Dar es Salaam. Wanywaji wa bia nchini Tanzania, leo Ijumaa Agosti 2, 2024 wanaungana na wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Bia inayolenga kuwaleta pamoja marafiki katika kufurahia ladha ya bia.
Siku ya Kimataifa huadhimishwa Ijumaa ya kwanza ya Agosti kila mwaka ambapo kwa mwaka huu imeangukia Agosti 2.
Maadhimisho ya siku hii yalianzia huko Santa Cruz, California nchini Marekani, mwaka 2007. Hadi sasa siku hii inasherehekewa katika miji 207 katika nchi 50 duniani zilizotawanyika katika mabara sita.
Lengo la kuanzishwa kwa kilevi hiki lilikuwa ni kuwaleta pamoja kufurahia ladha ya bia, kuwapongeza wanaozalisha bia na wanaohudumia pamoja na kuwaunganisha watu wa mataifa yote duniani kupitia kinywaji hiki pendwa.
Kila jamii duniani ina aina yake ya bia na historia inaonyesha kinywaji hiki kilianza kutengenezwa kisasa katika karne ya 18, hata hivyo, kabla ya hapo zilikuwepo pombe mbalimbali zilizokuwa zikitengenezwa kienyeji kutokana na teknolojia kuwa duni.
Tanzania pia ina wanywaji wengi wa bia ambao kuanzia siku za mwisho wa wiki kama Ijumaa, Jumamosi na Jumapili, wanakusanyika kwenye baa mbalimbali na kujumuika na watu tofauti.
Akizungumzia siku hii, mnywaji wa bia, Gaston Kimario amesema anapenda kunywa bia kwa sababu inampa ujasiri wa kuzungumza na watu na kwa njia hiyo amekuwa akikutana na watu wapya wanaomfungulia fursa mbalimbali.
“Bia inanipa vibe (msisimko), nakuwa najiamini kumfuata mtu, nikaongea naye na tukawa marafiki. Nimepata dili nyingi kwa watu niliokutana nao baa tu. Nafurahi kama kuna siku hii, nitasherehekea pia,” amesema Kimario ambaye ni mfanyabiashara.
Mwandishi mmoja wa habari ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amesema anakunywa bia ili kupunguza msongo wa mawazo unaosababishwa na kazi anayoifanya. Amesema anapenda kinywaji hicho kwani kinampa furaha hasa anapokutana na marafiki.
“Nakunywa kwa kujumuika na watu, pombe hainywewi nyumbani, baa ndiyo kuna burudani. Sijui nitaacha lini, lakini naendelea kunywa bia,” amesema mwanamke huyo.
Mmiliki wa baa moja iliyopo Pugu, jijini Dar es salaam, Onesmo Lyanga amesema hafahamu kama kuna siku ya kimataifa ya bia, hata hivyo, amesema kinywaji hicho hakiepukiki na kutokana na hilo aliona fursa na kuanzisha baa ili kujiingizia kipato.
“Miaka ijayo nitakuwa naifanya siku hii kuwa kubwa, mie nafanya biashara, siku kama hii ni fursa kwangu. Nitawawekea wateja wangu burudani itakayosindikiza unywaji wao,” amesema Lyanga.
Mkazi wa Katoro, Mkoa wa Geita, Frank John anasema kinywaji hicho kinapotumika vizuri kinachangia mapato ya nchini na jamii kwa ujumla.
“Kuna watu wanategemea uuzaji wa vinywaji, wanasomesha, wanajenga na kuendesha maisha yao kwa hiyo ni jambo jema kutambua siku hii muhimu na kwa kweli pombe tamu asikwambie mtu,” amesema John.
Akizungumzia mtazamo wa kiimani, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Viongozi wa Dini, Askofu William Mwamalanga amesema Biblia inaelezwa ulevi unakaribisha uvivu, hivyo haoni umuhimu wa kuwa na siku ya bia duniani.
Amesema watu wanaolewa hawafanyi kazi na hawezi kutoa majibu kwenye changamoto zinazomkabili yeye au jamii yake, hivyo ameiomba serikali kupiga vita siku hiyo kuadhimishwa hapa nchini kwani ulevi ni laana.
“Mapato ya bia ni ya laanaa, huwezi kupata maendeleo kwa pesa za bia. Kuna nchi zimepiga marufuku ulevi na zimefanikiwa kimaendeleo, mfano nchi za Kiarabu kama Qatar, wana maendeleo na hawanywi pombe,” amesema Askofu Mwamalanga.
Askofu huyo amehoji kwamba kwanini kusiwe na siku ya kuhamasisha amani duniani badala ya ulevi wa bia. Amesema imani inakataza unywaji wa pombe kwa misingi kwamba Taifa la walevi haliwezi kufanikiwa.
“Mungu anasema mkalewe katika roho na siyo katika mwili. Watu wanaolewa hawawezi hata kutunza familia zao, pesa zote wanazopata zinaishia kwenye bia. Wanaonufaika ni kampuni za bia tu, mlevi hanufaiki chochote,” amesema askofu huyo.
Wakati wadau walieleza hayo, tahadhari mbalimbali zimekuwa zikitolewa na kampuni zinazotengeneza bia kuhusu matumizi ya kinywaji hicho. Kwanza, kuna tahadhari isemayo “Kinywaji hiki hakipaswi kuuzwa kwa walio chini ya miaka 18”.
Pia, tahadhari nyingine inayotolewa ni “Unywaji kupitia kiasi ni hatari kwa afya yako. Kadhalika, wanywaji wanaonywa kupitia usemi wa kimombo “Don’t drink and drive” (usinywe pombe na kuendesha).
Tahadhari hizi zote tatu zinaandikwa kwenye chupa ya bia ili kumkumbusha mnywaji kuchukua tahadhari kuhusu matumizi ya kilevi hicho pendwa hasa kwa vijana. Kupuuzwa kwa tahadhari hizo, mnywaji anaweza kujikuta akipata madhara kwa namna tofauti yatakayomfanya ajutie kutumia bia maishani mwake.