SIMBA Queens imeibuka na ushindi wa mabao 7-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mlandizi Queens uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye kilele cha Tamasha la Simba Day.
Katika kikosi hicho cha Simba Queens, kulikuwa na nyota wapya wakiwemo viungo wa zamani wa Yanga Princess, Precious Christopher na Saiki Atinuke.
Mchezo huo uliopigwa kuanzia saa 9 alasiri, Precious aliyejiunga na Simba Queens kipindi hiki cha usajili wa dirisha kubwa, alifanikiwa kufunga bao moja ambapo mashabiki wa Simba walinyanyuka na kumshangilia mchezaji huyo alipouweka mpira nyavuni.
Mabao mengine yalifungwa na Shelida Boniface, Jentrix Shikangwa aliyepachika mawili na mabao matatu ‘hat trick’ kutoka kwa Asha Mwalala.
Ukiachana na viungo hao wawili raia wa Nigeria waliotua Simba Queens, timu hiyo pia imemsajili beki wa kulia kutoka Yanga Princess, Wincate Kaari raia wa Kenya ambaye aliingia kipindi cha pili.
Precious, Saiki na Wincate wakiwa Yanga Princess walikuwa wachezaji tegemeo kwenye timu hiyo iliyomaliza nafasi ya tatu kunako msimamo wa Ligi ya Wanawake msimu uliopita.