Manula apewa ‘Thank You’ | Mwanaspoti

ALIYEKUWA kipa namba moja wa Simba, Ashi Manula ametemwa kwenye kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao wa 2024/25 baada ya timu hiyo kutambulisha makipa wanne huku jina lake likiondolewa.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally ndiye alikuwa anataja majina ya mastaa wa kikosi hicho msimu ujao katika tamasha la Simba Day linalofanyika Uwanja wa Mkapa, ambapo ametaja majina manne eneo la makipa.

Makipa hao ni Ally Salim, Ayoub Lakred, Mohammed Camara na Hussein Abel ndiyo idadi ya walinda lango  watakaoiongoza Simba eneo la golini.

Wakati wa kutaja majina hayo nyomi ya mashabiki iliyojaza uwanja iliibua shangwe baada ya kusikia jina la Lakred ambaye inaelezwa kuwa atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi sita kutokana na kuumia akiwa mazoezini.

Pia shangwe kubwa limeibuka baada ya kutajwa kwa kipa mpya wa timu hiyo ambaye amesajiliwa kwa lengo la kuziba pengo la Lakred ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa muda akiuguza jeraha alilolipata.

“Hawa ndio walinda mlango ambao tutakuwa nao msimu ujao,” amesema Ahmed.

Related Posts