Dar/Moshi. Serikali imetoa tahadhari kwa wananchi kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa wa homa ya nyani (Mpox) unaosambaa kupitia majimaji ya mwili ikiwemo mate, matapishi, jasho na mkojo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo unasababishwa na virusi vya Mpox vinavyoweza kusambaa kwa njia za matone ya mfumo wa njia ya hewa, ngozi kupitia kugusa na kujamiana na mtu mwenye maambukizi. Pia, ugonjwa huo unaweza kueneza kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Agosti 3, 2024 na Wizara ya Afya imeeleza kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa za ongezeko la wagonjwa na vifo kutokana na ugonjwa huo katika baadhi ya nchi za jirani za Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Hata hivyo, Wizara ya Afya imefafanua kuwa hadi sasa Tanzania ni salama na hakuna mgonjwa yeyote aliyepatikana na ugonjwa huo ambao dalili zake ni upele, malengelenge au vidonda kwenye mwili hasa mikononi na miguuni, kifuani, usoni na wakati mwingine sehemu za siri.
“Dalili nyingine ni homa, maumivu ya kichwa, misuli, mgongo, uchovu na kuvimba mitoki. Ugonjwa huu haujaingia nchini, hivyo, ni vema tukashirikiana kuhakikisha nchi yetu inabaki kuwa salama,” imeeleza taarifa ya wizara hiyo.
Kutokana na hilo, Serikali imewataka Watanzania kuepuka kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana na kubusiana na mtu mwenye dalili za Mpox.
Serikali pia imewataka wananchi kuepuka kugusana na mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox, na kunawa mikono kila mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
Pia, wametakiwa kuepuka kula au kugusa mizoga au wanyama mfano nyani au swala wa msituni, kusafisha na kutakasa vyombo vilivyotumika na mhisiwa au mgonjwa pamoja na maeneo yote yanayoguswa mara kwa mara.
“Kuvaa barakoa iwapo itabidi kukaa na kuongea kwa karibu na mtu mwenye dalili za Mpox, kuwahi katika vituo vya huduma za afya unapoona dalili za ugonjwa wa Mpox. Watoa huduma za afya kuzingatia miongozo ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi (IPC) wakati wote wanapowahudumia wagonjwa,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkoa wa Kilimanjaro umechukua tahadhari za kudhibiti ugonjwa huo katika vituo vya mpakani vya Holili na Tarakea, baada ya ugonjwa huo kuwapo Kenya.
Taarifa za WHO zinaeleza kuanzia Mei 2022 ugonjwa huo ulipoanza hadi Mei 31, 2024 wagonjwa 97,745 na vifo 203 vimetolewa taarifa kutoka nchi 116 duniani.
Mwananchi imeshuhudia utaratibu wa watu kunawa mikono na kupima joto la mwili kwenye vituo hivyo.
Jana Agosti 2, 2024 imeshuhudiwa utaratibu wa kunawa mikono kwa wasafiri, watumishi na wananchi wa kawaida katika vituo hivyo ukipewa kipaumbele.
Msimamizi wa shughuli za afya katika Kituo cha Forodha Holili, Kasele Koba amesema moja ya tahadhari wanazozichukua ni pamoja na kuimarisha ukaguzi kwa wasafiri wote wanaoingia katika kituo hicho na kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo.
“Tahadhari ambayo tumechukua katika mpaka wa Holili ni pamoja na kuimarisha ukaguzi kwa wasafiri wote wanaoingia na hasa kwa suala zima la kunawa mikono kabla ya kupata huduma kwenye jengo hili na kupima joto mwili,” amesema Koba.
Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala amesema wilaya hiyo ipo salama na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
“Natoa wito kwa wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida wawe na amani, wachukue tahadhari katika maeneo yote ya mpakani na wakiona mtu yeyote mwenye dalili watujulishe tutatuma wataalamu mpakani kuangalia,” amesema.
“Tunaendelea kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi na kuwapa imani kuwa wako salama ila wakiona kiashiria chochote wasisite kutoa taarifa ili watalaamu wazifanyie kazi,” amesema.
Baadhi ya wananchi waliokuwa wakipita katika mpaka wa Holili wamesema wameendelea kupewa elimu kuhusu namna ya kuchukua tahadhari wanapoingia katika maeneo hayo.
Seleman Iddy, dereva kutoka nchini Burundi amesema wamepewa elimu kuhusu ugonjwa baada ya kufika Holili, wakisisitizwa kunawa mikono na kuepuka kupeana mikono.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Jairy Khanga alisema wameendelea na ufuatiliaji katika maeneo ya mipakani ambako timu za afya zimejipanga vizuri na kila mtu anayeingia nchini anakaguliwa.