BAADHI ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro, wamesema hawana deni na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa ahadi nyingi alizotoa amezitekeleza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Maelezo hayo ya wananchi yametolewa leo tarehe 2 Agosti 2024 na wananchi hao baada ya kusikiliza hotuba iliyotolewa na Rais Samia, Dumila wilayani Gairo, Morogoro.
Pia, wamesema wanaamini ahadi zilizotolewa na Rais Samia zitatekelezeka.
Miongoni mwa ahadi zilizotolewa na Rais Samia katika mkutano huo ni Serikali kuwatafutia wakulima masoko ya mazao pamoja na kutoa ruzuku ya alizeti.
Anorld Kalongola amesema “ziara ya mama tumeipokea, hatumdai chochote ahadi zote ametekeleza na kuna mambo tumemuomba amesema atatekeleza ataziweka kwenye ilani ya uchaguzi wa 2025/2030.”
Aidha, Kalongola amesema masoko yaliyotafutwa na Serikali kwa ajili ya mazao pamoja na utoaji ruzuku ya mbegu ya alizeti, vitaongeza uzalishaji wake mkoani humo na kuwainua kiuchumi wakulima.
Kwa upande wake Rehema Chuma, amesema Serikali Rais Samia imefanya kazi kubwa kuwakomboa wanawake katika sekta afya hususan wajawazito wanaojifungua watoto kwa kuwa amejenga hospitali na vituo vya afya hivi karibu na maeneo ya wananchi.
“Tunashukuru kwa ujio wa Rais Samia hapa kwetu Morogoro, sisi tunamshukuru sababu ametujengeea shule, vituo vya afya sasa hivi kina mama tunasaidika hususan kwenye suala la uzazi maana tulikuwa tunasumbuka sana,” amesema Rehema.