Serikali yatangaza ajira mpya | Mwananchi

Dar es Salaam. Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira Utumishi wa Umma, imetangaza ajira 6,257 za kada mbalimbali.

Kada za ununuzi, udereva, ofisa kilimo, wasaidizi wa kumbukumbu, uhasibu, waandishi waendesha maoni, maofisa maendeleo ya jamii na wasaidizi wa hesabu ndizo zenye nafasi nyingi za ajira.

Nafasi za ajira zimetangazwa leo Agosti 3, 2024 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma makao makuu jijini Dodoma na mwisho wa kuomba nafasi hizo ni Agosti 16, 2024.

Kwenye mchanganuo, Ofisa ununuzi daraja la (II) nafasi zilizotangazwa ni 350, madereva daraja (II) nafasi 514, maofisa kilimo wasaidizi daraja (II) nafasi 481, nafasi 350 za mwandishi mwendesha maoni daraja (II).

Nafasi zingine ni ofisa maendeleo ya jamii msaidizi 327, ofisa hesabu daraja la (II) nafasi 380, mhasibu daraja la (II) nafasi 350, msaidizi wa kumbukumbu daraja (II) nafasi 382.

Mbali na kada hizo, zipo nafasi 42 za msaidizi wa ufugaji nyuki daraja (II), wapima ardhi nafasi nne, maofisa uvuvi daraja la (II) nafasi 90, maofisa wanyamapori daraja (II) ajira 117, kada ya usafirishaji ajira 56, maofisa utalii daraja la (II) ajira 27, maofisa ushirika daraja (II) nafasi 27 na maofisa kilimo daraja la (II) nafasi 105.

Nafasi za ajira 447 kwa maofisa kilimo wasaidizi daraja la tatu, ofisa habari daraja la pili nafasi 63, maofisa ununuzi wasaidizi daraja la (II) nafasi 120,  wapishi daraja (II) nafasi 78, ofisa utamaduni nafasi sita.

Vilevile wahifadhi wanyamapori daraja (II) watu sita, maofisa michezo daraja la (II) nafasi 29, maofisa utumishi daraja (II) nafasi 95, maofisa ufugaji nyuki daraja la (II) nafasi 32.

Msaidizi wa mifumo daraja la (II) nafasi 182, mchumi daraja la pili nafasi 138, mtakwimu daraja la (II) nafasi 128 na ofisa Tehema msaidizi daraja (II) nafasi 64.

Wamo maofisa biashara daraja (II) nafasi 193, mhandisi ujenzi daraja la (II) nafasi 85, msanifu majengo daraja (II) nafasi 63, msaidizi wa hesabu daraja la (II) nafasi 200.

Idara nyingine ni wahandisi kilimo daraja (II) nafasi 30, nafasi ya ofisa ustawi msaidizi daraja la (II) ajira 229, msaidizi wa hesabu daraja la kwanza nafasi 150 na fundi sanifu-kilimo daraja la (II) nafasi 40, mkadiriaji ujenzi daraja (II) nafasi 30 na ofisa mazingira nafasi 119.

Kwa waombaji ambao tayari ni watumishi wa umma na wamejipatia sifa za kuingilia katika kada tofauti na walizonazo, wametakiwa wapitishe barua zao za maombi ya nafasi za kazi kwa waajiri wao na waajiri wajiridhishe ipasavyo.

Akizungumza na Mwananchi, Said Said ambaye ni mhitimu wa shahada ya awali ya uchumi tangu mwaka 2019 amesema nafasi hizo za ajira zilizotangazwa na Serikali zimewapa matumaini pengine wanaweza kunufaika na nafasi hizo.

“Kwa sisi ambao tuna muda mrefu mtaani bila ya ajira hii kwetu ni habari njema ambayo vijana tunatakiwa kuchangamkia kujaribu bahati yetu,” amesema.

Shani Shabani, mhitimu wa shahada ya uhasibu mwaka 2018 anasema nafasi hizo zitasaidia kupunguza vijana ambao wamehitimu na bado hawajafanikiwa kupata ajira au uwezo wa kujiajiri.

Waziri Kivuli wa Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Vijana, Kazi na Ajira kutoka chama cha ACT- Wazalendo, Petro Ndolezi amesema nafasi za ajira zilizotolewa na Serikali zitakwenda kupunguza kwa kiasi kidogo changamoto ya ajira.

Amesema hiyo inatokana na kuwa nafasi zilizotolewa ni chache ukilinganisha na uhitaji halisi wa ajira kwa vijana.

Ameshauri ili nafasi za ajira ziweze kuzalishwa kwa wingi Serikali inatakiwa kuendelea kuboresha sera na mazingira rafiki zaidi ya uwekezaji katika sekta ambazo zinaweza kuzalisha kiwango kikubwa cha ajira, akitoa mfano wa sekta za kilimo na uchimbaji wa madini.

“Ili wawekezaji waweze kuvutiwa kuwekeza zaidi katika maeneo hayo na vijana wenye mitaji kujiajiri katika sekta hizo na hatimaye kuwezesha ajira zaidi kuzalishwa,” amesema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mchumi, Oscar Mkude ambaye amesema nafasi zilizotolewa zitapunguza changamoto hiyo kwa uchache.

Ametoa wito kwa wenye sifa zilizoanishwa kujitokeza kuomba fursa hizo na kuachana na dhana ya kuwa nafasi za ajira zikijitokeza watu wanapeana.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus amesema nafasi hizo zitakwenda kusaidia kupunguza changamoto ya watumishi katika ofisi mbalimbali za umma.

Related Posts