Dodoma. Upigaji kura kwenye uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) umekamilika na matokeo yanatarajiwa kutangazwa saa 11.00 jioni leo Agosti 2, 2024 mara baada ya kura kuhesabiwa.
Wagombea sita wanawania urais katika uchaguzi huo ambao ni Boniface Mwabukuzi, Ibrahim Bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda, na Sweetbert Nkuba na wengine kwenye nafasi nyingine mbalimbali.
Uchaguzi huo umeanza saa 12:30 asubuhi katika viwanja vya Jakaya Convention Center kulikuwa na vituo kadhaa vya kupigia kura kukiwa na baadhi ya askari polisi wakisimamia usalama.
Wanachama wa TLS walikuwa wakipiga kura kadri wanavyofika hadi vituo hivyo vilipofungwa saa 6.00 mchana.
Katibu wa Kamati ya Uchaguzi wa TLS, Nelson Frank, ameiambia Mwananchi leo Agosti 2, 2024, kuwa mawakili wamehamasika kupiga kura na uchaguzi umefanyika katika hali ya utulivu bila rabsha yoyote. Amesema anaamini shughuli nzima itahitimishwa salama na viongozi waliochaguliwa wataapishwa kesho Agosti 3, 2024 katika mkutano mkuu unaoendelea.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi huo wakati kura zikiendelea kupigwa, Wakili Aziza Msangi amesema umeenda vizuri lakini hawezi kusema chochote kwa wakati huu kwa sababu kura ni idadi.
“Hatuwezi kutabiri itakavyokuwa lakini hadi tunaendelea hivi sasa tunaona mambo yako shwari na hakuna shida yoyote,” amesema.
Mmoja wa wagombea, Boniface Mwabukusi, amesema anamshukuru Mungu uchaguzi unafanyika salama, japokuwa kuna changamoto ndogondogo na hivyo amewashauri wenzake kusubiri matokeo.
“Sisi wagombea tumeshakamilisha kazi yetu, tumewapa kazi leo wapiga kura ni zamu yao kufanya maamuzi yao, lakini mwisho wa siku mimi imani yangu ni ile ile kwamba wanaoshinda ama kushindwa ni wapiga kura, si wagombea,” amesema.
Baada ya kupiga kura yake, Tundu Lissu, makamu mwenyekiti wa Chadema, amesema uchaguzi huo umemkumbusha mbali ikiwemo namna alivyopigwa risasi miaka saba iliyopita.
“Siku ya leo inanikumbusha mambo mengi sana, mara ya mwisho kulikuwa na mawakili wakichagua namna hii na ambayo nilishiriki mimi Machi 18, 2017 siku niliyokuwa nagombea urais nilipigiwa kura kama hivi Arusha. Miezi mitano baadaye nikapigwa risasi hapa Dodoma, sijashiriki tena kwenye shughuli kama hii mpaka leo, kwa hiyo inanikumbusha mengi sana ya miaka ile.
“Uchaguzi huu wa TLS ni muhimu sana na ndiyo maana nchi nzima inasubiri moshi mweupe kutoka Dodoma kwa sababu mawakili wakisema, Taifa huwa linasikiliza. Kwa hiyo ni siku muhimu sana kwa mawakili, kwa taaluma ya sheria na kwa nchi yetu,” amesema Lissu.