Hatua kwa hatua uchaguzi wa TLS

Dodoma. Safari ya kupatikana mshindi wa urais katika uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),  ilianza saa 12.30 asubuhi ya Agosti 2, 2024, pale wanachama walipoanza kupiga kura kuchagua viongozi watakaoongoza chama hicho kwa miaka mitatu.

Mchuano mkali katika uchaguzi huo ulikuwa kati ya wagombea wawili kati ya sita wa nafasi ya urais ambao ni Boniface Mwabukusi na Sweetbert Nkuba.

Wagombea wengine katika nafasi hiyo walikuwa ni Ibrahim Bendera, Paul Kaunda, Emmanuel Muga na Revocatus Kuuli.

Kuliwekwa vituo zaidi ya vitano katika mahema kwenye viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma kwa ajili ya kupigia kura.

Wagombea waliweka mawakala kusimamia upigaji kura, huku eneo hilo likilindwa na askari polisi kwa muda wote hadi kutangazwa matokeo.

Wakati uchaguzi ukiendelea, ilipofika saa 5.00 asubuhi karatasi za kupigia kura ziliisha,  jambo lililosababisha upigaji kura uliokuwa uhitimishwe saa 6.00 mchana, kuongezewa  kwa muda wa saa moja.

Wapiga kura walilazimika kusubiri kwenye viwanja hivyo, hivyo kukawa na makundi ya wajumbe walioendelea na mazungumzo.

Baada ya zaidi ya saa mbili karatasi zililetwa na kuhakikiwa na mawakala, hivyo upigaji kura uliendelea hadi saa 9.00 mchana ulipokamilika.

Kazi ya kuhesabu kura iliendelea wajumbe wakisubiri hadi saa 10.00 jioni walipoingia ukumbini kuendelea na ajenda nyingine zilizopangwa kwa siku hiyo ya Agosti 2, 2024.

Wamuaga mwenzao aliyefariki

Hata hivyo, wakati wajumbe wakiendelea na uchaguzi, walitangaziwa kwamba mmoja wa wanachama wa TLS, Maria Pengo (36) aliyefika jijini Dodoma kwa ajili ya kushiriki mkutano huo  alifariki dunia.

Maria alifariki dunia saa 7.00 usiku wa kuamkia Agosti 2, baada ya kuugua ghafla na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Wanachama walitangaziwa wanaotaka kutoa rambirambi kuweka kwenye moja ya boksi lililowekwa ndani ya ukumbi au kupitia namba maalumu kwa wale ambao wanataka kutoa kidijitali.

Saa 11.00 jioni, rais wa TLS aliyemaliza muda wake, Harold Sungusia alisimamisha mkutano kuruhusu kuagwa mwili wa Maria, kabla ya kumsafirisha kwenda nyumbani kwake Dar es Salaam.

Baada ya kumuaga wanachama waliendelea na mkutano hadi saa 3.00 usiku. Kwa nyakati tofauti Sungusia alikuwa akiwatangazia wajumbe kuwa kamati ya uchaguzi haijakamilisha shughuli ya kuhesabu kura hivyo wanaendelea na ajenda zilizobakia.

Wakati kikao kikiendelea tayari katika kurasa na mitandao ya jamii,  baadhi ya watu walikuwa wakitangaza kuwa Mwabukusi ameshinda katika uchaguzi huo,wengine wakitangaza kushindwa kwa mgombea huyo.

Hata hivyo, baada ya kumalizika kwa ajenda za mkutano zilizopangwa kwa siku hiyo, alisimama mmoja wa wajumbe akitaka Sungusia atoe mwongozo kwa kamati ya uchaguzi itangaze matokeo, hatua iliyofanya kiongozi huo kuondoka kwenye meza kuu kupisha kamati hiyo.

Baada ya kupisha kwenye meza hiyo, baadhi ya wajumbe walisimama na kuanza kuimba nyimbo kadhaa, wengine wakisikika wakiimba wana imani na Mwabukusi.

Saa 5.00 usiku kamati ilijitokeza kutangaza matokeo.

Jaji mstaafu Joaquine De Mello, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi alimtangaza Mwabukusi kuwa mshindi baada ya kujipatia kura 1,274 kati ya kura 2,218 zilizopigwa katika uchaguzi huo. Nkuba akipata kura 807.

Wagombea wengine katika uchaguzi huo na kura zao kwenye mabano ni Ibrahim Bendera (58), Paul Kaunda (51), Emmanuel Muga (18) na Revocatus Kuuli (7).

Baada ya kutangazwa matokeo hayo, Mwabukusi aliwashukuru Watanzania ambao wengine waliwapigia simu watoto wao ambao ni wanachama wa TLS kuwataka wampigie kura katika uchaguzi huo.

“Tunashukuru watu waliosafiri kutoka maeneo mbalimbali kuja hapa kuhakikisha wanahamasisha, watu wananipigia kura,” amesema.

Amesema chama hicho hakina rais mtendaji bali wamekuwa wakifanya kazi kwa mashauriano, lakini vipaumbele vyake ni kuirudisha TLS kufanya kazi yake ya kuwasemea Watanzania, kuishauri Serikali, kulinda wanachama wake na kuhakikisha utawala wa sheria Tanzania unafuatwa.

“Ninachowaahidi Watanzania kuwa TLS inarudi katika misimamo yake, misingi yake, inarudi kwenye dira yake, mimi pamoja na GC (baraza la uongozi) yangu tutawatumikia kwa unyenyekevu,” amesema.

Kamati ya uchaguzi yaeleza

Kuhusu sababu za kuchelewa kwa matokeo, Jaji De Mello amesema hali hiyo ilitokana na idadi ya watu kuwa kubwa ambayo haijawahi kutokea katika historia ya TLS.

Amesema suala hilo liliwalazimu kufanya uhakiki ili kuwa na uhakika wa kile walichokifanya.

Kwa upande wa upungufu wa karatasi zilizolazimu kuahirishwa kwa uchaguzi, amesema kulijitokeza changamoto kwenye uhakiki wa orodha ya wapiga kura.

Amesema walitoa orodha mara ya kwanza ili wapigakura wahakiki kama majina yao yapo au hapana lakini hawakupata mrejesho.

“Tulitoa ya pili wachache wakajitokeza tukairekebisha, tukatoa ya tatu juzi (Julai 31, 2024) wakati tunafanya chaguzi za kanda kuna baadhi ya watu walisema majina yao hayapo tena.

“Tukaona kuwa ni upungufu upande wao (wapigakura) kwa sababu tuliwapa nafasi mara tatu ya kupitia na kuhakiki. Lakini tukatumia busara tukaongeza nyingine jana usiku tulituma nyingine hatukupata idadi tukaenda na ile final (ya mwisho),” amesema.

Amesema baadaye walibaini karatasi za kupigia kura zinakwisha, hivyo ikawalazimu kuongeza ambapo juzi (Agosti Mosi) waliongeza karatasi 400 lakini (Agosti 2) waliongeza nyingine 200.

Mgombea aliyeshika nafais ya pili, Nkuba amesema hakubaliani na matokeo yaliyotolewa na kamati ya uchaguzi wa chama hicho, hivyo atakwenda mahakamani kuyapinga.

Related Posts