Dar es Salaam. Migogoro ya vizimba vya biashara kwenye masoko nchini ni suala linalojitokeza mara kwa mara.
Kwa kiasi kikubwa migogoro hii huwaathiri wafanyabiashara, mamlaka za serikali za mitaa na maendeleo ya masoko kwa ujumla.
Ufuatiliaji uliofanywa na Mwananchi katika baadhi ya masoko nchini, migogoro hiyo huchangiwa na utaratibu wa utoaji wa vizimba unaodaiwa kugubikwa na upendeleo au rushwa, hivyo wafanyabiashara wachache wenye uwezo wa kifedha au ukaribu na viongozi wa soko huvihodhi kisha kupangisha kwa wengine.
Baadhi ya wanaovihodhi wanadaiwa kuongeza kodi na ada za vizimba kwa kuvikodisha kwa wafanyabiashara wengine, huku wao wakijinufaisha kwa kuongeza gharama ya kupangisha.
Mbali ya hilo, kuna ukosefu wa uwajibikaji ikibainishwa hakuna uwazi katika usimamizi wa masoko.
Baadhi ya viongozi wa masoko na maofisa wa serikali za mitaa wanatuhumiwa kutumia vibaya nafasi zao kwa faida binafsi.
Ni kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara wadogo maarufu Wamachinga na wasio rasmi hujipatia maeneo ya kufanya biashara kiholela, hivyo kusababisha migogoro kati yao na wale waliolipia vizimba.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Viwanda na Biashara, Tanzania inakadiriwa kuwa na wafanyabiashara wadogo zaidi ya milioni 3.1 wakiwa ni asilimia 23.4 ya nguvu kazi ya Taifa na imechangia asilimia 27 ya pato la Taifa.
Julai 30, 2024 Soko la Tandale jijini Dar es Salaam ambalo limekarabatiwa kuliibuka mgogoro wafanyabiashara wa mboga na matunda wakipinga mpango wa viongozi wa soko hilo, wakidai wenzao wa nafaka wanapendelewa.
Soko hilo lililoanza kujengwa mwaka 2019, limegharimu Sh11 bilioni likiwa na ghorofa tatu na lina uwezo wa kuhudumia wafanyabishara 2,500. Ndani ya soko kuna eneo la vizimba, mabucha ya kisasa na maduka makubwa.
Kiongozi wa wafanyabiashara wa matunda, Pius Setebe anadai mwenyekiti wa soko hilo, Juma Dikwe anaonyesha upendeleo katika upangaji wafanyabiasara akiwapendelea wanaojihusisha na nafaka.
Kambi Ramadhani, mfanyabaiashara wa matunda anasema wapo hapo tangu mwaka 1986 walipohamishwa barabarani Manzese. Mwaka 2019 walihamishwa kupisha ujenzi wakiahidiwa kupewa kipaumbele litakapomalizika.
Ramadhani amesema Julai 29, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule alikutana nao na kuwaeleza soko limeshakamilika, hivyo ofisa biashara na mwenyekiti wa soko watakuwa na dhamana ya kuwapanga.
Mwenyekiti wa soko hilo, Dikwe amesema kitaalamu biashara za nafaka na za matunda haziwezi kuchanganywa sehemu moja na kwa kuwa ndio zinaongoza kwa kuzalisha takataka, hivyo wakaona ni vema wawaweke chini ili kuwe na urahisi katika uzoaji taka.
Dikwe amesema suala hilo walishirikishwa tangu awali soko lilipoanza kujengwa, hivyo anashangazwa kuona wanapinga.
Amesema wanapanga wafanyabiashara kutokana na orodha iliyopo kwenye kitabu, akieleza kabla soko hilo kujenga walikuwa 1,055 lakini kipindi cha ujenzi walipungua na kubaki 350.
Mwenyekiti Serikali ya Mtaa wa Sokoni ambapo soko hilo lipo, Salum Kaponda amesema mgogoro huo ameufikisha ngazi ya wilaya ambayo inaushughulikia.
Hivi karibuni baada ya kukamilika ukarabati wa Soko la Kariakoo, Julai 11, 2024 wafanyabiashara zaidi ya 800 waliandamana kuelekea ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam wakihoji kutokuwapo kwenye orodha ya wafanyabiashara wanaotakiwa kurejeshwa katika soko hilo lililokamilika ukarabati wake baada ya kuungua Julai, 2021.
