Safari ya Mwabukusi TLS ilikuwa ngumu kama Lissu

Dar es Salaam. Licha ya milima na mabonde aliyopitia wakili Boniface Mwabukusi, magumu hayo hayakumzuia kushinda urais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).

Misukosuko aliyopitia mbali na kuwekewa pingamizi na hatimaye kuenguliwa asigombee urais huo, pia amekumbana na matukio ya kukamatwa na polisi, kushtakiwa kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili na kupewa onyo, masuala ambayo yamefanya jina lake liwe maarufu zaidi ya wagombea wenzake. 

Aliyoyapitia kabla na wakati wa mchakato huyo, yanatwajwa kuwa  yalimjengea umaarufu uliomwezesha kushinda uchaguzi wa chama hicho uliofanyika Dodoma Agosti 2, 2024.

Katika uchaguzi huo, Mwabukusi amepata kura 1,274 kati ya 2,218 zilizopigwa, akiwashnda wagombea wenzake watano, akifuatiwa na Sweetbert Nkuba aliyepata kura 807.

Wagombea wengine katika uchaguzi huo na kura zao kwenye mabano ni Ibrahim Bendera (58), Paul Kaunda (51), Emmanuel Muga (18) na Revocatus Kuuli (7).

Aliyoyapitia Mwabukusi yanafananishwa na waliyopitia baadhi ya marais wa TLS, akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na Fatma Karume anayesema hali hiyo hutokana na kuikosoa Serikali.

Mwabukusi aliyeapa leo Agosti 3, mbele ya Wakili Mwandamizi Dk Mkunga Mtingele jijini Dodoma, atakuwa madarakani kwa miaka mitatu hadi mwaka 2027.

Njia walizopita Lissu, Fatma

Mwabukusi anaonekana kupita njia walizopita Lissu na Fatma ambao walipitia misukosuko kuufikia urais wa TLS.

Mwabukusi ambaye pia ni mwanasiasa alipata umaarufu alipojitokeza hadharani kupinga mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na ile ya Dubai kuhusu uwekezaji wa bandari unaotekelezwa na kampuni ya DP-World.

Pamoja na mawakili wenzake, walifungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, lakini walishindwa kesi hiyo.

Aliwahi kukamatwa akiwa njiani kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam na kurejeshwa Mbeya alikowekwa mahabusu baadaye aliachiwa bila masharti.

Julai 31, 2023, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alimfikisha Mwabukusi mbele ya Kamati ya Maadili ya Mawakili akidaiwa kutoa kauli ya utovu wa nidhamu kwa viongozi wa Serikali.

Mei, 2024 kamati hiyo ilimtia hatiani na kumpa onyo.

Alipogombea urais TLS, Mwabukusi nako alikumbana na misukosuko. Siku moja kabla ya kuanza kwa kampeni za urais, kamati ya rufaa ya TLS ilimwengua kuwania nafasi hiyo akiwa ameshapitishwa na Kamati ya Uchaguzi.

Kilichotajwa kama sababu ya kuenguliwa kwake ni kupitia rufaa ya mmoja wa mawakili, ni onyo alilopewa na Kamati ya Maadili ya Mawakili, suala ambalo alilipinga kortini na mahakama ikabatilisha uamuzi uliomwengua na kurejesha jina lake miongoni mwa wagombea.

Mapito hayo yanaweza kufanana na aliyopitia Lissu alipotangaza kugombea urais mwaka 2017, kwa kuwa naye almanusura ashindwe kuhudhuria uchaguzi huo.

Kwanza, uchaguzi huo uliwekewa pingamizi mahakamani na Lissu akaomba kuingia kama mnufaika, na baadaye pingamizi hilo lilitupwa.

Zikiwa zimebaki siku mbili kabla uchaguzi huo, Lissu alikamatwa na Polisi jijini Dodoma Machi 16, 2017 na alisafirishwa hadi Dar es Salaam, akidaiwa kukiuka masharti ya dhamana ya kesi moja ya kisiasa.

Machi 17, 2017 alifikishwa mahakamani ambako, licha ya dhamana yake kupingwa, mahakama ilimpa dhamana akasafiri kwenda Arusha kuwahi Machi 18, 2017.

Baada ya uchaguzo huo uliompa ushindi mkubwa, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alinukuliwa akitishia kuifuta TLS kwa madai kuingiza siasa katika majukumu yake.

Hata hivyo, Lissu aliiongoza TLS kwa miezi mitano tu, kabla ya kushambuliwa kwa risasi akiwa anaingia nyumbani kwake jijini Dodoma Septemba 7, 2017 na baada ya hapo alikwenda kutibiwa jijini Nairobi, Kenya na baadaye nchini Ubeligiji na hakuwahi kujihusisha na masuala ya TLS hadi uchaguzi wa mwaka huu.

Baada ya uongozi wa Lissu, Sheria ya TLS ilibadilishwa na kuzuia viongozi wa siasa wakiwamo wabunge na madiwani kugombea uongozi kwenye chama hicho.

Aprili 2018, wanachama wa TLS walimchagua Fatma Karume kuwa rais wao. Fatma ni mwanaharakati na alikuwa mkosoaji wa mara kwa mara wa Serikali.

