MASHABIKI wa Yanga mzuka umepanda wakati Kilele cha Mwananchi kitakapohitimishwa kesho Kwa Mkapa, jijini Dar es Salaam huku shoo nzima ikiachwa chini ya Harmonize a.k.a Konde Boy akishirikiana na Christian Bella pamoja na wakali wengine kulipamba tamasha hilo la sita tangu liasisiwe mwaka 2019.
Harmonize aliyeachia wimbo maalumu wa tamasha hilo, ataliamsha mapema pamoja na Mfalme wa Masauti, Christian Bella, Meja Kunte, Pado MC, BillNass, Chobis Twins, DJ Ally B na wengine kuanzia saa 4 asubuhi kisha kikosi kipya cha Yanga kuvaana na Mabingwa wa Kagame 2024, Red Arrows ya Zambia saa 2:00 usiku.
Katika tamasha la kwanza la mwaka 2019 halikunoga sana kwa sababu ya ugeni, lakini yaliyofuata yalikuwa balaa na hapa chini ni kudhibitisha Konde Boy hana jambo dogo.
Ukiwa ni mwaka wa pili wamaka 2020, Harmonize alilipamba tamasha hilo kwa kishindo kwani siku moja kabla ya shoo yenyewe wakati anakwenda kukagua mazingira ya Uwanja wa Mkapa alitumia usafiri wa helikopta, ili kuonyesha ukubwa wa jina lake na kuifanya iwe simulizi kwa wengine watakaokuja nyuma yake, kuhakikisha anafanya ubunifu mkubwa.
Katika tamasha hilo, Konde Boy aliacha historia inayosimuliwa hadi sasa, kwani alitumia kamba kuingia uwanjani, zoezi ambalo linafanywa na wanajeshi,kitendo kilichowagawa mashabiki wapo waliokuwa wanamshangilia na wengine kuingiwa na hofu, kutokana na umbali wa juu kwenda chini.
Wakati akishuka kwenye kambi iliyokuwa nyembamba alivalia nguo za kijeshi, mgongoni alibeba kibegi cha kijeshi na mkononi bendera ya Yanga, shoo yake ilibakia simulizi kwa mashabiki wake, wakilinganisha na alichofanya Diamond kwenye Simba Day aliyeingia na helikopta akiongoza na aliyekuwa msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara ambaye kwa sasa wote wapo Jangwani.
Baadhi ya wasanii wengine waliotumbuiza siku hiyo kabla ya Konde Boy ni Sir Juma Nature na Temba, Chege Chigunda, Billnass, G Nako na Young Killer.
Msimu wa tatu mabosi wa Yanga waliamua kumshusha Papa Ngwasuma, Koffi Olomide mmoja ya wanamuziki nguli barani Afrika ili kuwapa raha Wananchi.
Shoo hiyo ilivutia mno wanayanga walioujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa, japo waliikosa ile burudani walioitarajia kutoka kwa Mopao Mokonzi, kwani shoo ilikuwa ya kawaida sana, juapo wasanii wengine wa hapa nchini walifanikiwa kufikia mashimo kinomanoma.
Wasanii wengine walionogesha shoo ya msimu huo ambao pia ilitumika kumtambulisha Haji Manara aliyekuwa amehama mtaa kutoka Msimbazi hadi Jangwani ni pamoja na TMK Wanaume Family iliwajumisha kila KR Mullah, Chegge, Mhe Temba na Sir Juma Nature.
Pia kulikuwa na Nandy, Marioo, Chid Benz, Stamina, Mr Blue, Madee, Msaga Sumu, Mimi Mars na wengine mbali na burudani ya mechi kadhaa za utangulizi zilizowapa raha Wanayanga.
Tamasha hili la nne lilikuwa tamu likienda na hashtag ya Byuti Byuti na shoo ilipambwa sana na wasanii wa ndani na Chebz Queens, Mzee wa Bwax, TMK Wanaume Family, Sir Jay, Mr Blue. Mzee na wengine ambao hawakulaza damu mwanzo mwisho.
Licha ya kwamba mwishowe timu ililala mbele ya Vipers ya Uganda, lakini mashabiki walienjoi ile kitu inataka kutoka kwa wasanii hao wa muziki sambamba Dokii.
Msimu uliopita Yanga ilifanya shoo nyingine iliyopambwa na Sholo Mwamba, Dullah Makabila (Singeli), MC Kidochi, Chobis Twins, Mchina Mweusi na Dj Ally B, huku mtumbuizaji mkuu alikuwa Riger aliyefahamika zaidi na songo la Tabulele Laa.
Riger ni memba wa kundi la vijana zaidi ya 100 wanaounda kundi la KKL Bomoko lililokuwa likifanya bato ya freestyle ambaye alitua nchini na kushirikiana na Harmonize kufyatua Tabulele Remix na kuwasha tamashani.
Kwa msimu huu mashabiki wanasubiri kuona itakuwaje, ila Harmonize na Christian Bella wana kazi ya kusuuza roho za Wananchi Kwa Mkapa.