Njombe. Tanzania inatarajia kuanza uzalishaji wa chuma ndani ya nchi katika miaka mitatu ijayo, baada ya kupatikana mwekezaji ambaye atatekeleza mradi huo katika Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe.
Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limeingia mkataba na kampuni ya Fujian Hexingwang Industry Tanzania Co. Ltd, kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya chuma. Mkataba huo umesainiwa leo, Agosti 3, 2024.
Kwa sasa, Tanzania inatumia wastani wa dola za Marekani 1.22 bilioni (Sh3.2 trilioni) kununua chuma kutoka nje ya nchi, ikishika nafasi ya pili kwa matumizi makubwa ya fedha za kigeni baada ya mafuta.
Mkurugenzi wa NDC, Dk Nicolous Shombe, amesema mradi huu wa uchimbaji wa madini ya chuma ni wa kwanza nchini na utachochea maendeleo ya viwanda.
Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya dola 77 milioni, fedha ambazo ni mtaji kutoka kwa wawekezaji na si mkopo.
“Tunatarajia mradi utachukua miaka mitatu, kwa hiyo mwaka 2027 utaanza uzalishaji na wananchi wa pale ambao ni zaidi ya 300, wataanza kulipwa fidia jumla ya Sh4.2 bilioni kabla ya Januari mwakani,” amesema Dk Shombe.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, amesema mikataba inayoingiwa katika uchimbaji wa chuma na makaa ya mawe ni lazima iwe bora na itakayowanufaisha wananchi.
Ameihakikishia jamii ya Mkoa wa Njombe, hususani Wilaya ya Ludewa, kwamba mikataba itakuwa yenye manufaa kwao.
Aliongeza kuwa asilimia 36 ya mradi huo itamilikiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku wawekezaji wakimiliki asilimia 64.
Biteko amesema hawatakubali kuona uongozi wa mgodi au kiwanda kitakachojengwa ukiwa na viongozi wote kutoka nje ya nchi.
Sehemu ya mkataba imeweka wazi kwamba baadhi ya nafasi za uongozi zishikiliwe na Watanzania.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amesema mradi wa Maganga Matitu uliopo wilayani Ludewa una umuhimu mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.
Ameeleza kuwa madini ya chuma yana mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda, na uhakiki uliofanywa mwaka 2020 kwenye mradi wa Maganga Matitu umeonyesha uwepo wa tani milioni 101 za chuma.
Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Dk Yamungu Kayandabila, amesema shirika hilo ni taasisi ya kimkakati katika kuchochea uchumi wa nchi na hata Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, amesema wamejiandaa kuwa mkoa unaoongoza kwa kuweka mazingira nafuu zaidi kwa wawekezaji.
Akizungumzia mradi huo, Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga, amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni kufungua njia ya kuwalipa fidia wananchi wanaopisha mradi huo.