WAZIRI KIJAJI ATETA NA NAIBU BALOZI WA NORWAY

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na Naibu Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Kjetil Schie alipokutana naye ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo tarehe 01 Agosti, 2024. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Taifa cha Ufuatilaji wa Kaboni (NCMC) Prof. Eliakim Zahabu.

….

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amewaasa Watanzania kuchangamkia fursa za miradi itakayosaidia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia pamoja na kushiriki katika shughuli za kuendeleza uchumi wa buluu.

Hayo yamebainika wakati wa kikao kati ya Waziri Dkt. Ashatu Kijaji alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Kjetil Schie katika Ofisi ndogo jijini Dar es Salaam leo tarehe 01 Agosti, 2024.

Katika mazungumzo yao Mhe. Dkt. Kijaji ameishukuru Serikali ya Norway kwa ushirikiano na Tanzania hususan katika sekta ya uhifadhi wa mazingira ambayo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inaisimamia.

Amesema ni muhimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika juhudi zinazofanywa na Serikali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mbinu asilia.

Mhe. Dkt. Kijaji amesema anatambua makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali za Tanzania na Norway ziliyosaini mwaka 2023 katika maeneo mbalimbali yakiwemo kuwezesha upatikanaji wa fedha za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo, ametoa wito kwa watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais kuchangamkia fursa hiyo kwa kuandaa maandiko ya miradi ambayo itasaidia katika hifadhi ya mazingira kuwa endelevu.

Halikadhalika, amehimiza kuimarishwa kwa tafiti za mabadiliko ya tabianchi, ambazo zitasaidia katika kutambua namna ya kuimarisha mikakati ya kukabiliana nayo pamoja na kusaidia katika kilimo himilifu cha mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Naibu Balozi Schie amesema kuwa Noway imekuwa ikishirikiana na Tanzania kwa kipindi kirefu sasa hususan katika masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amefafanua kuwa katika ushirikiano kwanza kulikuwa na miradi miwili ya mwisho ambayo iliisha mwaka 2023 ambayo ni Mradi wa Kuazisha Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) na Mradi wa REDD unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Amesema katika makubaliano ya ushirikiano wa pili wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosainiwa mwaka 2023, kuna maeneo  yameliyofanyiwa kazi hadi sasa ambayo ni andiko la Mradi wa MRV4Tanzania lililowasilishwa na NCMC wakishirikiana na Taasisi ya Utafiti ya NIBIO ya Norway.

Ametaja eneo lingine ni Mradi wa UNCDF wakishirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Fedha wa kusaidia halmashauri tatu za Mkoa wa Dodoma namna ya  kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kupata fedha za mabadiliko ya tabianchi na Mradi wa utafiti wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi unaosimamiwa na COSTECH.

Naye Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme ametoa wito kwa Serikali ya Norway kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika nishati safi ya kupikia.

Amesema Tanzania ipo katika hatua ya kuhakikisha wananchi wanaachana na kutumia nishati isiyo rafiki wa mazingira na afya ya binadamu hivyo inahitaji kuungwa mkono na nchi washirika ili ifikie azma hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akisalimiana na Naibu Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Kjetil Schie alipokutana naye ofisini kwake jijini Dar es Salaam

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na Naibu Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Kjetil Schie alipokutana naye ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo tarehe 01 Agosti, 2024. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Taifa cha Ufuatilaji wa Kaboni (NCMC) Prof. Eliakim Zahabu.

Naibu Balozi wa Norway nchini Tanzania Kjetil Schie akifafanua jambo wakati wa kikao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa kikao kilichofanyika Ofisi ndogo jijini Dar es Salaam. Wengine ni Mkuu wa Masuala ya Kilimo, Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Bi. Guro Glavin na Mshauri Mwandamizi wa Masuqla Kilimo, Hali ya Hewa, Mazingira na Elimu ya Juu kutoka Ubalozi wa Norway Dkt. Yassin Mkwizu.

Related Posts