Shirika la Masoko Kariakoo lilitoa orodha ya wafanyabiashara watakaorejea sokoni na kati ya watu 1,662 waliokuwapo waliokidhi vigezo kurejea ni 891.
Hata hivyo, akizungumza na wafanyabiashara hao, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema baada ya uhakiki wa awamu ya kwanza kufanyika, majina ya watu 819 ndio waligundulika hawana mawaa.
Alisema kabla ya soko kuungua, kulikuwa na uholela usiokuwa na tija kwa mtu mmoja kuchukua vibanda zaidi ya 10 kuvipangisha na kujikuta soko hilo limemezwa na madalali.
“Kati yenu hapa wapo wafanyabiashara, wapo madalali jambo hili tutaelewa tu japo papo patakapouma na kwa utaratibu wa sasa wa soko niwaambie tumekata mzizi wa udalali,” alisema.
Chalamila alisema tatizo la watu kuhodhi vizimba ni kutokana na tabia yao ya kujiona kuwa wana haki na hayo maeneo ya Serikali na wengine hata kurithishana vizazi na vizazi.
Baadhi ya wafanyabiashara walidai kupata vizimba baada ya kulipa Sh51,000 kwa mwezi na ushuru kwa siku Sh1,700 kwa Shirika la Masoko Kariakoo.
Kwa wanaofanya biashara nje ya soko hilo walidai kulipa Sh85,000 kwa Manispaa ya Ilala.
Baadhi ya wanaohodhi maeneo wamekuwa wakiyakodisha kwa Sh200,000 na hupaswa kulipa kwa miezi sita, yaani Sh1.2 milioni na kama ukitaka kuuziwa liwe lako unalipa Sh3 milioni.
Mfanyabiashara Brenda Kamugisha anasema wafayabiashara wanakimbilia kununua maeneo hayo wakiamini fedha zao zitarudi ndani ya muda mfupi.
Kwa upande wa soko la Machinga Complex ambapo jengo lake lilijengwa mahususi kwa ajili ya machinga, mmoja wa madalalai sokoni hapo Jaffar Masha anasema wafanyabiashara wengi wamepangishwa kwa kati ya Sh30,000 hadi Sh50,000 na mtu anapaswa kulipa miezi mitatu hadi sita.
“Hali ya ukodishaji imejitokeza baada ya vizimba kujaa hii ni kutokana na wafanyabiashara waliounguliwa soko la Karikaoo kuhamishiwa hapo,” anasema.
Ni kutokana na hilo, Masha anadai wapo walionunua vizimba kati ya Sh8 milioni hadi Sh9 milioni.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Mwenyekiti Umoja wa Wamachinga Mkoa wa Dar es Salaam, Namoto Yusufu amekiri wapo wanaokodisha vizimba.
Ametoa mfano akisema meza zilizowekwa katika mitaa 11 ya Karikoo waliyoruhusiwa kufanya biashara watu wanakodishwa.
Amesema wamejitahidi kufanya uhakiki mara kwa mara ila usiri ni sababu ya watu kutowataja waliowakodishia.
Ni kutokana na hali hiyo anasema wamejikuta wakiongezeka kutoka wafanyabiashara 5,245 hadi kufika 7,628. Amesema Dar es Salaam pekee kuna wamachinga 360,000.
jijini Dodoma baadhi ya wafanyabiashara waliopewa vizimba na halmashauri ya Jiji wanadaiwa kuviuza kwa kati ya Sh1 milion hadi Sh3 milioni.
“Ukitaka vizimba vipo ila bei inategemeana na eneo kilipo vinaanzia Sh1 milioni hadi Sh3 milion na pia ukitaka kukodisha unapata kwa Sh50,000 hadi Sh100,000 inategemeana na maelewano na bidhaa unayoiuza,” anadai mmoja wa wafanyabiashara.
Anadai mauziano hayo huwahusisha viongozi wa soko.
Agnes Nicolaus amesema huwa analipa Sh150,000 kwa mwezi kwenye kizimba alichokodi kwa ajili ya kufanyia biashara na kwamba aliyemkodisha huwa anadai kodi ya miezi sita.
Mwenyekiti wa Soko la Machinga Complex, Athuman Ally amesema sheria za soko hilo haziruhusu kuuza, kukodi wala kurithisha kizimba cha kufanyia biashara na wanaofanya hivyo wanafanya kwa siri bila kushirikisha uongozi wa soko.