Katika kipindi chake cha urais, misuguano kati ya TLS na Serikali pia iliendelea na hasa pale ilipoonekana kana kwamba chama kimebeba sura ya uanaharakati, hata baada ya uongozi wake.

Septemba 20, 2019, Fatma alisimamishwa uwakili na Mahakama Kuu kwa madai ya kuishambulia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na alifikishwa mbele Kamati ya Maadili ya Mawakili kujadiliwa. Kamati hiyo ilimfutia uwakili, hata aliporejeshewa mahakama hadi sasa hajarudishiwa leseni yake ya uwakili.

Akieleza sababu za misukosuko kwa wanasheria hao, Fatma amesema ni kwa sababu ya kuikosoa Serikali.

“Mwabukusi kaingia kwenye misukosuko kwa sababu alikuwa anaikosoa Serikali. Alivyoingia kwenye kinyang’anyiro cha urais wa TLS, hapo sasa ndio wakaanza kumfanyia rafu, kujaribu kumwengua asiingie.

“Alipoingia kwenye kinyang’anyiro na akaondolewa ni mwendelezo wa ile misukosuko,” amesema Fatma.

Fatma amesema yeye bado anapitia misukosuko hata leo kwa sababu bado hajapewa leseni yake.

“Mpaka leo mimi bado napitia misukosuko kwa sababu bado hawajanirejeshea leseni yangu.”

Hata hivyo akizungumzia hali hiyo, Wakili Mpale Mpoki amesema misukosuo hiyo ni ishara ya kukomaa hasa kwenye kujumuika na haki ya kuchagua kiongozi unayemtaka.

“Sasa katika jamii yoyote ni lazima kuwe na mvutano wa masilahi, ndio maana kunakuwa na misukosuko.

“Pili hakuna kitu ambacho wananchi wanafuatilia sana kama uchaguzi wa TLS kwa sababu ya mvutano wa masilahi na kwa sababu majukumu ya chama ni kuwa mshauri mkuu wa masuala ya sheria kwa Bunge, Serikali na umma.

“Kama mshauri mzuri mara nyingi anasema ukweli, sasa akisema hivyo ndivyo inaonekana kama anaikosoa Serikali, lakini si kwamba anakosoa bali anashauri,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi Agosti 3, 2024, Mwabukusi amesema katika uongozi wake atajikita kwenye kifungu cha 4 cha Sheria ya TLS kukirudisha chama hicho kwenye misingi yake.

“Kama nilivyosema, mimi naanza na kifungu cha 4 cha Sheria ya TLS kuirudisha TLS kwenye misingi yake ili kuhakikisha chama kinatekeleza wajibu wake,” alisema.

Kifungu hicho, kinaeleza malengo ya chama ambayo ni kuwaunganisha, kuwatetea na kusaidia ustawi wa mawakili nchini.

Pili, kina wajibu wa kuishauri Serikali na vyombo vyake kama Bunge na Mahakama. Jukumu jingine ni kusimamia masilahi na ustawi wa jamii ya Watanzania.

Mwabukusi amejipambanua kuwa wakili wenye msimamo na kupigania haki na masilahi ya wananchi kupitia majukwaa mbalimbali aliyowahi kushiriki ikiwemo mikutano ya hadhara.

Alipoulizwa jinsi atakavyoshirikiana na viongozi wa Serikali, akitajwa kwa tabia ya ukali, Mwabukusi amesema licha ya kuwa na tabia hiyo atazingatia sheria.

“Watu wanavyosema nina confrontation (jazba) ni kama ninafanya mambo kwa hisia zangu. Hii ni taasisi na mimi huwa naongozwa na kanuni, sheria na Katiba, hayo ndiyo maisha yangu siku zote.

“Pia siku zote huwa nimezoea kulitamka jambo kama lilivyo, kama ni zuri nitalimka jinsi lilivyo na kama ni baya nitalitamka vivyo hivyo, kwa hiyo siyo kupinga kama watu wanavyosema,” amesema.

Amesema katika mapambano yake amekuwa akitumia mahakama kudai haki zake ikiwa ni pamoja na kwenda mahakamani. 

Ametoa mfano alipogombea ubunge katika jimbo la Busokelo mwaka 2020 akidai kuwa alidhulumiwa katika uchaguzi huo baada ya kuambiwa matokeo yake hayakujumlishwa.

“Nilikuwa na kundi kubwa la watu na ningeweza kuwaambia wafanye lolote, lakini niliondoka nikaenda mahakamani, nilikuwa Mtanzania pekee aliyegombea na niliyekwenda mahakamani.

“Kudai haki yako siyo utovu wa nidhamu lazima watu waelewe. Wakati nakukemea siyo confrontation, hata nikikupongeza sijakuogopa.

“Wakati wa kupongeza ninakupongeza, wakati wa kukemea nakemea, wakati wa kubomoa nabomoa, wakati wa kuvunja navunja na wakati wa kujenga najenga, nazungumza lugha inayotokana na tukio husika,” amesema.

Licha ya kufuata sheria, Mwabukusi amesema ataendeleza misimamo yake bila kuogopa vyeo vya watu.

“Mimi mjinga nitamkemea, sitakuogopa hata kama una cheo, lakini ikija kwenye courtesy (heshima) tutafanya. Nchi haiendeshwi kihuni, inaendeshwa kwa sheria, Katiba na kanuni,” amesema.

Related Posts