Arusha. Mahakama ya Rufani imetengua hukumu ya kifungo cha maisha jela aliyokumiwa mkazi wa Ilala, Dar es Salaam, Matiku Thomas baada ya kutiwa hatiani kwa ulawiti.
Hukumu imetolewa ikielezwa Mahakama ilikosea kumtia hatiani ilipobaini utofauti wa ushahidi na hati ya mashtaka aliyoshtakiwa mahakama ya awali.
Matiku alidaiwa kumlawiti mtoto wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 12 hadi 13 kwa nyakati nne tofauti.
Jopo la majaji watatu walioketi jijini Dar es Salaam kusikiliza rufaa hiyo namba 638/2022 ni Rehema Mkuye, Zephrine Galeba na Abraham Mwampashi.
Kupitia uamuzi walioutoa Julai 31, 2024 uliowekwa kwenye mtandao wa Mahakama Kuu Tanzania wa TanzLII, majaji hao baada ya kupita mwenendo wa shauri hilo wamebaini dosari hiyo ya kisheria.
Jaji Mkuye alieleza kwa kuzingatia waliyojadili wanaruhusu rufaa na kutengua hukumu ya kifungo cha maisha baada ya kukubaliana na hoja ya kwanza kuwa kulikuwa na utofauti kati ya hati ya mashtaka na ushahidi, ikiwemo tarehe tukio hilo linalodaiwa kutokea kushindwa kuthibitishwa wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi.
Rufaa hiyo inatokana na hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ya Septemba 28, 2022 katika rufaa ya kwanza.
Awali mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Matiku alishtakiwa kwa kutenda kosa kinyume cha kifungu cha 154 (1) (a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu.
Alidaiwa Julai 29, 2016 katika eneo la Banana, wilayani Ilala jijini Dar es Salaam alimlawiti mtoto huyo na alipotiwa hatiani alihukumiwa kifungo cha maisha jela.
Upande wa mashtaka ulidai mtoto huyo mara kwa mara alikuwa akirudi nyumbani kwa kuchelewa ambako bibi yake aliyekuwa akiishi naye hakuridhishwa na hali hiyo ndipo akafuatilia shuleni ikabainika alikuwa mtoro.
Baada ya uchunguzi alieleza alikuwa akienda kwa Matiku mara kwa mara ambaye alimwingilia.
Matiku alikata rufaa Mahakama Kuu akakwaa kisiki.
Katika Mahakama ya Rufaa, Matiku alikuwa na hoja mbili akidai mahakama hiyo ilikosea kisheria na ukweli kushikilia hukumu dhidi yake bila kuzingatia tofauti za ushahidi na hati ya mashtaka.
Sababu ya pili alidai mahakama ya kwanza ya rufaa ilikosea kisheria kuona kwamba kesi dhidi yake ilithibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Matiku aliwakilishwa na wakili Josephat Mabula, wakati mjibu rufaa akiwakilishwa na mawakili wa Serikai Eric Shija na Nicas Kihemba.
Alidai katika hati ya mashtaka ilidaiwa Matiku alitenda kosa hilo Julai 29, 2016 ila hakuna shahidi hata mmoja wa upande wa mashtaka aliyethibitisha kuwa kosa hilo lilitendwa siki hiyo.
Alidai shahidi wa kwanza wa mashtaka alidai kushuhudia kwamba siku moja akiwa amelala kwenye duka la Matiku pia alilala hapo na kisha kumlawiti jambo ambalo liliashiria kuwa ni siku moja tu na tarehe isiyojulikana na kuwa kuhusu madai ya kosa hilo kutendwa mara kadhaa ilipaswa kuthibitishwa mahakamani.
Kuhusu hoja ya pili, alidai katika makosa ya kujamiiana mwathiriwa ndiye shahidi bora na mahakamaa inapaswa kuzingatia ushahidi kutoka kwa mashahidi wengine wanaothibitisha na kuwa mashtaka walishindwa kumpigia simu mwalimu wa darasa ambaye alimfahamisha bibi kuwa mwathiriwa alikuwa mtoro. Aliiomba mahakama kuruhusu rufaa hiyo.
Wakili Erick alitupilia mbali hoja ya wakili Mabula kuwa kulikuwa na tofauti kati ya hati ya mashtaka na ushahidi kwa kuzingatia ukweli kwamba, wakati shtaka liliposomwa kwa Matiku, alikana kosa hilo, kwa hiyo alielewa asili ya kosa dhidi yake.
Alisema ingawa shtaka hilo lilikuwa na lengo la kumjulisha mrufani asili ya kosa, tarehe, mahali ila kushindwa kwa mwathirika kutaja tarehe katika ushahidi wake si mbaya kwani inatibika kwa mujibu wa kifungu cha 388 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Alieleza ingawa shahidi wa kwanza alidai alilawitiwa mara nne, kushindwa kueleza ukweli huo hakumaanishi kwamba hakumtambua Matiku na kwamba tatu, kosa hilo lilithibitishwa bila shaka kuwa shahidi wa kwanza ililawitiwa kulingana na ushahidi wake ambao ulithibitishwa na shahidi wa nne.
