Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka halmashauri zote nchini kuwasimamia wenyeviti wa serikali za vijiji kuwa watatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji badala ya kuwa wepesi wa kunyoosha mikono kupokea fedha.
Amesema kufanya hivyo, kutawezesha kukabili migogoro ya wakulima na wafugaji katika wilaya mbalimbali nchini.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumamosi, Agosti 3, 2024 alipozindua programu ya ‘Tutunzane’ inayolenga kuwaweka pamoja wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Mvomero, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani Morogoro.
Amesema malalamiko yaliyopo ni uongozi wa vijiji kuwa wepesi wa kunyoosha mikopo kupokea fedha, badala ya kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
“Mamlaka za mikoa na wilaya hakikisheni yeyote atakayeingilia uhuru wa mwenzake kwa kuingiza mifugo kwenye shamba lake, mnamchukulia hatua,” amesema.
Katika hotuba yake hiyo, amesema programu ya Tutunzane itaepusha migogoro na kutunza amani kwa wakulima na wafugaji wa maeneo mbalimbali.
Pia, ameeleza itaongeza wigo kwa wakulima na wafugaji wa kukopesheka kupitia hati watakazozipata.
Amesema wakulima na wafugaji ni kama watoto waliozaliwa kwenye familia moja, kwa kuwa wanategemeana.
Amesema nchi huwa na nguvu zaidi iwapo kutakuwa na umoja, kwani migogoro husababisha machafuko.
Katika maelezo yake, amerejea Katiba ya Tanzania inayomtaka kila mmoja afanye mambo yake bila kuingilia haki ya mwingine.
Ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inatafuta wadau hasa wa sekta binafsi, kuwekeza kwenye programu hiyo ya kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji
Hata hivyo, amesema ni vigumu kuyaepuka mabadiliko ya namna ya kulima na kufuga kwa sababu ardhi haiongezeki huku binadamu wanaongezeka.
“Lazima tuwe wabunifu wa kuja na mbinu zitakazofanya ardhi tuliyonayo izalishe zaidi. Kama ni mkulima azalishe zaidi kwa kipande cha ardhi alichonacho vivyo hivyo kwa mfugaji,” amesema.
Ametaja uwepo wa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, akisema teknolojia za kisasa ni muhimu kuhakikisha wanalima, kufuga na kupata mazao ya kutosha.
Awali, akizungumzia programu hiyo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema wakulima 1,066 wamesajiliwa.
Hata hivyo, amesema Sh70 milioni imeombwa na Halmashauri ya Mvomero kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
“Tayari nimeshamwelekeza Katibu Mkuu (Gerald Mweli) kuangalia fedha hiyo na kuifikisha kwa halmashauri hiyo kwa ajili ya kutekeleza programu,” amesema.
Akizungumza katika tukio hilo, Mbunge wa Mvomero, Jonas Zeelan ameomba kujengwa kwa kilomita 25 za barabara ya Magole kwenda Mvomero.
Amesema barabara hiyo inauunganisha Mkoa wa Morogoro na Tanga hivyo anaomba ijengwe kwa kiwango cha lami.
Pamoja na barabara hiyo, Zeelan ameomba Mvomero iwe moja ya maeneo yatakayonufaika na mradi wa maji unaotarajiwa kuhudumia Morogoro Mjini.
Kadhalika, Mbunge huyo ameeleza uwepo wa changamoto ya tembo katika Tarafa ya Mlari, akisema inawalazimu wananchi waishie kulima ufuta pekee.
“Naomba wale tembo warudishwe hifadhini na kujengwe ukuta utakaozuia wasitoke hifadhini na kuja katika mashamba ya wakulima,” amesema.
Ombi lake kuhusu kunufaika na mradi wa maji, lilijibiwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akisema mradi huo hautafika Morogoro Mjini kabla haujawanufaisha wakazi wa Mvomero.
Kuhusu barabara, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema ujenzi umeshaanza kwa upande wa Tanga na kwamba itafika hatua kipande hicho nacho kitajengwa.