MASTAA wa zamani wa Yanga Princess, viungo Precious Christopher na Saiki Atinuke ni miongoni mwa wachezaji waliocheza kwenye mechi ya kirafiki kati ya Simba Queens na Mlandizi Queens.
Mchezo huo umepigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 9 alasiri kwenye kilele cha kuadhimisha Simba Day.
Wachezaji hao wawili wamesajiliwa na Simba katika dirisha hili la usajili baada ya kupewa mkono wa kwaheri na Yanga.
Kwenye kikosi kilichocheza mchezo huo viungo hao walianza na Precious akifunga bao la pili. Baada ya kufunga bao hilo mashabiki wa Simba walinyanyuka na kumshangilia.
Ukiachana na viungo hao, wawili raia wa Nigeria, timu hiyo pia imemsajili beki wa kulia kutoka Yanga, Wincate Kaari, raia wa Kenya ambaye hakuanza kwenye mchezo huo.
Precious, Saiki na Wincate wakiwa Yanga walikuwa wachezaji tegemeo kwenye timu hiyo iliyomaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu uliopita.