Dk Mwinyi: Mapinduzi ya kilimo kipaumbele Zanzibar

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali imedhamiria kwa dhati kuleta mageuzi ya kilimo, kukitoa kwenye mazoea na kukifanya kiwe cha biashara na chenye tija.

Amesema Mapinduzi ya kilimo Zanzibar ni jambo la msingi na kupewa kipaumbele kwani kwa muda mrefu sekta hiyo haijaweza kutoa matokeo halisi yanayotarajiwa.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Agosti 3, 2024 wakati akifungua maonyesho ya saba ya Nane Nane katika eneo la Kizimbani.

Amesema siku hiyo ina hadhi ya pekee kwani kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa kwa maana asilimia 40 ya wananchi wamejiajiri moja kwa moja katika sekta hiyo.

“Nipongeze kaulimbiu ya mwaka huu isemayo ‘Kilimo ni utajiri kila mtu atalima’ kwani lengo la Serikali ni kuleta mageuzi ya kilimo kiwe cha tija, kwa muda mrefu kilimo hakijatufikisha tunapotaka kufika,” amesema.

Amesema takwimu za mwaka 2023 sekta hiyo imechangia asilimia 24.3 ya pato la Taifa Zanzibar na kwamba, ikiwa itafanya vizuri zaidi katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, itaweza kuwa na mchango mkubwa zaidi.

Amesema sekta hiyo inaziunganisha sekta nyingi zikiwemo za biashara, viwanda, utalii na maji, hivyo itasababisha uchumi mzima kupanda.

Dk Mwinyi amesema amefurahishwa kusikia miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa ni kuimarisha kilimo cha mboga na matunda, akisema ni dalili njema zimeanza kuonekana kwa kuongezeka uzalishaji.

Katika kuthibitisha hilo, amesema takwimu zinaonyesha uzalishaji wa mbogamboga na matunda umeongezeka kutoka tani 66,310 mwaka 2022 na kufikia tani 87,971 mwaka 2023.

“Matokeo ya hatua hiyo yatasaidia kupunguza utegemezi mkubwa wa mazao ya matunda na mbonga kutoka nje ya Zanzibar,” amesema.

Dk Mwinyi amesema Serikali kupitia mpango wa mageuzi ya kilimo inatarajia kuanzisha vituo maalumu katika kila wilaya kurahisisha shughuli hizo.

Kwa upande wa mifugo, amesema Serikali inatarajia kutekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji maziwa kwa wafugaji wadogowadogo utakaozingatia mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, mradi huo una gharama ya Sh7.5 bilioni ukiwa ni mkopo wa bei nafuu kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (Ifad), ukilenga kuleta mageuzi katika mnyororo wa thamani.

Mradi huo utakuza ari za maisha za wananchi na kuimarisha uhakika wa chakula na lishe.

Amewataka vijana kutumia fursa hiyo kujiajiri na kujifunza mbinu bora za kilimo na kufuga, kwani Serikali ipo tayari kuwasaidia kuleta mageuzi.

Dk Mwinyi ameitaka wizara ya kilimo kuendelea kuwa karibu na wadau wa kilimo na wafugaji kwa kusimamia sera na mikakati inayopangwa.

Amewataka wakuu wa mikoa, wilaya na wadau wengine wa kilimo kushirikiana, akisema mipango ya kilimo inahitaji ushiriki wa kila mdau na si Serikali pekee.

Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Ali Khamis Juma amesema miundombinu katika maonyesho hayo imeboreshwa ikiwa ni pamoja na ujenzi barabara za lami.

“Uliahidi kujenga barabara za lami, zimejengwa kilomita 3.2 ambayo imegharimu Sh2.1 bilioni na kujenga tangi la maji lenye ujazo wa lita milioni 1.5 kwa gharama ya Sh200 milioni,” amesema

Amesema maonyesho hayo yalikadiriwa kutumia Sh712 milioni, mpaka sasa wameshapata Sh445 milioni kutoka serikalini na wadau wa biashara, huku washiriki wakiwa 315 kutoka taasisi tofauti na wajasiriamali ikilinganishwa na washiriki 275 wa mwaka jana.

“Hii inadhihirisha mwitikio mkubwa wa kutumia fursa kupitia eneo hili la maonyesho. Kwa mwitikio huo tumeongeza ukubwa wa eneo la kilimo kutoka hekta tisa hadi 10.5,” amesema.

Katika siku hizo za maonyesho ambayo kwa mwaka huu yatakuwa ya siku 14, zitatolewa tafiti 11 zilizofanywa na wizara kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo uzalishaji bora wa chakula na utafiti wa uzalishaji wa nyama ya ng’ombe wenye kilo nyingi.

Tafiti zingine zitakazotolewa ni udhibiti wa wadudu kwa kutumia dawa asili na utafiti wa maradhi ya wanyama hatarishi kama mbwa.

Waziri wa wizara hiyo, Shamata Shaame Khamis amesema kutokana na maboresha yanayoendelea kufanyika, idadi ya wakulima waliokuwa wakienda kuonyesha mazao Tanzania Bara imepungua.

“Haya maonyesho yatakwenda mwaka mzima, baada ya siku 14 tutaondoa mahema tu lakini wanaotaka kujifunza shughuli hizi eneo litakuwa wazi na wale waliopewa maeneo watakuwa hapa,” amesema.

Related Posts