Soloka: Simba ni kama Real Madrid 

MDAU wa Simba, Mohammed Soloka amesema mwitikio mkubwa wa mashabiki wa timu hiyo kujaza Uwanja wa Mkapa ni kielelezo cha kiu yao kutaka kuiona timu yao mpya.

Soloka amesema mashabiki wenzake wengi wamefurahishwa na namna uongozi wa klabu hiyo ulivyojenga kikosi kipya chenye wachezaji wengi vijana.

Kigogo huyo amesema wachezaji waliosajiliwa ni wenye vipaji vikubwa wasio na majina makubwa, sera ambayo inatumika hata Real Madrid ya Hispania.

“Watu wamefurahishwa na usajili ulivyofanyika wakati huu, tumekuwa na timu ya wachezaji vijana wasio na majina makubwa. Hii ni sera inayotumika hata kwa Real Madrid ya Hispania ambao ni Mabingwa wa Ulaya,” amesema Soloka.

“Tumekuja kuwaona wachezaji wetu, ndio maana unaona tumeujaza uwanja kwa haraka. Tunaamini kwamba wataturudishia heshima iliyopotea kwa miaka mitatu Sasa.”

Soloka ambaye ni mtendaji Mkuu wa kampuni ya Silent Ocean, ameongeza kuwa timu hiyo imefanya uamuzi mzuri na mgumu kwa kuwaacha wachezaji wenye umri mkubwa bila kujali vipaji vyao.
*****

Related Posts