Samia ampigia chapuo Profesa Kabudi kiaina

Dar/Moro. Rais Samia Suluhu Hassan ni kama amempigia chapuo Mbunge wa Kilosa (CCM), Profesa Palagamba Kabudi, achaguliwe tena na wananchi wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

Hiyo imetokana na kauli yake mbele ya wananchi wa Kilosa aliyoitoa leo Agosti 2, 2024 akisema:“Endeleeni kuniletea Kabudi.”

Kauli inayofanana na hiyo aliitoa pia alipokuwa Dumila mkoani Morogoro, alipowataka wananchi wa eneo hilo wamchagulie viongozi wazuri wanaotokana na CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba, 2024.

Rais Samia alimnadi Profesa Kabudi alipozindua daraja la Berege wilayani Kilosa akiwa katika ziara ya siku sita mkoani Morogoro.

Kabla ya kuwataka wananchi  waendelee kumchagua mbunge huyo, alianza kwa kumsifu kwa utendaji wake jambo alilosema amekuwa akimtumia hata serikalini.

“Ndugu zangu, tunapozungumza wabunge Kilosa mmepata mbunge. Mbunge huyu si kwenu tu hata mimi namtumia kwenye mambo mengi. Nikikwamakwama huko nauliza jamani Kabudi yupo, nikiambiwa yupo nasema hebu muingizeni kamati hiyo anichapie kazi. Kwa hiyo nawashukuru sana wana-Kilosa endeleeni kuniletea Kabudi asanteni sana,” amesema.

Akiwa Dumila, Rais Samia aliwataka wananchi wa eneo hilo katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu, wamchagulie viongozi wazuri akisema wale wanaotokana na CCM.

Profesa Kabudi aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria aliachwa katika baraza jipya la mawaziri lililotangazwa Januari 8, 2022.

Januari 10, 2022 akiwaapisha mawaziri

aliokuwa amewateua,  Samia alieleza Profesa Kabudi amempangia kazi maalumu.

Pamoja na Profesa Kabudi, mwingine aliyeachwa ni  aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

“Nina kaka zangu wawili, William Lukuvi na Palamagamba Kabudi ukiwatazama hao umri wao ni kama wangu na niliowateua hamfanani kabisa kwa hiyo kaka zangu hawa nimewavuta waje kwangu ili waje wanisimamie kuwasimamia nyie kwa hiyo kuwaacha kwangu kwenye ile orodha hapo wote ni wadogo na mnahitaji kusimamiwa vizuri.

“Kaka yangu Kabudi amefanya kazi nzuri sana kusimamia mazungumzo ya Serikali na mashirika na ndiyo kazi ninayotaka nimkabidhi sasa kindakindaki aendelee na kazi hiyo ila kazi yake kwa sababu haipo kwenye muundo haitangazwi, mashirika yote kazi zote zitakazoingia ubia na Serikali yeye ataongoza hiyo timu kwa hiyo yeye ni baba mikataba,” alisema Rais Samia.

Novemba 13, 2020 hayati Rais John Magufuli alimteua Profesa Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, nafasi aliyoitumikia katika Baraza la Mawaziri kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka huo.

Katika hatua nyingine, Rais Samia akiwa ziarani mkoani Morogoro ameziagiza halmashauri nchini kuhakikisha zinawapanga vema watumishi walioajiriwa hivi karibuni ili wasaidie kutoa huduma katika maeneo yote yenye uhitaji.

Amesema Serikali kwa sasa haina uwezo wa kufikia asilimia 100 ya mahitaji, lakini angalau wachache waliopo wagawanywe ili wawanufaishe wananchi wote.

Serikali imetangaza nafasi za ajira 11,015 za sekta ya elimu na zingine 9,483 katika sekta ya afya.

Rais Samia ametoa maelekezo hayo akijibu ombi la Profesa Kabudi aliyeomba kupatikana kwa watumishi wa afya katika zahanati na vituo vya afya wilayani Kilosa.

“Hivi karibuni Serikali iliajiri watumishi wengi, mgawo utakapokuja hapa, halmashauri ifanye mgawo mzuri ndani ya halmashauri hii ili vituo vya afya vyote na hospitali zilizoko ndani ya wilaya hii zipate madaktari na wauguzi,” ameagiza.

Kuhusu daraja la Berege amesema litasaidia kuwaunganisha wananchi na kuvusha mazao kwa magari makubwa, badala ya pikipiki walizokuwa wanatumia awali.

“Kujengewa daraja ni jambo moja kulitunza ni jambo lingine. Kama mlivyosikia daraja hili limetumia fedha nyingi, niwaombe sana tunzeni daraja litumike miaka mingi vizazi kwa vizazi,” amesema.

Rais Samia pia ameridhia ombi la Profesa Kabudi la kubadili majengo yaliyokuwa ya shirika la World Vision kuwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi.

Akiwa Dumila kuelekea Morogoro Mjini, Rais Samia alitoa Sh20 milioni kwa ajili ya uboreshaji wa soko la mbogamboga la Dumila.

Sababu ziara ya siku sita

Akiwa wilayani Gairo, Rais Samia alitaja sababu ya kutenga siku sita za ziara mkoani humo, akisema ni kutatua kero zinazowakabili wananchi na kuwasalimu kwa kuwa hakuwahi kufanya hivyo katika eneo hilo, tangu alipoapishwa kuwa Rais Machi 19, 2021.

“Nimekuja kuwaona ndugu zangu tangu mwaka 2021, nilipokabidhiwa dhamana sikuja kuonana nanyi, nimeamua kuja tuonane wengi mna hamu ya kuniona. Nimekuja kusikiliza shida zenu tuzichukue na kuzifanyia kazi,” amesema.

Dhamira nyingine ya ziara hiyo amesema ni kuona matokeo ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya kuondoa changamoto za wananchi kupitia miradi mbalimbali kama zinatumika vema.

“Bahati nzuri asubuhi nimeanza kutembelea Hospitali ya Gairo, nimeridhika na matumizi ya fedha na kazi iliyofanyika pale. Ni hospitali nzuri yenye vifaa vya kisasa, naomba tuitunze ili iendelee kutupa huduma bora,” amesema.

Kupitia ziara hiyo, amesema ataweka mawe ya msingi na kuzindua miradi iliyogharimiwa na Serikali ili kuboresha huduma kwa wananchi.

“Jingine nimekuja kujionea maendeleo ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na mvua kubwa za Elnino,” amesema.

Mvua kubwa zilizonyesha mapema mwaka huu zilisababisha uharibifu wa miundombinu hasa ya barabara za kilomita 3,115 kati ya kilomita 6,256.9 zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura).

Pia makalavati 211 kati ya 3,500 yanayohudumiwa na Tarura yalisombwa na maji, changamoto hiyo ilisababisha baadhi ya watumiaji wa barabara kusitisha kutoa huduma zao kwa wiki kadhaa.

Rais Samia amewataka wananchi wa Morogoro kuitunza amani iliyopo, ili viongozi watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.

Pia amewataka kujitokeza kwa wingi katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongaji utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Related Posts