TANZANIA YAJIPANGA KUFANYA VIZURI KATIKA KRIKETI AFRIKA

Na Mwandishi Wetu

KOCHA wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 19 ya mchezo wa kriketi, Salum Jumbe, amesema wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye ardhi ya nyumbani katika mashindano ya mchezo huo ya divisheni ya pili Afrika.

Michezo hiyo ilianza kutimua vumbi jana kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Dar es salaam ambapo nchi nane za Afrika zinashiriki.

Akizungumza jana na waandishi wa habari katika mkutano wa kuzitambulisha nchi shiriki katika mashindano hayo, Jumbe alisema kutokufanya vizuri katika mashindano ya mwaka jana kwao ni wanachukulia kama chachu ya kuhakikisha wanafanya vizuri mwaka huu.

“Mwaka jana hatukufanya vizuri na kujikuta tukishuka daraja, mwaka huu mashindano haya yanafanyika hapa nyumbani, tumejipanga na tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunafanya vizuri na kupanda daraja,” alisema Jumbe.

Aidha, nahodha wa timu hiyo, Lakshi Bakrania, alisema waliumia sana mwaka jana kwa kutofuzu licha ya kujituma lakini mwaka huu wamejiandaa kuhakikisha wanaipeperusha vyema bendera ya Tanzania katia mashindano hayo.

“Mwaka huu tuna timu mpya na malengo mapya, tutapambana kuhakikisha tunafanya vizuri, haitapendeza kushindwa tukiwa kwenye ardhi ya n yumbani,” alisema Bakrania.

Kwa upande wake, mratibu wa mashindano hayo yanayoandaliwa Baraza la Kimataifa la Mchezo huo (ICC), ATif Salim, alisema mashindano hayo yatashirikisha nchi za NIgeria, Ghana, Sierra Leon, Malawi, Msumbiji, Botswana, Rwanda na wenyeji Tanzania.

“Nchi hizi zitagawanywa kwenye makundi mawili, na timu mbili katika kila timu zitasonga mbele kucheza fainali na moja kwa moja zitakuwa zimepanda daraja, timu moja tutaipata kwa kuchukua timu zilzioshika nafasi ya tatu kila kundi watacheza mchezo mmoja kusaka nafasi ya tatu ambayo ataungana na timu nne kuingia divisheni ya kwanza,” alisema Salim.


Related Posts