Ndege za kivita za Urusi ni lazima ziharibiwe – DW – 03.08.2024

Kiongozi huyo wa taifa lililo vitani, amesema mabomu hayo yalifyetuliwa kwa ndege za kivita na kuelezea haja ya Ukraine kuzikabili ndege za Urusi kama njia ya kulemaza uwezo wa Moscow kwenye uwanja wa vita.

“Ndege za kivita za Urusi ni lazima ziharibiwe popote zilipo na kwa njia yoyote inayofaa.” amesema Zelensky katika ujumbe aliouchapisha kupitia mitandao yake ya kijamii.

Taarifa hiyo ya Zelensky imetolewa wakati utawala mjini Kyiv umesema mapema leo Jumamosi kwamba droni zake zimeulenga uwanja wa ndege na bohari moja ya mafuta ndani ya Urusi.

Chanzo kimoja cha ndani ya serikali kimenukuliwa na Shirika la Habari la AFP kikisema “usiku wa kuamkia leo, droni za Ukraine ziliufikia uwanja wa ndege wa Morozovsk uliopo kwenye mkoa wa Rostov.”

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine.
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine. Picha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

Inaarifiwa uwanja huo ndiyo unahifadhi ndege za kivita za Urusi na mabomu yanayofyetuliwa kutokea angani. Chanzo hicho kimeongeza kusema kwamba “droni za Ukraine zilifanya kazi nzuri, kwa kulilenga ghala la silaha za anga.”

Maelezo hayo ya Ukraine yametolewa baada ya Urusi kusema ilizima shambulizi kubwa la anga usiku wa kuamkia leo. Maafisa wa Urusi hawakuzungumzia lolote kuhusu madai ya kulengwa na kuharibiwa kwa uwanja wa ndege.

Hata hivyo gavana wa mkoa wa Rostov Vasily Gobulev aliandika kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba mamlaka za wilaya ya Morozovsk zimetangaza hali ya dharura.

“Hivi sasa tumerikodi uharibifu wa madirisha kwenye majengo kadhaa ikiwemo shule, nyumba kadhaa na eneo la viwanda,” ameandika Golubev.

Ukraine yadai kuishambulia bohari ya mafuta ndani ya ardhi ya Urusi 

Droni ya Ukraine
Droni ya Ukraine. Picha: Inna Varenytsia/REUTERS

Katika shambulizi jingine, chanzo kimoja ndani ya Ukraine kimesema vikosi vya nchi hiyo vimeilenga bohari ya mafuta kwenye wilaya ya Kamensky iliyopo pia kwenye mkoa wa Rostov.

Mapema maafisa wa Urusi kwenye mkoa huo waliarifu kutokea hujuma iliyofanywa na droni ambayo imesababisha moto kwenye matangi ya mafuta.

Utawala mjini Moscow haujasema kuhusu mkasa huo lakini wizara yake ya ulinzi imesema imedungua karibu droni 76 zilizorushwa na Ukraine, ikiwemo 36 kwenye mkoa wa mpakani wa Rostov na 17 kwenye mkoa mwingine wa Oryol.

Mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi iliharibu pia droni nane katika anga la mkoa wa Kursk na nyingine 9 kwenye mkoa mwingine wa mpakani wa Belgorod.

Katika miezi ya karibuni, Ukraine imetanua kampeni yake ya mashambulizi ya anga ndani ya ardhi ya Urusi ikisema ni jibu kwa hujuma nzito zinazofanywa kila siku na vikosi vya Moscow katika miji na maeneo mengi ya Ukraine.

Kyiv inatumia stratejia ya kuilenga miji midogo na vijiji kwenye mikoa ya mpakani na Urusi pamoja na kuvishambulia vituo vya nishati inavyosema vinaisaidia Urusi kuendelea na vita.

Related Posts