RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewatumia salamu Simba SC na kuwatakia kila la kheri katika msimu wa 2024-2025 huku akiwapa ujumbe wa upambanaji.
Katika salamu zake hizo, Rais Samia ambaye mwaka jana alikuwa mgeni rasmi kwenye Simba Day huku mwaka huu akishindwa kuhudhuria akibainisha kwamba alikuwa na ziara ya kikazi, amewataka Wanasimba kusahau yaliyopita na kuangalia yajayo.
Rais Samia amefikisha salamu hizo kwa njia ya simu wakati akizungumza na Wanasimba waliofika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam katika kilele cha Simba Day.
Kupitia simu ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, Rais Samia amesema anafuatilia tamasha hilo kupitia runinga baada ya kurejea akitokea kwenye ziara ya kikazi.
“Nawashukuru sana, nimerudi ziara sasa hivi nimefungua TV nimeona uwanja umejaa na shughuli zinaendelea. Nakumbuka mwaka jana tulikuwa sote hapo lakini mwaka huu limenipita lakini nikaona lisinipite kabisakabisa mpaka niongee nanyi.
“Mimi nawapongeza sana sana mmefanikisha vizuri siku ya Simba, najua mnajipanga vyema kwa msimu ujao na najua mmesajili vizuri. Wanasema yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
“Kwa hiyo mimi niwatakie kila la kheri,” alisema Rais Samia.
Simba kuelekea msimu ujao imefanya usajili wa wachezaji wapya 14 wakiwemo nane wa kimataifa na wazawa sita ikiwa ni katika kuimarisha kikosi chao ili kuanza tena kubeba makombe ya Ligi Kuu na FA baada ya kuyakosa kwa takribani misimu mitatu mfululizo.