“Utaratibu wa kuomba vizimba kwenye masoko yetu upo na unajulikana ni lazima utume maombi kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma ambaye akiona kuna nafasi ya kufanyia biashara atakukabidhi kizimba chako kupitia kwa ofisa masoko wa Jiji na si kuuziana au kukodishana kiholela,” amesema Ally.
Amesema kuna kesi nyingi za watu kukiuka utaratibu kwenye soko hilo na wanachokifanya ni kuwanyang’anya vizimba na kuvitangaza upya kwa wanaohitaji ili Halmashauri isikose mapato yake.
Katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, hali hiyo inaonekana kudhibitiwa kutokana na uongozi kufuatilia waliowapangishia maeneo ya biashara.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Mwajuma Nasombe amesema wamekuwa wakiwachukulia hatua wanaopangisha wengine katika maeneo waliopewa.
“Wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao wanatuhujumu kwenye vibanda vya halmashauri, tunaendelea na utafiti na tutakwenda kuchukua hatua, kwani kwa mujibu wa mkataba ni kosa kuingia mkataba ndani ya mkataba, lakini tunao baadhi ya wafanyabiashara ambao siyo waaminifu, wao wameingia mkataba na halmashauri ambapo anakodishiwa kibanda kwa Sh100,000 au Sh200,000 lakini yeye anakwenda kumpangisha mfanyabiashara mwingine kwa Sh500,000,” amesema.
“Mbaya zaidi ni kwamba yeye analipwa kwa wakati na mtu aliyempangisha lakini yeye hailipi halmashauri, kwenye operesheni zetu sisi tunakwenda kwenye kibanda mfanyabiashara anakwambia mimi nilishamlipa mwenye kibanda, na anakuonyesha risiti zake ambazo zinaonyesha ameshamalizana na huyo mtu lakini yeye hajalipa halmashauri,” amesema.
Nasombe amesema kwa mwaka wa fedha uliopita wanadai kwenye vibanda vya biashara deni la zaidi ya Sh502 milioni na sehemu ya deni hilo, linatokana na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao, wamepangishiwa vibanda na wao kupangisha kwa watu wengine, ambapo licha ya kulipwa, hawajalipa halmashauri.
Mwanasheria wa Manispaa hiyo, Sifael Kulanga amesema wapangaji wa vibanda na maduka ikiwemo katika kituo kikuu cha mabasi Moshi, kwa mujibu wa mkataba waliosaini na halmshauri, haruhusiwi kumpangisha mtu mwingine bila ya kutoa taarifa.
“Kwa mujibu wa mikataba kipengele cha 3f na 5c (3), kinasema mpangaji yoyote ambaye amepangishwa na Manispaa haruhusiwi kmpangisha mtu mwingine bila kutoa taarifa kwa manispaa, lengo ni kwamba kusiwe na mikataba miwili kwa mpangaji mmoja,” amesema.
Mwenyekiti wa Soko la Kingalu Manispaa ya Morogoro, Khalid Mkunyegele amesema vitendo vya watu kuchukua vizimba na kupangishia wafanyabiashara wengine katika soko hilo kama vipo basi vitakuwa vinafanyika kwa siri, kwa sababu ipo mikakati iliyowekwa na uongozi wa soko kwa kushirikiana na halmashauri katika kudhibiti vitendo hivyo.
“Hapa sokoni kuna wafanyabiashara zaidi ya 3,000 ambao wanafanyabiashara mbalimbali na kuhusu kupangishana vizimba kinyume cha utaratibu jambo hilo linaweza likawepo, lakini ninafanyika kwa siri sana,” amesema Mkunyegele.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exhaud Kigahe, licha ya kusema kuwa suala hilo liko chini ya Ofisi ya Rais Tamisemi, amekiri kuwapo kwa tatizo hilo akitoa mfano wa Wilaya ya Mufindi anakotokea kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara waliotoa malalamiko.
Amesema jambo hilo limekuwa likifanywa na watu wasiokuwa waadilifu ambao wamekuwa wakifanya hivyo kujinufaisha.
Imeandikwa na Nasra Abdallah, Aurea Simtowe, Lydia Mollel, Hamida Sharif, Rachel Chibwete na Saddam Sadick.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.