SIKU moja kabla ya kufanyika kwa Kilele cha Wiki ya Mwananchi, nyota wawili wapya wa timu hiyo, beki Chadrack Boka na straika Jean Baleke wameshusha presha ya mabosi na mashabiki baada ya sasa kuwa na uhakika wa kutumika ndani ya kikosi hicho cha Jangwani.
Awali ilikuwa ikielezwa huenda Yanga isingewatumia wachezaji hao katika mechi za awali za msimu mpya wa Ligi Kuu kutokana na kuchelewa kwa hati zao za uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka klabu walizokuwa wakizitumikia, lakini tishio hilo ni kama limeondoka na sasa Wanayanga wamejiandae tu kupata raha.
Nyota hao kutoka DR Congo, wamesajiliwa hivi karibuni, Boka akitokea FC Lupopo na Baleke akitokewa Al Ittihad alikokuwa akicheza kwa mkopo akiwa ni mchezaji wa TP Mazembe wote huenda wakakosa mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O ya Burundi zitakazocheza jijini Dar es Salaam.
Ishu ya Baleke, ni kwamba klabu ya Al -Ittihad ya Libya imeweka mgomo kuachia ITC, baada ya mshambuliaji huyo na Mazembe kusitisha mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja.
Al Ittihad ilikuwa bado inamhitaji Baleke, lakini mshambuliaji huyo hakuwa na furaha na maisha nchini humo na kuamua kusitisha mkataba huo akuiiomba Mazembe imalizane na Yanga ambayo imeshalipa kila kitu na kumruhusu nyota huyo wa zamani wa Simba kutua nchini na kubaki kumalizana na Walibya waiachie ITC hiyo.
Hata hivyo, hata kama ITC hiyo itawasili leo bado itamlazimu Baleke kukosa mechi mbili za hatua ya awali za nyumbani na ugenini dhidi ya Vital’O ya Burundi, kwa kuwa muda wa kuthibitisha usajili wake CAF umepita, lakini endapo Yanga itafuzu basi atacheza mechi zinazofuata za raundi ya pili.
Kwa Boka, inaelezwa ITC yake imekwishaingia tangu jana kutoka FC Lupopo na tayari imeshatumwa Yanga, baada ya katibu wa Lupopo kuwasili Kinshasa juzi na kukamilisha mchakato huo.
Taarifa za ndani zinasema, licha ya ITC ya Boka kufika jana, lakini bado hatoweza kucheza mechi hizo kwani kibali chake kilishachelewa.
“Kama Yanga itafanikiwa kufuzu hatua hiyo basi itaungana na wachezaji hao katika mchezo unaofuata hivyo watakosa mechi mbili tu za mwanzo ambazo zote zitachezwa hapa nchini,” kilisema chanzo hicho kutoka ndani ya Yanga.
Kukosekana kwa Boka kumempa nafasi mzawa Nickson Kibabage, ambaye ndiye chaguo la kocha kwa sasa, kwani amekuwa akimpanga katika mechi nyingi tangu msimu uliopita kabla ya ujio wa mrithi wa Joyce Lomalisa.
Kwa upande wa Baleke licha ya kufunga bao pekee katika mechi dhidi ya Ausburg ya Ujerumani, lakini ni wazi kuwa katika eneo analochezea kocha ana machaguo mengi na yote ni majembe, akiwamo Prince Dube, Clemeny Mzize na Kennedy Musonda atakaoshirikiana na viungo washambuliaji wakiongoza na MVP wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua, Duke Abuya na Clatous Chama.
Yanga kesho itashuka kwa Mkapa kutambulisha majembe mapya ya msimu ujao mbele ya mashabiki zao wakiwa wamevalia uzi mpya wa kijani, nyeusi na njano, huku mechi hizo za kimataifa zikichezwa Agosti 17.