Alidai hakukuwa na haja ya kuwaita mwalimu wa darasa na mwanamke anayeuza mikate ili kutoa ushahidi kwani hawakushuhudia wakati kosa hilo lilipofanyika na kushikilia kuwa mahakama ya awali ya rufaa iliidhinisha ipasavyo hukumu hiyo na hukumu iliyotolewa dhidi ya mrufani.
Baada ya kupitia hoja hizo, majaji walieleza kwa kuzingatia misingi ya rufaa, rekodi ya rufaa na mawasilisho ya pande zote mbili, wanapendekeza kushughulikia msingi wa kwanza wa kukata rufaa unaotegemea suala la kama kulikuwa na tofauti kati ya shtaka na ushahidi na kuwa unaweza kuondoa rufaa bila kujadili sababu iliyobaki.
Jaji Mkuye alieleza vifungu vya 132 na 135 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai vinataka shtaka liwe na taarifa ya kosa au makosa ambayo mtuhumiwa anashtakiwa nayo, na maelezo kama itakavyohitajika ili kutoa taarifa kuhusu asili ya kosa aliloshtakiwa.
Alieleza wanadhani ni muhimu pia kuonyesha katika maelezo ya kosa, wakati au tarehe wakati mtuhumiwa alitenda kosa kwani lingemuwezesha mtuhumiwa kuelewa asili ya kosa na kuandaa utetezi unaoeleweka.
Jaji Mkuye alieleza kupitia kumbukumbu za rufaa hiyo, kupitia hati ya mashtaka inaonyesha miongoni mwa vipengele vya kosa lililoshtakiwa, tarehe ambayo kosa hilo lilidaiwa kutendwa, imeonyeshwa kuwa ni Julai 29, 2016 na ilipaswa kuthibitishwa.
Alieleza hakukuwa na shahidi yeyote (pamoja na mwathiriwa) ambaye alitoa ushahidi wa ni lini kosa hilo lilitendwa na wanadhani, madhumuni ya kutaja tarehe ambayo kosa lilitendeka katika maelezo ya kosa ni kama ilivyowasilishwa na Wakili wa Serikali, ili kumwezesha mshtakiwa kuelewa ni lini hasa kosa linalodaiwa lilitendeka ili kumuwezesha kuandaa utetezi wake.
“Lakini shahidi wa kwanza ambaye ni mwathirika wa tukio hilo alishindwa kutaja tarehe ambayo kosa hilo lilitendeka, katika hatua fulani kama inavyoonyeshwa kwenye ukurasa wa 17 wa rekodi ya rufaa, alisema kwamba mrufani alimbaka dukani kwake mara nne, mambo haya yote yanaonyesha kuwa kuna tofauti ya wazi juu ya tarehe kati ya hati ya mashtaka na ushahidi.
“Kwa busara, katika hali ambapo kuna tofauti ilikuwa ni lazima kwa upande wa mashtaka kurekebisha shtaka ili kutafakari kwamba kosa kama hilo lingeweza kutendeka kwa tarehe tofauti zaidi kwa sababu, mwathirika hakuwa na uhakika juu ya tarehe ambayo kosa lilitendeka bali pia kutokana na ukweli kwamba alisema kwamba alifanyiwa hivyo mara nne,” alisema.
Alisema ushahidi wa bibi wa mwathirika huyo kwamba mwathiriwa alikuwa akichelewa kutoka shule akisema alikuwa akiitwa na Matiku dukani kwake ilihalalisha mwendesha mashtaka kurekebisha shtaka hilo.
Jaji alisema ingawa shtaka hilo linaonyeshwa kufanyika Julai 29, 2016 mwathirika hakusema chochote kuhusu tarehe hiyo kisha akadai alifanyiwa mara moja ila aliporudia tena akaeleza amefanyiwa mara nne, hivyo inaonyesha kwamba shtaka halikuthibitishwa kutokana na tofauti ya wazi kati ya shtaka na ushahidi uliotolewa na shahidi huyo.
Alisema kwa kuangalia ushahidi wa shahidi wa pili na tatu ili kujua kama utasaidia katika kuokoa kesi kuhusu tarehe ambayo kosa linalodaiwa lilitendeka, lakini wamegundua kuwa, haiwezi hivyo upande wa mashtaka haukuthibitisha shitaka hilo na kwa kuongozwa na kesi ya Abel Masikiti (supra), hali hiyo mbaya ilifanya mrufani aachiwe huru na kukubali hoja hiyo.
“Kwa kuzingatia hitimisho la msingi wa kwanza wa kukata rufaa, msingi wa pili kwamba kesi haikuthibitishwa bila shaka yoyote inafanikiwa moja kwa moja, na tunaruhusu,” alisema.