UPANUZI WA KIWANDA CHA SUKARI KILOMBERO-K4 KUKIDHI MAHITAJI YA SUKARI NCHINI

Katika mkakati wa kuunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha nchi inakua na utoshelevu wa bidhaa ya Sukari, Kiwanda cha cha Sukari Kilombero kipo mbioni kukamilisha ujenzi wa upanuzi wa kiwanda chake cha K4. Kupitia mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika Agosti 1, Kampuni hiyo ilitangaza tukio kubwa la uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi huo unaotarajiwa kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi siku ya tarehe 04 Agosti.

Gharama ya upanuzi wa mradi huo itakuwa ni Sh 744 bilioni punde mradi utakapo kamilika mwezi Juni 2025. Kukamilika kwa mradi huu kutaongeza uwezo wa Kampuni hiyo katika kuzalisha Sukari kutoka tani 126,000 kwa mwaka hadi kufikia tani 271,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya Sukari Kilombero Ndugu Derick Stanley alisema “Kiwanda hiki cha K4 kilianza kujengwa miaka miwili iliyopita, ambapo ni kiwanda cha kisasa pia ni kiwanda kinachoongoza kwa ukubwa, Afrika Mashariki. Kukamilika kwa kiwanda hiki kutapunguza changamoto za uhaba wa Sukari hapa nchini, hivyo kuisaidia Serikali yetu kutoagiza Sukari nje ya nchi”.

Ndugu Derick Stanley aliongeza kuwa “Mradi unaenda kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya Uchumi hapa nchini, hii ina ambatana na dira ya Serikali kwamba ifikapo mwaka 2025 nchi ya Tanzania iwe na utoshelevu wa Sukari ya matumizi ya majumbani”.

Kupitia kiwanda hiki cha K4 kutakuwa na ongezeko la mapato kwa wakulima wa bonde la Kilombero kutoka shilingi za kitanzania bilioni 75 hadi kufikia takribani shilingi bilioni 165 kwa mwaka. Sambamba na ongezeko la idadi ya wakulima kutoka 8,000 hadi kufikia takribani 16,000.

Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano na Mahusiano kwa wadau, Bw. Victor Byemelwa amewahimiza wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi siku hiyo ili kushuhudia tukio hilo la kihistoria ambalo linaenda kuinua maisha ya wakulima kupitia uzalishaji wa miwa.

Naye Meneja wa Masuala ya Biashara wa Kampuni ya Sukari Kilombero Bi. Willa Haonga aliwataka akina mama kuchangamkia fursa ya mradi huu kwani tafiti zinaonesha kuwa wanaume ndio wanaongoza kwa biashara ya kilimo cha mua. Aliwataka akina mama kuchangamkia fursa hii ili kujiinua kiuchumu na kuunga juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekua mstari wa mbele katika kuwainua wanawake.

Bw. Derick Stanley, Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano Kampuni ya Sukari Kilombero (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Agosti 1, katika ofisi za Kampuni hiyo zilipozo wilayani Kilombero. Bw. Derick alizungumzia suala zima la juhudi zilizowekwa na Kampuni juu ya mradi wa upanuzi wa Kiwanda cha Kilombero K4 kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya Sukari Tanzania. Katika hatua hiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uwekaji wa jiwe la msingi kiwandani hapo. Pamoja nae pichani kushoto ni Bw.Victor Byemelwa Meneja Mawasiliano na Mahusiano kwa Wadau na Bi. Willa Haonga, Meneja wa masuala ya Biashara.

Related Posts