Dar es Salaam. Kufuata ushindi alioupata, Rais mpya wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amesema atakirudisha chama hicho kwenye misingi yake.
Katika uchaguzi huo uliofanyika jijini Dodoma Agosti 2, 2024 Mwabukusi aliibuka mshindi kwa kupata kura 1,274 kati ya 2,218 zilizopigwa akifuatiwa na Sweetbert Nkuba aliyepata kura 807.
Wagombea wengine katika uchaguzi huo na kura zao kwenye mabano ni Ibrahim Bendera (58), Paul Kaunda (51), Emmanuel Muga (18) na Revocatus Kuuli (7).
Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 3, 2024, Mwabukusi amesema katika uongozi wake, atajikita kwenye kifungu cha 4 cha Sheria ya TLS kukirudisha chama hicho kwenye misingi yake.
“Kama nilivyosema, mimi naanza na kifungu cha 4 cha Sheria ya TLS kuirudisha TLS kwenye misingi yake ili kuhakikisha chama kinatekeleza wajibu wake,” amesema
Kifungu hicho, kinaeleza malengo ya chama hicho ambayo ni kuwaunganisha, kuwatetea na kusaidia ustawi wa mawakili nchini. Pili, ni kuishauri Serikali na vyombo vyake kama Bunge na Mahakama. Jukumu jingine ni kusimamia maslahi na ustawi wa jamii ya Watanzania.
Alipoulizwa jinsi atakavyoshirikiana na viongozi wa Serikali, huku akitajwa kuwa na tabia ya ukali, Mwabukusi amesema licha ya kuwa na tabia hiyo atazingatia sheria.
“Watu wanavyosema nina confrontation (jazba) ni kama ninafanya mambo kwa hisia zangu. Hii ni taasisi na mimi huwa naongozwa na kanuni, sheria na Katiba, hayo ndio maisha yangu siku zote.
“Pia siku zote huwa nimezoea kulitamka jambo kama lilivyo, kama ni zuri nitalitamka jinsi lilivyo na kama ni baya nitalitamka hivyo hivyo, kwa hiyo sio kupinga kama watu wanavyosema,” amesema.
Amesema katika mapambano yake amekuwa akitumia mahakama kudai haki zake.
Ametoa mfano wake alipogombea ubunge katika jimbo la Busokelo mwaka 2020 akidai kuwa alidhulumiwa katika uchaguzi huo.
“Nilikuwa na kundi kubwa la watu na ningeweza kuwaambia wafanye lolote, lakini niliondoka nikaenda mahakamani, nilikuwa Mtanzania pekee aliyegombea na aliyekwenda mahakamani.
“Utaona hata katika uchaguzi huu nimefanyiwa mizengwe mingi lakini mara zote nimekuwa radical (mkali) na nimekwenda mahakamani.
“Kudai haki yako sio utovu wa nidhamu lazima watu waelewe. Wakati nakukemea sio confrontation, hata nikikupongeza sijakuogopa.
“Wakati wa kupongeza nakupongeza, wakati wa kukemea nakemea, wakati wa kubomoa nabomoa, wakati wa kuvunja navunja na wakati wa kujenga najenga, nazungumza lugha inayotokana na tukio husika,” amesema.
Licha ya kufuata sheria, Mwabukusi amesema ataendeleza misimamo yake bila kuogopa vyeo vya watu.
“Mimi mjinga namkemea sitakuogopa hata kama una cheo, lakini ikija kwenye courtesy (heshima) tutafanya. Nchi haiendeshwi kihuni, inaendeshwa kwa sheria na Katiba na kanuni,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi Julai 26, 2024 mara baada ya kupata ushindi katika kesi aliyopinga kuenguliwa kugombea TLS, Mwabukusi alisema mbali na kusimamia kifungu cha 4 cha Sheria ya TLS, pia anataka kusimamia mpango mkakati wa chama hicho wa mwaka 2021 hadi 2025 na kuifanya TLS kuwajibika na kufuata malengo yake kwa wanachama na kuitumikia jamii.
Akieleza jinsi atakavyoitumikia jamii, Mwabukusi amesema katika utumishi wake wa miaka 14 kama wakili, amekuwa akiitumikia jamii kwa kuwatetea wananchi katika changamoto mbalimbali.
“Watu wanafikiri nimefungua kesi tu ya mkataba wa bandari, katika utumishi wangu wa miaka 14 nimefungua kesi nyingi za watu wanaoporwa mali zao, migogoro ya ardhi na utetezi wa haki za watu mbalimbali.
“TLS ni lazima iendane na mahitaji ya wananchi, kwa mfano katika masuala ya Katiba kuwa na utawala bora, haki za binadamu na kuwa na sheria bora zitakazolinda haki za watu,” amesema.
Amesema katika uongozi wake atahakikisha anasimamia masilahi ya wananchi na malalamiko yaliyokosa majibu.
“Tunaona watu wanatekwa na wengine wanapotea, watu wananyimwa haki zao, hayo yote tutashughulikia,” amesema.
Kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba, amesema ni moja ya ajenda zake kuhaikisha inapatikana.
“TLS ina wajibu wa kuhakikisha Katiba inapatikana na tunasimamia sheria. Tutasimama na wananchi katika majukumu yetu yote,” amesema.