HIVI karibuni Mwanaspoti liliripoti kuwa Straika wa Simba ametoroka kambini na leo kwenye kilele cha siku ya ‘Simba Day’ mchezaji huyo hajaonekana.
Simba leo inaadhimisha kilele cha Simba Day ambayo iliambatana na burudani mbalimbali za soka ikiwemo mchezo wa Ligi ya vijana U-17 na ule wa kirafiki kati ya Simba Queens na Mlandizi Queens.
Kwenye kikosi cha Simba Queens kilichocheza leo ambacho pia kimetambulisha wachezaji wapya na wale watakaoendelea nao msimu ujao straika huyo, Aisha Mnunka hayupo hata kwenye benchi.
Leo kikosi hicho kilianza na washambuliaji wawili, Jentrix Shikangwa ambaye alifunga bao la kwanza kwenye mchezo huo.
Ukiachana na kutotokea kwenye utambulisho wa wachezaji ambapo Simba Queens imepiga picha na kuwatambulisha wachezaji wake hata kwenye usiku wa tuzo za Shirikisho la Soka TFF hajatokea pale Masaki akichukuliwa tuzo yake na nahodha wa Simba, Violeth Nickolaus.
Kwenye usiku wa tuzo hizo, Mnunka aliondoka na tuzo tatu ile ya mchezaji bora (MVP), mfungaji bora na kuingia kwenye kikosi bora cha mwaka Ligi ya Wanawake.
Mnunka ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu uliopita akiweka kambani mabao 20.