Msako wa viuatilifu feki waja

Mbeya. Mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu nchini (TPHPA), inatarajia kufanya operesheni na msako wa kushtukiza nyumba kwa nyumba,  kubaini viwanda bubu na mashine zinazozalisha viuatilifu visivyo na ubora.

Hatua hiyo inalenga kumlinda mkulima kuzalisha kwa tija, kuweka biashara shindani na kumlinda mlaji kupata chakula chenye ubora na  kulinda afya yake kuepuka magonjwa yakiwamo saratani, ngozi na kifua.

Akizungumza leo Agosti 3 katika maonesho ya wakulima ‘Nene Nane’  Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika jijini hapa, Ofisa ukaguzi ubora wa mamlaka hiyo, Nuru Senu amesema operesheni hiyo tayari imeanza na lengo ni kuhakikisha wakulima wanafanya shughuli zao kwa tija.

Amesema TPHPA inaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wananchi kwa ujumla namna ya kutambua viuatilifu visivyo na ubora pamoja na kutambua aina ya magonjwa sumbufu shambani na namna ya kukabiliana nayo.

“Zipo tetesi tumezipata baadhi ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini za uwapo wa viwanda bubu na mashine zisizo na ubora kuzalisha viuatilifu, mamlaka inafuatilia zaidi na itachukua hatua kali kwa mujibu wa sheria” amesema Nuru.

Kwa upande wake,  Kaimu Meneja wa mamlaka hiyo Nyanda za Juu Kusini, Pius Kawala amesema katika kumlinda mkulima na mtumiaji, TPHP imetoa masharti kwa waingizaji wa viuatilifu kujisajili na kupewa vibali na kwamba wameimarisha doria maeneo ya mipakani kudhibiti uingizwaji bidhaa feki.

Amesema kwa sasa wanatumia mipaka yote kubaini mzigo unaoingizwa na kujiridhisha ubora wake kabla ya kufikishwa nchini na wanapobaini upungufu wowote, bidhaa huchomwa moto na muda mwingine mhusika huchukuliwa hatua.

“Adhabu kwa wanaoingiza bidhaa feki kupitia njia za panya kwanza tunaziteketeza, lakini mhusika analipa faini hadi Sh100 milioni au kwenda jela, ndio maana tunahimiza kujisajili na kupewa kibali na cheti” amesema na kuongeza:

“Tunataka kuona kilimo cha biashara shindani na kumlinda mtumiaji wa chakula hicho anakuwa na afya, tumeweka programu maalumu kwa wakulima kufanya tafiti za magonjwa na wadudu na matumizi ya dawa.’’

Mmoja wa wakulima wa mpunga wilayani Kyela, Jonathan George amesema mabadiliko ya tabianchi, wadudu na magonjwa mengine, yamekuwa kikwazo katika kilimo, akiomba wataalamu kutoa elimu namna ya kupambana nayo.

“Itolewe elimu za mara kwa mara namna ya kukabiliana na magonjwa na wadudu, kuna kipindi nyuma tulivamiwa na wadudu fulani mashambani na kuharibu mazao yetu, lakini hata viuatilifu navyo kuna ambavyo havina ubora” amesema George.

Related Posts