Wakili afariki dunia Dodoma akihudhuria mkutano TLS

Dodoma. Wakili Maria Pengo (36) amefariki dunia ghafla usiku wa kuamkia leo Ijumaa jijini Dodoma alipokwenda kuhudhuria mkutano mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) unaoendelea.

Taarifa zilizosambazwa kwa mawakili zinasema kuwa mwili wa wakili huyo utasafirishwa leo usiku kwenda nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.

Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Renetha Mzanje amethibitisha kupokelewa kwa mwili wa wakili huyo saa 7:00 usiku wa kuamkia leo.

Leo Ijumaa Agosti 2, 2024, imetangazwa kwenye mkutano huo kuwa chama hicho kimeshafanya kila kitu, ikiwemo kulipia gharama za usafiri wa mwili huo na kuwataka mawakili kutoa rambirambi.

Wametangaza kuwekwa kwa boksi na namba kwa ajili ya kutumia rambirambi kwa wale wanaotaka kutuma kidijitali.

Vilevile, shughuli za mkutano huo zimesitishwa kwa muda ili kutoa fursa kwa mawakili hao kuuaga mwili wa mwenzao.

Mawakili wanachama wa TLS wako jijini Dodoma tangu jana kwa ajili ya mkutano mkuu, unaofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC) ambao pia umefanyika uchaguzi wa viongozi wa chama hicho katika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo rais.

Jumla ya wagombea sita wanawania urais wa chama hicho ambao ni Boniface Mwabukusi, Ibrahim Bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda na Sweetbert Nkuba.

Related Posts