Simba Day 2024, Ubaya Ubwela

ILE siku ndio leo. Kilele cha wiki ya Simba kitafanyika Wanasimba zaidi ya 60,000 watakutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kukamilisha vaibu lao la kuukaribisha msimu mpya chini ya kauli mbiu ya Ubaya Ubwela.

Ndio siku ya furaha zaidi kwa Wanasimba. Saa chache zijazo wanakwenda kushuhudia furaha mpya baada ya kupitia miezi kadhaa ya machungu na karaha za kutoona ladha ya pira biriani waliyoizowea.

Ukiachana na mengine yote shauku ya Wanasimba leo ni kushuhudia usajili mpya. Unafananaje? Hawataki kuhadithiwa maana katika karata waliyoicheza viongozi ni kuficha kabisa mechi za maandalizi wakiwa kambini Misri zisionekana laivu mpaka walipomaliza.

Lakini vilevile mashabiki wanataka kuona kikosi chao cha kwanza kinafananaje? Nani anafanya nini? Ingawa za ndani ni kwamba mastaa wengi wapya huenda wasijiachie sana na watatumika muda mfupi kuficha silaha za mechi ya dabi Agosti 8.

Hata umoja wa vigogo na kurejea kwenye usukani kwa tajiri Mohammed Dewji kumeongeza hamasa kwa mashabiki hao pamoja na watani wao kupata shauku ya kuona inakuwaje, wamejipangaje? Ingawa hata kauli mbiu ya ubaya ubwela imekuwa na msisimko wa aina yake na kufanya mashabiki kulihodhi tamasha la leo.

Mageti ya Uwanja wa Benjamin Mkapa yatakuwa wazi kuanzia saa 3:00 asubuhi kuwaruhusu mashabiki waliokata tiketi kuanza kuingia huku wengi wakionekana kujivunia zaidi uzi wao mpya ambao safari hii umetoka mapema zaidi ya kipindi cha nyuma hivyo kufanya wengi kuchukulia kama mtoko wao.

Mashabiki tangu juzi walianza kutamba baada ya kutangaziwa tiketi za tamasha hilo zimemalizika, pamoja na yote kikubwa kinachowapeleka uwanjani leo ni kupata kiburi cha kuwatambia watani wao Yanga kutokana na kile watakachoshuhudia ndani ya dakika 90 na wanataka kuweka pia rekodi ya kuujaza uwanja mapema kwani kesho ni Mwananchi Day.

Achana na kauli mbiu aliyoibuni ya Ubaya Ubwela ambayo imeshika kasi. Leo mashabiki wanashauku ya kuona anakujaje?Amejipangaje? Kwani ndiye kiongozi aliyekuwa akiwahamasisha tangu msimu umalizike. Tamasha lililopota Ahmed aliingia uwanjani akiwa na ngamia kisha akavutia kwa ile “Wanasiiimbaaaaa” iliyoteka vibaya.

Safari hii acha tusubiri kuona ataingiaje.

Utamu zaidi wa tamasha hilo utakuwa ni utambulisho wa wachezaji watakaoiwakilisha Simba kuelekea msimu ujao ikiwa na mastaa wapya 12 waliosajiliwa dirisha hili.

Mastaa wapya ambao wanasubiriwa kwenye utambulisho huo ni Kelvin Kijiri, Yusuf Kagoma, Karaboue Chamou, Valentin Nouma, Deborah Fernandez, Augustine Okejepha, Valentino Mashaka, Abdulrazack Hamza,  Jean Ahoua, Steven Mukwala, Joshua Mutale na Moussa Camara aliyetambulishwa jana mchana.

Kitu ambacho kitavutia wengi kwenye utambulisho huu wa wachezaji ni namna msemaji wa klabu hiyo Ahmed Ally atatumia maneno ya mbwembwe na yenye kukera kuwatambulisha wachezaji hao wapya.

Inaelezwa pia baadhi ya wachezaji wa Simba nao watakuwa na mbwembwe zao kwenye kuingia ndani ya uwanja katika utambulisho huo.

Ndani ya tamasha hilo kutakuwa na burudani mbalimbali za muziki ambapo kuna wasanii wasiopungua sita ambao watafanya shoo kali kwenye jukwaa.

Yumo Joh Makini ‘Mwamba wa Kaskazini’, Chino Wana Man, Ally Kiba huku Tundaman alitarajiwa kuthibitishwa jana mchana kuwa sehemu ya watakaotoa burudani.

Msanii Dulla Makabila Simba imemuondoa jina lake kabisa miongoni mwa watakaotoa burudani ikielezwa mashabiki wengi wa wekundu hao wamemkataa kwa kuwahi kuisema vibaya timu yao.

Hapa ndio patamu. Ubaya ubwela ndio uko hapa kuanzia saa 1:30 usiku. Kocha mpya Fadlu Davids kwa mara ya kwanza mbele ya Wanasimba ataupanga mziki wake kukiwasha na APR ya Rwanda.

Simba chini ya Fadlu haijaonekana ikicheza uwanjani hata kwa dakika moja ambapo mechi zao za kirafiki ilizocheza ilipokuwa kambini jijini Ismailia nchini Misri hazikuonyeshwa kokote na kuwafanya mashabiki wa wekundu hao kuwa na kiu kubwa.

APR ambao ni kaimu bingwa wa Kombe la Kagame ndio watakuwa kipimo cha kwanza kwa Simba tangu itue nchini, ukiacha zile ambazo wekundu hao wamezicheza kambini Misri na kushinda zote. Tukutane kwa Mkapa. Ubaya Ubwela.

Kocha mkuu wa APR ya Rwanda, Thierry Hitimana alisema; “Sijaiona Simba yenye wachezaji wapya, kulingana na maandalizi yao ya msimu mpya, waliyoyafanya nchini Misri, ina kocha mpya, hivyo hautakuwa mchezo mwepesi, nautarajia utakuwa wa kimbinu zaidi.

“Ukiachana na hilo, Simba ni klabu kubwa, kitakuwa kipimo kizuri kwetu, kujiandaa na mashindano mbalimbali yaliopo mbele yetu kama Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Hitimana kocha msaidizi wa zamani wa Simba chini ya Didier Gomes.

APR kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, hatua ya awali itakutana na Azam FC, jambo ambalo kocha Hitimana alisema; “Kucheza na Simba itatusaidia zaidi, kwani ina wachezaji ambao wana ushindani wa kimataifa, kulingana na usajili walioufanya.”

Kwa uchambuzi zaidi soma toleo maalumu la Simba Day kuanzia Ukurasa wa 7.

Tabiri kikosi cha leo: 0658-376 417.

Related Posts