na kuingilia kati ugonjwa wake na kufariki.”

Anasema wanaoshindwa kupumua hupata nafuu kidogo na wanakufa kwa aina moja kwa kushindwa kuupatia ubongo na moyo hewa ya kutosha kufanya kazi.

Related Posts