MENEJIMENTI ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, umejiongeza ili kuwarahisisha kazi mashabiki wa Simba waliojitokeza kushangweka na Tamasha la Simba Day, baada ya kuongeza mageti zaidi ya kuingilia uwanjani baada ya kuibuka malalamiko ya mashabiki walioidai wamekaa muda mrefu katika foleni ya kuingia ndani.
Awali mashabiki waliokata tiketi kwa ajili ya kuingia uwanjani kushuhudia Tamasha la Simba Day walikuwa wakitumia mageti manne ya kuingilia uwanjani, lakini walipata wakati mgumu kwa kuchukua muda mrefu wakiwa wamepanga foleni wakifanyiwa ukaguzi kabla ya kuingia.
Kutokana na hali hiyo, wasimamizi wa uwanja huo wakalazimika kufungua geti lingine na kuwa matano ili kupunguza msongamano uliokuwepo kwani hadi kufikia saa 7:20 mchana kulikuwa na watu wengi nje wakipambana kuingia.
Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Milinde Mahona amesema: “Mageti manne yalianza kufanya kazi, ni kweli eneo letu dogo kwa maana ya kukiwa na mistari mirefu inakuwa changamoto, lakini watu wanaendelea kuingia kwa utaratibu maalum.
“Tumesikia kilio cha mashabiki wakidai wamepanga foleni muda mrefu kupambana kuingia, wanapaswa kuvumilia kwani lazima tufanye ukaguzi. Hata hivyo, tumegundua kwamba watu wamekuja kwa wingi wakati mmoja hivyo tumeongeza geti lingine,” amesema Mahona na kuongeza;
“Tunaendelea kuongeza mageti kadri muda unavyokwenda lengo ni kutatua changamoto kulingana na mazingira yanavyojitokeza.”
Leo ni kilele cha Tamasha la Simba Day ambalo ni msimu wa 16 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009 ambapo Simba itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya APR ya Rwanda, kabla ya hapo itatambulisha kikosi chake cha msimu wa 2024-2025.