NMB yaahidi neema Wadau Sekta ya Kilimo ili kunyanyua uzalishaji

Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya KilimoBiashara wa NMB, Nsolo Mlozi, alipozungumza katika banda la benki hiyo kwenye Maonesho ya 31 ya Kilimo ya Nane Nane, yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini hapa.

NMB ni miongoni mwa wadhamini wenza wa Maonesho hayo ya Kitaifa na yale ya Kanda, yanayofanyika chini ya kaulimbiu isemayo: Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Akizungumza katika Banda la NMB lililoko kwenye Hema la Wadhamini wa Maonesho, Mlozi alisema Kilimo, Ufugaji na Uvuvi ni mnyororo wa thamani wa kimkakati, unaohitaji sio tu nguvu za Serikali, bali sapoti ya wadau wote ili kukuza uzalishaji na kuongeza tija kwa taifa.

“Tuko hapa kwa namna mbili, kwanza ni wadhamini wa Maonesho ya Kitaifa na ya Kanda zote nane nchini, pili NMB tunashiriki kama wadau wakubwa wa kilimo, sekta inayojumuisha kilimo chenyewe, ufugaji, uvuvi na misitu.

“Katika kunyanyua na kukuza uzalishaji, ili kuongeza mchango wa sekta hii katika Pato la Taifa, NMB ilikuwa ni benki ya kwanza nchini kutoa mikopo nafuu ya asilimia 9 ya riba kama Serikali ilivyoagiza miaka miwili iliyopita,” alisema Mlozi.

Aliahidi ya kwamba, benki yake itaendelea kuwa bega kwa bega na Serikali katika kunyanyua kiwango cha uzalishaji kwa wakulima nchini, kupitia mtandao mpana unaojumuisha matawi matawi 231 yaliyotapakaa kote Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.

“Kupitia Mameneja wa Matawi na Mameneja Mahusiano wa Kanda, tumejipanga kuwafikia kila mmoja miongoni mwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wazalishaji wa Mazao ya Misitu, ambao moja ya changamoto zao ni kufikiwa na Taasisi za Fedha,” alisisitiza.

Sambamba na hilo, Mlozi alisema wanayo NMB Foundation, ambayo ni taasisi isiyo ya kibiashara, inayotoa elimu kwa wadau wa Kilimo ambao wanaelimishwa na kuongezewa uwezo wa kufahamu njia bora za kilimo chenye tija kwao na taifa.

“Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kilimo cha umwagiliaji kimekuwa muhimu zaidi, kwani kilimo cha kutegemea mvua kimepitwa na wakati, lakini pia tunazo Bima Nafuu za Kilimo na Mifugo, ili kuhakikisha wadau wanaepuka majanga katika uzalishaji wao,” aliongeza Mlozi.

Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Bi. Janeth Shango, aliwataka wakazi wa wadau wa kilimo mkoani Dodoma na wakulima kote nchini kutumia fursa ya uwepo wa maonesho ya Kitaifa na Kanda, ikiwemo mikopo ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao.

“Banda letu hili linatoa huduma sawa na tawi, kwahiyo wakija hapa watajua huduma zetu, watapa elimu ya bima za kilimo na mikopo ya pesa na zana za kilimo ikiwemo matrekta, ‘power tiller’ na pembejeo mbalimbali,” alisema Bi. Janeth Shango.

“Hapa Dodoma kwa mfano tuna wakulima wa alizeti, zabibu, mpunga, mahindi, kuna fursa mbalimbali hapa wanazoweza kunufaika nazo, tunatoa wito kutembelea banda letu na kwenye matawi yote ili kujiongezea tija katika kilimo chao,” alibainisha.

Naye Rehema Athanas Mlowe, ambaye ni mkulima wa mahindi na mnufaika wa mikopo nafuu ya NMB, alisema kwa kipindi chote alichotumia huduma za benki hiyo, amepata mafanikio makubwa, anayotamani kuona kila mkulima anayapata.

“Nimefika hapa nikiwa mmoja wa wanufaika wa huduma zao, awali sikuwa na mafanikio kutokana na aina ya kilimo changu, lakini kupitia mkopo wa pesa taslimu na zana za kilimo kutoka NMB nimefanikiwa kukuza mtaji, kuongeza mashamba na mavuno yangu.

“Mafanikio niliyopata kupitia huduma za NMB, ndio anayostahili kupata mkulima yeyote nchini, ndio maana nawatoa wasiwasi kwa kuwahimiza kutembelea matawi ya NMB ili kuwezeshwa kimtaji na kuachana na kilimo cha kizamani, kisicho rafiki,” alisema.






Related Posts