Rais Samia ataja kitakachowaingiza Gen Z barabarani

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kutokuwepo kwa chakula ndiko kutawafanya vijana wa kizazi cha Z maarufu Gen Z, waingie barabarani.

Mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo wakati akielezea umuhimu wa Serikali kusimamia masilahi ya makundi yote katika jamii.

Ameyasema hayo leo Jumamosi, Agosti 3, 2024 alipozindua bwawa la umwagiliaji la Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani Morogoro,  ambao ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini.

Amesema inapoonekana Serikali imeegema upande wa kundi linaloonekana kukosa nguvu haimaanishi ina masilahi huko, bali ni katika msingi wa kutekeleza jukumu la kutetea masilahi ya wote.

“Wanasema chakula ni siasa, kukiwa hakuna chakula ile Generation Z haitatulia itaingia barabarani, au ukiwapandishia sukari kilo kwa Sh7, 000 hawatatulia,” amesema.

Amesisitiza kuwa Serikali inayosimamia kundi la wananchi wanaotaka sukari kwa bei ya uhakika na himilivu, msingi wake ni huo.

Sambamba na hayo, Rais Samia amewasihi wawekezaji kuendelea kuwekeza kwenye teknolojia na mbinu za kisasa katika uzalishaji ili kupunguza gharama na kuongeza tija zaidi.

Ameahidi kufanyia kazi ombi la ujenzi wa barabara ya Wami – Dakawa – Madizini lililotolewa na kiwanda cha Mtibwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali inatoa Sh220 bilioni ikiwa ni misamaha ya kodi katika seta ya sukari.

Misamaha hiyo, amesema inalenga kuhakikisha sekta ya sukari nchini inaimarika, huku uzalishaji ukiongezeka.

Kwa mujibu wa Bashe, Serikali kwa sasa inaandaa Sera ya Taifa ya Fedha katika sekta ya kilimo ili kuhamasisha uwekezaji wa muda mrefu.

Amesema mahitaji ya sukari nchini kwa sasa ni tani 650,000, lakini matarajio ya uzalishaji mwaka huu ni tani 550,000.

Lakini, kufikia mwaka 2026, amesema uzalishaji unatarajiwa kufikia tani 750,000, huku mwaka 2030 ukifika tani milioni moja.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Mtibwa, Seif Ally Seif amependekeza kuboreshewa barabara kutoka Wami-Dakawa hadi katika eneo la kiwanda.

Kadhalika, amependekeza kuwepo mazingira wezeshi yanayohamasisha uwekezaji na taasisi za fedha ziongeze ukopeshaji.

Lakini yote hayo, amesema yatapaswa kubebwa na uwepo wa sera zinazotabirika za uwekezaji.

Ameeleza katika mradi wa upanuzi wa mradi huo, mitambo 47 imeshafungwa na mradi utakapokamilika itafikia 112.

Amesema uwekezaji umefanyika kwa kuweka mitambo mipya kiwandani na wanachakata miwa tani 180,000 kwa saa, wakitarajia kufikia tani 230,000 mwaka 2027.

Related Posts