Ikiwa ni Siku moja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kuzindua Reli ya Mwendokasi (SGR) watalii ambao ni watumishi wa kada ya ualimu zaidi ya 1000 kutoka mkoa wa Dar es Salaam wametumia usafiri wa reli hiyo kutembelea Hifadhi ya Taifa Mikumi.
Ziara hiyo iliyoratibiwa na Ofisi ya mkoa wa Dar es Salaam imelenga kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Rais Samia ikiwemo kutangaza vivutio vilivyopo Hifadhi za Taifa ambapo kwa umoja wao walichagua Hifadhi ya Taifa Mikumi lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia.
Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es salaam Dkt. Toba Nguvila, amesema kuwa watalii hao ambao ni walimu wa mkoa wa Dar es Saam wameamua kuchangisha fedha zao wenyewe kwa ajili ya kuja kutembelea Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa kutumia usafiri wa reli ya kisasa ya SGR lengo likiwa ni kumuunga mkono Rais Samia.
“Baada ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kuizindua reli hii, walimu wa mkoa wa Dar es Salaam wameamua kuuunga mkono juhudi zake na ndiyo sababu ya kuamua kuchangishana fedha kuja kutalii hapa hifadhi ya Mikumi”alisema Dkt. Nguvila.
Aidha, Katibu Tawala huyo aliupongeza uongozi mzima wa Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa kutengeneza miundombinu inayofikika kwa urahisi ambapo alitoa wito kwa watumishi wengine kuiga mfano wa walimu hao kutembelea hifadhi za Taifa kuona vitutio hasa wanyama mbalimbali wanaopatikana katika hifadhi hizo kutalii pamoja na kuimarisha afya ya akili.
“Naipongeza Hifadhi hii ya Mikumi kwa mapokezi tuliyoyapata,tumeona wanyama wengi kabla na baada ya kuingia hifadhini tunaahidi kwamba tutakuwa mabolozi wa hifadhi hii popote pale tutakapokuwa”alisema Nguvila.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi Herman Mtei,aliwapongeza walimu hao kwa kuyaishi maono ya Rais Samia vitendo kwa kutenga muda wao kwa ajili ya kutembelea hifadhi ambapo aliongeza kwamba uwepo kwa reli ya SGR kumewarahisishia watalii wengi kufika katika hifadhi hiyo.
Pia,Mhifadhi Mtei aliongeza kuwa TANAPA Kanda ya Mashariki ambayo inasimamia Hifadhi ya Mikumi, Milima ya Udzungwa,Nyerere pamoja na Saadani imejipanga kikamilifu kuwapokea wageni mbalimbali watakaokuwa wakitembelea hifadhi hizo kutokana na usafiri wa kufika maeneo hayo kurahisishwa na reli ya SGR.
“Uwepo wa SGR kwetu sisi ni ushindi mwingine mkubwa katika sekta ya utalii nchini na katika kanda ya Mashariki,Awali Rais wetu Samia alianza kwa kuboresha miundombinu ya hifadhi hizi ambapo Kupitia fedha zilizotolewa na Rais Samia tumewekeza kwenye miundombinu vya kutosha ili kuhakisha watalii wengi wanaokuja hapa Mikumi na hifadhi zingine wanastarehe vyema ” alisema Mtei.
Naye, Mwalimu Bundala Masanyiwa,kwa niaba ya walimu wenzake aliupongeza uongozi wa hifadhi hiyo kwa ujumla kutokana na na kuwekeza miundombinu inayopitika kwa urahisi ambapo aliahidi atakuwa balozi wa utalii kwa kuzitangaza hifadhi za Taifa hususani hifadhi ya Mikumi.